×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Tanzania yatunga sheria ya umwagiliaji kusaidia wakulima kupambana na mabadiliko ya tabia nchi

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Wednesday, 4 September 2013 19:09 GMT

Provisions to protect villagers from land grabs in the name of irrigation projects were tightened after legislators raised concerns

DAR ES SALAAM (Thomson Reuters Foundation)- Ili kulinda wakulima wa Tanzania kutokana na ongezeko la dhiki zinazi sababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, na ile ya tabia nchi, bunge limetunga sheria mpya itakayoendeleza kilimo cha umwagiliaji, wakiwa na matumaini kuwa itaongeza uzalishaji wa chakula na kupiga vita umaskini

Wachambuzi wa mambo wanasema Sheria ya Umwagiliaji ya mwaka 2013—iliyopitishwa mwishoni mwa mwezi August, kabla ya kuidhinishwa na rais — itaipa sekta ya kilimo nguvu mpya katika kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania. Kinachangia  zaidi ya robo ya pato la taifa, kinatoa asilimia 85 ya mauzo ya nje na kuajiri zaidi ya asilimia 80 ya wale wanao weza fanya kazi. Nchi ina ekari milioni 29.4 inayoweza kutumika katika umwagiliaji kati yake ni ekari 589,245 tu ndizo zinamwagiliwa.

Waziri wa Kilimo na chakula wa Tanzania, Christopher Chiza, ameliambia bunge kwamba sheria mpya italeta fikra mpya kwa nchi katika kutumia shamba kama rasilimali katika kilimo endelevu cha umwagiliaji

 “Tutatumia kila tone la maji lililopo nchini mwetu kuendeleza kilimo cha umwagiliaji - kufikia mwaka 2015 angalau asilimia 25 ya chakula lazima itoke katika kilimo cha umwagiliaji,” alisema.

Katika utangulizi, sheria hiyo inasema kilimo cha umwagiliaji ni nyeti kwa kuwa ukame na mafuriko yanaathiri sana kilimo kinachotegemea mvua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, yanayoathiri pia uchumi wa taifa na wakulima wadogo wadogo.

“Ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, tunahitaji mikakati inayoungana. Moja wapo ni kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji kinachotambua nafasi ya wakulima na changamoto wanazokabiliana nazo katika kuendeleza sekta,” Alisema Damian Gabagambi anayefundisha  kilimo chuo kikuu cha Sokoine mjini morogoro.

MFUKO WA UMWAGILIAJI

Licha ya jitihada za serikali kuboresha kilimo, uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara  umedhoofishwa  na ukosefu wa miundomsingi ya umwagiliaji pamoja na uongozi mbovu wa miradi iliyopo ya umwagiliaji

 Sheria ya taifa ya umwagiliaji inaimarisha sera ya umwagiliaji ya mwaka 2010 ambayo haina nguvu za kisheria  kuitekeleza. Hali hiyo itabadilika sasa.

Sheria mpya, mbali na mambo mengine, inaanzisha tume ya umwagiliaji—chombo cha kitaifa chenye dhamana ya kusimamia, kuendeleza na kudhibiti shughuli za umwagiliaji nchi nzima.

Sheria hii pia inaanzisha mfuko wa taifa wa umwagiliaji utakao saidia mipango ya umwagiliaji ambayo imekuwa taabani kifedha. Mfuko wa pesa—utakaotoka katika serikali na sehemu zingine zile—itatumika kulipia gharama za umwagiliaji zinazofanywa na mkulima mmoja mmoja na wawekezaji kupitia mikopo na dhamana.

Waziri amesema serikali kwa sasa inatekeleza miradi 39 ya umwagiliaji kwenye ekari 16,710 ikitumia teknolojia ya umwagiliaji ya dondoka kwa gharama ya Tsh 677.5 billion (Zaidi ya dola za kimarekani million $400). Hata hivyo, tume hiyo ikianza kufanya kazi, italazimika kuanzisha  zaidi ya mipango 1000, kulingana na upatikanaji wa fedha.

Sheria pia itaweka utaratibu kuwezesha vikundi vya wakulima, wawekezaji binafsi, na makampuni kumiliki miundomsingi ya umwagiliaji inayojengwa na serikali. Wawekezaji watakaojenga miundomsingi yao binafsi wanatarajiwa kulipa malipo maalumu ya huduma kwa tume.

MIGOGORO YA ARDHI

Baadhi ya mabadiliko yaliwekwa kwenye sheria baada ya mvutano mkali ulioibuka kati ya wabunge walioonyesha hofu kuu endapo mswada utapita hivyo hivyo unaweza ukazua wimbi la uporaji ardhi. Walidai kwamba huenda ukaipa serikali jeuri ya kuchukua mashamba ya wanavijiji bila ya kufuata taratibu muafaka.

Hata hivyo sheria bado inampa mamlaka waziri wa ardhi kuazimia eneo lolote kama ni sehemu ya umwagiliaji.  

“Ambapo itakapoonekana inafaa, waziri kwa kushirikiana na waziri mwenye dhamana ya ardhi na serikali za mitaa, anaweza kumshauri rais kuchukua ardhi bila ya kuathiri kipengele chochote cha sheria hii, kwa minaajili ya uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji,” sheria hiyo inasema    

Hata hivyo, kabla mswaada huo kuwa sheria wabunge wengi kutoka vyama tofauti vya kisiasa waliitaka serikali kubadilisha vipengele vyenye utata ambavyo vingechochea uporaji holela wa ardhi kwa wawekezaji kutoka kwa wanavijiji.                                                               

Christopher Ole Sendeka, mbunge wa Chama Cha Mapinduzi, alisema kifungu cha 17 na 18 huenda vikapenyeza mwanya kwa wawekezaji kupora ardhi kwa kufanya mazungumzo yasiyo rasmi na wanakijiji. Alisema jamii za wanavijiji ni lazima wawe na hisa na siyo watazamaji tu.

 Migogoro ya ardhi ya hivi karibuni baina ya wakulima na wafugaji zimesababishwa na upungufu wa mashamba, alisema, iwapo mswada huu utapita bila ya mabadiliko, wakulima wengi maskini watakuwa wahanga wa uporaji mashamba utakaochochewa na serikali ikishirikiana na wawekezaji

“Iwapo serikali inawaambia wawekezaji kuna ardhi ya kutosha kwa umwagiliaji, kwa nini inashindwa kumega sehemu ya ardhi hiyo na kuwapa watu kwenye maeneo  yanayotawaliwa na migogoro ya ardhi  baina ya  wakulima na wawekezaji?

Wabunge walisema ni lazima wakulima wawe na hisa kwenye miradi ya umwagiliaji iwapo ardhi yao inaangukia ndani ya eneo la umwagiliaji.

Pia walikataa kifungu kinachosema fidia italipwa kwa wakulima vijijini ambao ardhi yao itakuwa imechukuliwa kwa minaajiri ya uwekezaji.

“Msilete hapa swala la fidia, kwa kuwa mkifanya hivyo mtaruhusu ardhi kuuzwa, na kupelekea wakulima vijijini kukosa makazi na kuwafanya watumwa kwenye nchi yao wenyewe.

KINGA MADHUBUTI

Ikiwa ni matokeo ya hoja zilizotolewa na waheshimiwa wabunge, serikali imeongeza kipengele kitakachoruhusu wakulima wadogo kuwa wanahisa kwenye mikataba ya ardhi, pamoja na kuwa na nguvu za majadiliano na wawekezaji.

Wabunge pia walifanikiwa pia kupenyeza kipengele kingine kinachoeleza kwamba maamuzi yoyote juu ya maombi ya ardhi kwa ajili ya uwekezaji ni lazima yaamuliwe na mkutano mkuu wa kijiji.

 Kwa mujibu wa kitivo cha uwekezaji cha Tanzania, idara ya serikali, mchakato wa kupata ardhi unahitaji mwekezaji kuwasilisha maombi kwenye baraza la kijiji kupitia viongozi wa wilaya. Mkutano wa kijiji utaitwa kujadili ombi hilo na endapo kipande cha ardhi kitaidhinishwa kitumike kwa uwekezaji, umiliki wake huamishiwa serikalini, na serikali inabaki na mamlaka ya kulikodisha kwa miaka isiyozidi 99.

Waziri Chiza alijaribu kuondoa mashaka juu ya uvamizi wa ardhi. Haki za wananchi juu ya umiliki ardhi zitaendelea kulindwa na katiba na sheria zilizopo za ardhi na hakuna mtu hata mmoja ataruhusiwa kupora ardhi, alisema.

“Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu haitatokea popote kwenye sheria hii, mwekezaji wa kigeni kuwa mbadala wa mkulima wa kawaida,” alisema.

Kizito Makoye ni mwandishi mwandamizi aliyepo Dar es salaam, huanadika habari za mabadiliko ya tabia nchi utawala bora na haki za wanawake.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->