×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Ukulima wa mpunga kwa kutumia maji kidogo wafaulu nchini Kenya

by Isaiah Esipisu | @Andebes | Thomson Reuters Foundation
Monday, 25 March 2013 10:10 GMT

MWEA, Kenya (AlertNet) – Kutokana na upungufu wa vifaa vya umwagiliaji wa maji ya kunyunyuzia mpunga kufuatia mabadiliko katika hali ya hewa na idadi ya watu inayozidi kuongezeka, wakulima wa mpunga katika sehemu nne nchini Kenya wameanza kutumia mbinu mpya ya kukuza mmea huo bila kumwagilia maji msimu wote.

Serikali ya Kenya, kupitia taasisi ya Kilimo cha Unyunyizaji na Maendeleo cha Mwea (MIAD), imeiga mbinu mpya kutoka nchini India ijulikanayo kama Mfumo wa Uimarishaji Mchele, yaani, System of Rice Intensification katika lugha ya kimombo. Hii imebainika kuwa njia mwafaka katika kukuza mpunga kwa kutumia maji kidogo katika katika nchi hii ya Afrika Mashariki

Mfumo huo umetumiwa kwa upana kwa miaka zipatazo kumi kule barani Asia, ambapo imeweza kuimarisha mavuno makubwa. Hivyo basi, ni mara ya kwanza kabisa kwa mfumo huo ulioanzishwa na MIAD kujaribiwa nchini Kenya.

Kutoka jadi, wakulima wa mpunga nchini Kenya wamekuza mmea huo katika sehemu iliyotota maji kutoka wakati wa kupanda hadi wakati wa kuvuna. Hivyo basi, mfumo huu mpya unawatoa kwa mtindo wa zamani na kuwaelekeza kwa mtindo mpya ambapo mpunga unanyunyiziwa maji kidogo, lakini wakati mwingine unawachwa kukauka. Na miche hupandwa kwenye laini huku nafasi pana ikiwachwa kutoka mmea mmoja hadi mwingine.

 Kulingana na Raphael Wanjogu ambaye ni mtafiti mkuu katika MIAD, haikuwa rahisi kushawishi wakulima kuiga mbinu mpya ambayo hawajawahi kuona.

Afisa huyo aelezea kuwa mfumo huo mpya wa kilimo cha mpunga-kwa lugha ya kimombo ijulikanayo kama system of rice intensification(SRI) ni baadhi ya mbinu zinazotumiwa na serikali ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, na pia ni mbinu mwafaka ya kuongeza uzalishaji wa chakula nchini.

Mchele ni mojawapo ya vyakula vikuu nchini Kenya, na inaliwa na jamii zote. Lakini, Kenya huzalisha tani 110,000 kila mwaka, ambacho ni kiwango cha chini zaidi ikilinganishwa na tani 300,000 zinazoliwa na Wakenya kila mwaka. Hayo ni kwa muujubu wa Wizara ya kilimo nchini. Tofauti hiyo hujazwa na mchele inayoletwa kutoka nchi za Asia, hususan Pakistan, Thailand na India.

Mfumo huu mpya unalenga kubadilisha hayo.

KUKABILIANA NA WALIO NA WASIWASI

Moses Kareithi Mwangi ambaye amekuwa akifanya kilimo cha mpunga kwa zaidi ya miaka kumi, ni mmoja wa wakulima waliotanguliza mfumo huo wa SRI nchini Kenya mnamo mwaka wa 2009. Lakini, asema kuwa haikuwa rahisi kwa sababu alipata pingamizi kutoka kwa bibi yake, watoto wake, majirani na hata marafiki.

Bwana huyo alifadhiliwa na serikali kushiriki mpango wa kubadilishana mawazo kule nchini India.

Majirani wake hawangeelewa ni kwa nini alianza kupandikiza miche changa zikiwa na matawi mawili peke yake, na ni kwa nini alikuwa anapanda miche chache, ambapo alikuwa akipanda mche moja kwa shimo badala ya tano ilivyo kawaida.

Lakini kwa kuzingatia mbinu hii mpya, Mwangi alipata mavuno kwa wingi isivyo kawaida. Kutoka ploti ya robo hekta(0.6) ambapo kwa kawaida hutoa mpunga magunia tisa ya maguni o ya kilo 90 kila moja, alivuna magunia 12. Hilo lilisababisha wakulima wengine kuiga mtindo huo mnamo msimu wa kupanda wa mwaka wa 2011 -12.

Kulingana na MIAD, wakulima ambao walipanda kwa kutmia mbinu mfumo wa SRI, walivuna tani tisa za mpunga kwa kila hekta, ikilinganishwa na tani tano walizozivuna wakulima waliotumia mbinu za kawaida.

Kwa wale waliopanda mchele aina ya IR ambayo ina mavuno mengi kwa kutumia mbinu mpya walivuna tani 17 ikilinganishwa na tani kumi zilizovunwa kwa kutumia mbinu za kawaida.

Hivyo basi, Wanjogu anatumahi kuwa kwa kutumia mbinu mwafaka zilizojaribiwa na kudhibitishwa, basi Kenya itaweza kupunguza kiwango cha chakula kinacholetwa kutoka nchi za kigeni.

Ikilinganishwa na mbinu za upanzi wa mchele za kawaida ambapo miche zinapandwa bila mpango, mbinu mpya ya kutoka India inazingatia miche kupandwa kwa laini, na kwa umbali wa sentimita 25 ili kuhakikisha kuwa mimea zinapata mwangaza wa jua na madini ya mchanga ya kutosha. 

Katika mbinu mpya, miche hupandwa zikiwa zingali changa – kati ya siku 8 na siku 15 – badala ya siku 30 ilivyo kawaida.

La muhimu, mbinu hiyo mpya inapinga unyunyizaji wa maji mfululizo katika shamba la mpunga, mbinu ambayo inatumiwa sana kote duniani. Linalohitajika ni kuhakikisha kuwa mchanga una unyevu wa kutosha kila mara.

Wanasayanzi wasema kuwa mbinu hii husaidia kushikilia hewa aina ya oksijeni katika mchanga, jambo ambalo husaidia mizizi za mimea kukua kwa ustadi na pia kutumia madini ya mchanga inavyostahili.

Kulinagana na MIAD, zaidi ya wakulima 2000 kote nchini Kenya tayari wameanza kutumia mbinu hiyo mpya katika sehemu nne za unyinyizaji, yaani Ahero, Kano ya Magaribi, Bunyala na Mwea.

Paul Njoroge Kuria, ambaye ni mmojwapo wa wakulima waliopinga mbinu hii mpya asema kuwa mbinu hiyo ndio njia mwafaka, na kuwa Kenya yahitaji mbinu zingine kama hizo ili kuimarisha uzalishaji wa chakula.

Wataalam wa mazingira wameonya kuwa hali ya hewa inayozidi kuharibika kote duniani itafanya vigumu kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji yanayozidi kuongezeka.

Hii, ndiyo sababu njia za kukabiliana na hali mbaya ya anga zinahitajika ili kuimarisha uzalishaji wa chakula, asema Dkt Evans Kituyi, mtaalam kutoka Shirika la Utafiti wa Maendeleo Kimataifa.

Isaiah Esipisu ni mwandishi wa kujitegemea,huripoti katika maswala ya taaluma ya kilimo na mazingira, mkaazi wa Nairobi.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->