×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Ongezeko la watu lachochea shinikizo la mabadiliko ya hali ya hewa kwa wakaazi mjini Tanzania

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Thursday, 12 September 2013 11:45 GMT

With little support to adapt to worsening drought, farmers are moving to cities, and urban slums are swelling into flood-prone areas

DAR ES SALAAM, Tanzania (Thomson Reuters Foundation) —  Zacharia Masesa alihamia mjini  ilikubadilisha maisha yake. Miaka kumi iliyopita, aliwasili Dar es Salaam kutokea Mtwara, mji uliopo kusini mashariki mwa Tanzania, na punde alipata kazi kama muuzaji kwenye moja ya maduka eneo la Kariakoo. Kwa sasa Masesa mwenye umri wa miaka 37 anaishi na mkewe na watoto wawili kwenye nyumba aliyoijenga.

Hata hivyo siku hizi maisha ya Masesa yanabadilika kwa namna inayomtia hofu. Alivyonunua kiwanja kujenga kibanda maeneo ya Chanika wilayani Temeke, hakujua lilikuwa ni eneo linalokumbwa na mafuriko mara kwa mara.

Mwaka 2011, familia ya Masesa nusura isombwe na mafuriko yaliyozingira nyumba yake baada ya mvua kubwa. Tangu wahamie kwenye makazi yao mapya miaka mitatu iliyopita, wimbi la mafuriko limezidi kuwazingira, kutokana na ukosefu wa mifumo ya kutoa maji.

“Nililazimika kuwaokoa watoto wangu kwa kuwabeba mabegani ili wasizame,” anakumbuka. Vitu vyake vingi, hata ile radio kubwa aliyopewa na bosi wake kama zawadi ya harusi iliharibika.

“Sina amani kabisa,” anasema. “Kila mvua inyeshapo, najua ni lazima italeta mafuriko.”

WANAVYOKABILIANA NA MAFURIKO

Temeke ni miongoni mwa maeneo kadhaa jijini Dar es Salaam yanayoathiriwa sana na mafuriko yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa, ambayo wataalam wa mambo wanayahusisha na tabia nchi. Licha ya haya, wilaya hiyo imevutia wakaazi wengi sana wanaomiminika kila kukicha kutoka pande zote nchini kwa kuwa kuna fursa ya kupata na kumiliki ardhi na kujenga.

Wakazi wengi Temeke  wamejifunza mbinu za kukabiliana na mafuriko, baadhi yao wamejenga nyumba zao kwa mtindo wa kuhifadhi vitu vya thamani darini wakati wa mafuriko.

 

 

Wakati wa mafuriko, baadhi ya vijana hujipatia ajira, kwa kuhamisha wahanga wa mafuriko na vitu vyao kwa kutumia mikokoteni. Hutoza kati ya shilingi 1000, na 5000 kulingana na ukubwa wa kazi.

“Huwezi jua lini mafuriko yatakuja. Ni vyema kuweka akiba ya pesa kuwalipa hawa vijana kukusaidia,” alisema Shafi Hussein, mkazi wa hapo.

Masesa hutumia muda wake mwingi wakati wa kiangazi, kuanzia mwezi Juni hadi Novemba kuikinga nyumba yake na kwa kutumia mifuko ya mchanga ikiwa ni namna ya kuzuia mafuriko yasimzingire.

“Siweki mzaha hata kidogo kwenye swala hili, najua mwisho wa msimu mmoja wa mafuriko ni mwanzo wa msimu mwingine,” alisema.

WIMBI LA WAHAMIAJI KUTOKA VIJIJINI

Jiji la Dar es salaam, ni miongoni mwa majiji yanayokua kwa kasi barani Africa. Lina idadi ya watu million 3.5 na huenda ongezeko la watu likavuka million 10 kufikia mwaka wa 2040.

Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Said Meck Sadick anasema ongezeko la watu Dar linasababishwa na umasikini vijijini unaochangiwa na ukame wa muda mrefu.

“Watu wanatelekeza shughuli za kilimo kwa kuwa hawaoni mwelekeo kwa kuwa maisha yao hutegemea kilimo cha mvua,” alikubaliana na haya, Samuel Wangwe, mtafiti katika shirika lisilo la kiserikali, REPOA, linalojihusisha na tafiti za maendeleo.

Kadiri jiji linavyozidi kukua, wakazi wengi masikini wanalazimika kuishi katika maeneo oevu na hatari kwa mafuriko, pamoja na kukua kwa kimo cha bahari.

Na kwa kuwa serikali inashindwa kudhibiti uhamiaji wa watu mjini, miundomsingi ya jiji inakuwa taabani.

“Hatuna mfumo wa kuangalia idadi ya watu wanaokuja na kutoka Dar, hivyo basi, ni vigumu kuwa na mpango wa kuzuia kumiminika kwingi kwa watu,” amesema Sadick.

Hata hivyo Wangwe anafikiri serikali inaweza kuweka sera zitakazowasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kama vile kilimo endelevu, na mazao yanayodhibiti ukame pamoja na kuwa na bima za kilimo zitakazo walinda wakulima wakati wa msimu mbaya ya mimea.

TISHIO LA UMASIKINI

Chapisho la Benki ya dunia  linasema mabadiliko ya mwenendo wa mvua, kuongezeka kwa kimo cha bahari  na dhoruba, ni miongoni mwa matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoikumba dunia na kutishia mamilioni ya wakazi wa mijini kukumbwa na ukame.

Kwa  mujibu wa utafiti wa mwaka 2011 uliofanywa na serikali, unaoitwa economics of climate change in Tanzania, zaidi ya asilimia 8 ya eneo la Dar, pamoja na watu 140,000 na thamani za dola 170 million zimo katika maeneo hatari, kati ya watu hao, watu 31,000 wamo kwenye hatari kuu.

Utafiti huo unasema bila ya mbinu madhubuti ya kustahimili mabadiliko hayo idadi ya watu walio kwenye hatari mjiji Dar huenda ikaongozeka mpaka kufukia 100,000 na thamani za dola 400 milioni zikiwa hatarini.

Wadadisi wa mambo wanasema miji mingi Tanzania itakabiliwa na wimbi kubwa, na ongezeko la watu miaka kumi ijayo kutokana na uhamiaji holela, ukisababisha matatizo kadhaa ikiwemo makazi duni, uchafu, msongamano, uchafuzi wa hali ya hewa, upungufu wa chakula na upungufu wa maji.

 “Viongozi wa serikali wana wajibu wa kuweka mipango ya miji na kuangalia maendeleo ya makazi. Hata hivyo, kazi hii inaonekana kuwa ngumu kwao” alisema Lusuga Kironde, mtaalamu wa mambo ya uchumi na mipango ya miji, wa chuo kikuu cha ardhi Dar es Salaam.” Wakazi wengi wa mijini wanaishi katika mabanda zinazokuwa kwa kasi ukilinganisha na maeneo mengine.

Akiongea kwenye mdahalo uliofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam kuhusu Changamoto za ongezeko la watu mijini katika muktadha wa mabadiliko ya tabia nchi, Mkufunzi wa chuo kikuu cha Dar es Salaam Pius Yanda alisema tishio la mabadiliko ya hali ya hewa linaweza adhiri jamii ya watu wanaoishi pembezoni mwa bahari barani kote Africa, baadhi ya mambo ni mmomonyoko wa udongo, mpenyo wa maji chumvi, na uharibifu wa nyumba.

Aliwahimiza wale wanohusika na mipango ya miji waongeze mikakati itakayo weza punguza athari. Wataalam wanaamini sehemu zilizo katika athari ni miundomsingi, usambazaji wa maji, maji taka na usimamizi wa taka na umeme.

Kizito Makoye ni mwandishi mwandamiz aliyepo Dar es Salaam

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->