×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Redio yasaidia wakulima kupambana na mabadiliko ya tabia nchi

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Thursday, 22 August 2013 08:58 GMT

A local radio show targeted at farmers in north Tanzania is helping onion and rice growers adapt to shifting weather patterns

KILIMANJARO, Tanzania (Thomson Reuters Foundation) — Wakati maelfu ya wakulima wanakabiliana na athari za ukame zinazotokana na mvua hafifu kaskazini mwa Tanzania, Shirika la Canada likishirikiana na wadau limeanzisha programu ya Redio kusaidia wakulima wa mpunga na vitunguu kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Farm Redio International ikishirikiana na kituo cha redio binafsi MoshiFM, vimeanzisha programu, kusaidia wakulima kata ya Ruvu Wilayani Same na maeneo jirani juu ya kuhifadhi mazao na kutafuta masoko.

 Ikiwa ni mwaka mmoja tu toka kuanzishwa kwake, Kipindi cha Heka-Heka Vijijini kinapeperushwa mara mbili kwa wiki kwa muda saa moja, kufundisha wakulima njia bora za kilimo ikijumuisha kuchanganya aina tofauti ya mazao, umwagiliaji maji katika kuongeza nguvu ya rutuba.

Wakisaidiwa na maofisa ugani, kipindi kinafunza wasikilizaji kutambua msimu maridhawa wa kupanda, pamoja na kuwapa taarifa halisi za hali ya hewa na namna wanaweza kuongeza mazao na  kuepuka changamoto mbalimbali za tabia nchi.

 Kila Jumatano na Jumamosi, Gloria Meena hukaa kitako kusikiliza kipindi hiki akiwa na wakulima wenzake kijijini Ruvu.

“Ni kipindi kizuri sana, kinafunza mbinu bora za kilimo na namna wakulima wanaweza kukabiliana na mafuriko na kustahimili mabadiliko ya tabia nchi” amesema.

 Meena, ambaye ni mjane mwenye umri wa miaka 53 anasema hali ya hewa katika mkoa wao imekuwa haitabiriki kwa kipindi cha miaka minane sasa. Anakumbuka alivyopoteza ekari nzima ya vitunguu miaka mitatu iliyopita baada ya mvua kubwa kupiga kijijini nzima hapo kiasi cha kusababisha mafuriko yaliyosomba kila kitu alichopanda na kumsababishia hasara kubwa.

“Kabla sijaanza kusikiliza kipindi hiki, sikujua kuzuia mmomonyoko wa udongo, ambao ni tatizo kubwa hapa, kupitia kipindi hiki nimejifunza namna ya kutunza shamba langu” alisema Paulina Ngauka, mkulima Ruvu.

 Afisa mtendaji wa MoshiFM Yusuph Masanja alisema HekaHeka vijijini imewalenga wakulima zaidi ya 7,000 wanaotegemea kilimo kwa maisha yao, na kimenuia kuendeleza kilimo bora cha mpunga huku kikielimisha juu ya mabadiliko ya tabia nchi.

“Tumefurahi kuona kwamba mwitiko kutoka kwa wakulima umekuwa mkubwa” alisema.

 

 Masanja alisema redio imerahisisha kazi ya maofisa ugani ambao sasa wanaweza kuwasiliana na wakulima moja kwa moja kwa radio kwa kuwa si rahisi kutembelea kila mkulima.

“Maofisa ugani ni wachache... hivyo tunawapa ukumbi wa kuzungumza na wakuliama na kueneza ujumbe wao,” alisema.

Onesmo Mbaga, Mkulima wa vitunguu Ruvu amesema kipindi hicho kimemfundisha namna bora ya kuhifadhi maji kwa ajili ya matumizi wakati wa kiangazi.

“Mbegu za vitunguu hazihitaji maji mengi kukua,” Mbaga alisema. “Nimetengeneza tanki nikisaidiwa na wakulima wenzangu hapa kijijini.”

 Programu ya redio inarahisisha kupata msaada wa maofisa ugani, hasa namna ya kurutubisha udongo,” Mbaga aliongeza.

 Mfumo holela wa mvua ukichangiwa na vipindi virefu vya ukame vimeathiri sana maisha ya watu vijijini.

Wanasayansi wanasema njia rahisi za kuhimili kama vile kubadili tarehe za kupandia na kubadilisha mazao zinaweza kusaidia sana wakulima wadogo wadogo kuepuka hatari ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Ofisa wa Ruvu, Dawson Maine alisema programme za redio zimesaidia wakulima kuongeza mazao iliyokuwa imedidimia katika miaka ya hivi karibuni.

“Tunafuatilia takribani hekari 400 za vitunguu ambazo zimewekwa kwenya mfumo wa umwagiliaji, na tunatoa msaada wa mawazo kwa wakulima,” Maine alisema. “Wakulima wanakabiliana vyema kutokana na mambo mabalimbali yanayoathiri maisha yao.”

Kata ya Ruvu ina wakazi 12,820. Kabla ya kuathiriwa na ukame kata hii ilikuwa kitovu cha uzalishaji wa vitunguu an mpunga kaskazini mwa Tanzania, ikivutia wateja kutoka Moshi Arusha na Nairobi.

“Ni lazima wakulima wastahimili mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanaathiri mapato yao kutokana na kupungua kwa mazao yao,” alisema Henri Laswai, Mtafiti wa mambo ya kilimo chuo kikuu cha Sokoine. “Matokeo yake,  wanasukumwa kwenye lindi la umaskini.”

 Mchuuzi wa vitunguu wilayani Same amesema licha ya matatizo ya hali ya hewa, vitunguu vingali biashara yenye faida. Ekari moja huzalisha zaidi ya kilo 600 zenye thamani kati ya laki 6 na milioni 1.2 

 Farm Radio International, imetoa mchango mkubwa katika kuanzisha mpango huu.  Inasaidia zaidi ya redio 250 barani Africa kuwafikia wakulima. Nchini Tanzania, shirika hilo limeanzisha programu mbalimbali za redio zenye malengo ya kusaidia wakulima. 

Kizito Makoye ni mwandishi wa habari mwandamizi aliyepo Dar es Salaam, amebobea zaidi kwenye habari za mazingira, uongozi na mambo ya wanawake.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->