×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Mbegu ya wimbi mseto inayostahimili ukame kupambana na njaa, hata ugonjwa wa kisukari

by Isaiah Esipisu | @Andebes | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 17 September 2013 11:45 GMT

Hybrid finger millet grows in a test field in Kenya. THOMSON REUTERS FOUNDATION/Isaiah Esipisu

Image Caption and Rights Information

New Kenyan millet could help with crop losses to extreme weather, and prove a popular food for people with diabetes thanks to its low sugar content

KAKAMEGA, Kenya (Thomson Reuters Foundation) – Mmea unaopendwa zaidi nchini Kenya, ijapokuwa haujulikani kutokana na mazao yake haba, sasa umeboreshwa kwa kubuni mbegu mpya ya mseto.

Wanasayanzi nchini Kenya wasema kuwa nchi hiyo ni ya kwanza barani Afrika kubuni mbegu ya mseto ya wimbi, ambayo inatarajiwa kuwa zao mbadala ya mahindi inayozidi kuathiriwa na ukame. Mmea huo pia utasaidia kupambana na ugonjwa wa kisukari.

Wimbi ni mojawapo ya mimea muhimu zaidi nchini Kenya kwa kustahimili ukame, lakini wakulima hukuza kiwango kidogo zaidi kutokana na mazao yake haba. Takwimu za serikali zaonyesha kuwa mmea huo hupandwa kwa shamba lenye ukubwa wa ekari 65,000 kila mwaka, licha ya ukosefu wake unaopelekea bei yake kuwa juu.

Tofauti na nafaka zingine kama vile mpunga na mahindi zilizofanywa mseto, wakulima wanaokuza wimbi hutegemea mbegu isiyomseto iliyo na mazao haba. Hili huwavunja roho ya kuongeza kilimo hicho, asema Chrispus Oduori, mwanasayanzi kutoka Taasisi ya utafiti wa kilimo nchini Kenya ijulikanayo kama – KARI.

Lakini kwa sasa, wimbi umefanywa mseto, na mbegu hiyo mpya inazaa mara mbili zaidi ikilinganishwa na ile ya kawaida. Majaribio ya mapema imebainisha kuwa mbegu hiyo ya mseto yaweza kutoa kati ya magunia 18 na 24 ya wimbi kwa kila ekari moja, ikilinganishwa na magunia 12 kutokana na mbegu ya kawaida.

Kulingana na Joyce Maling’a, mkurugenzi mkuu wa KARI Kakamega, taasisi hiyo kwa sasa inashugulikia mimea zilizosahaulika haswa kutokana na mazao duni. Mimea kama hizo zimebainika kuwa na uwezo wa kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa.

KARI imeanzisha duka la kuuza mbegu zilizosahaulika, ambapo wakulima hununua mbegu kama vile wimbi, mtama, maharagwe na kadhalika. Hii ni kwa sababu kampuni za mbegu hutegemea kuuza mbegu ambazo hulazimisha mkulima kuzinunua kila msimu.

Maling’a anaamini kuwa kuboresha mazao ya mimea kama hizo ni hatua itakayosaidia kupambana na upungufu wa chakula nchini, hali ambayo inahatarishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Njia moja ya kutatua tatizo hilo ni kubuni miseto kwa kuchavuliwa kwa mbegu ya uzazi kutoka mmea aina moja hadi aina nyingine ili kupata ubora uliopo katika mbegu vizazi.

Kabla ya miaka ya 1960, mahindi kwa mfano, haikuwa na mazao bora zaidi kama ilivyo hivi leo, asema Oduori. Lakini hivi leo, nafaka hiyo imekuwa ya kutegemewa katika nchi ya Kenya na Afrika kwa jumla kutokana na teknolojia ya mseto, asema bwana huyo, ambaye ndiye mwanasayansi anayeongoza mradi wa wimbi wa mseto, kwa ufadhili kutoka Alliance for Green Revolution in Africa (AGRA).

Oduori aliambia Thomson Reuters Foundation kuwa mazao bora ya wimbi yatahimiza wakulima wengi kupanda mbegu hiyo. Asema kuwa haya ni mafanikio makubwa yatakayoamsha jitu hilo lililolala.

KARI imeendeleza utafiti huo kutoka mwaka wa 2004, na wanasayanzi katika taasisi hiyo wasema kuwa wanamalizia majaribio ya mbegu hiyo kitaifa, ambayo ni hatua ya mwisho kabisa inayotekelezwa na shirika la kuchunguza afya ya mimea nchini Kenya – yani KEPHIS.

Oduori asema kuwa kuna mamilioni ya watu katika Afrika ya Mashariki ambao hutegemea wimbi kama chakula, na wengine wengi wanaotumia nafaka hiyo kwa sababu za kiafya. Wataalam wa afya wasema kuwa wimbi una kiwango cha sukari cha chini zaidi, jambo ambalo hupelekea nafaka hiyo kuwa kiungo muhimu katika lishe ya kudhibiti kisukari.

Nancy Ngugi, ambaye ni Mwenyekiti wa Diabetes Management Information Centre asema kuwa watu wanaougua kisukari wanahimizwa kula chapatti iliyotengenezwa kutokana na unga wa wimbi, mkate wa wimbi, na hata kunywa uji wa wimbi kama njia ya kudhibiti maradhi hayo.

Utafiti wa awali, uliochapishwa katika jarida la ScienceDirect ulibainisha kuwa lishe ya wimbi hudhibiti kiwango cha sukari mwilini, na pia husaidia vidonda kupona kwa haraka.

Kisukari ni mojawapo ugonjwa muhimu usiyoambukizana nchini Kenya, na barani kwa jumla. Ngugi asema kuwa asilimia 4.2 ya Wakenya wanaugua ugonjwa wa kisukari, ambapo wengi wanaishi mijini. Asema kuwa, ugonjwa huo usiyopona unaweza kudhibitiwa kwa kutumia vyakula vinavyofaa.

Alisema kuwa zaidi ya asili mia 50 ya wagonjwa wanaoenda hospitalini nchini Kenya wanaugua magonjwa yasiyoambukizana, huku asili mia 25 wakiwa na kisukari.

Hata hivyo, sababu muhimu iliyopelekea KARI kuanzisha utafiti wa mbegu ya mseto ya wimbi ilikuwa kupatia wakulima mbegu mbadala ya nafaka, kwa sababu ya upungufu kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Ni wazi kuwa Kenya yategemea mahindi zaidi ya nafaka zingine, asema Oduori. Ilhali, kutokana na mabadiliko ya tabianchi mahindi hukosa kuzaa vyema kutokana na ukame ama mvua liliyozidi, magonjwa, wadudu, na hata kwa kukosa kupanda wakati unaofaa.

KARI kwa sasa inalenga utafiti wa wimbi, mtama, mihogo, na mimea zingine ambazo zina uwezo wa kustahimili hali ya ukame.

Unga wa wimbi unaosagwa na kampuni kubwa kubwa nchini Kenya sasa unauzwa katika maduka yaliyobobea nchini kwa bei ya juu.

Isaiah Esipisu ni mwandishi wa mambo ya sayanzi, na ni mkaazi wa Nairobi. Anaweza kufikiwa kupitia esipisus@yahoo.com

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->