Kenya yakabiliwa na tatizo la usimamizi wa miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa

by Justus Bahati Wanzala | Thomson Reuters Foundation
Monday, 30 September 2013 11:08 GMT
Kenya lacks rules for making sure climate funds are used properly and that communities get their fair share, governance experts say

NAIROBI (Thomson Reuters Foundation) – Kabila la wachache la Ogiek nchini Kenya  ambalo  linaishi katika Msitu wa Mau katika eneo la Bonde la Ufa  na hutegemea uwindaji na ukusanyaji wa matunda, linalalamika kuwa limetengwa katika harakati za kuufufua msitu huo ambao ulikuwa umeharibiwa huku harakati hizo zikihusisha upanzi wa miti ya kigeni  badala ya miti asili ambayo wanategemea. 

 “Tumeteseka muno,” asema Joseph Lesingo, ambaye ni mwanachama wa baraza la wazee la jamii hiyo. “Wakati msitu wa Mau ulipoharibiwa kupitia ukataji kiholela wa miti, tulipoteza makazi na pia kupokonywa rasili-mali za msitu kama vile asali, matunda ya porini na tiba asili,” aliliambia shirika la habari la Thomson Reuters Foundation.

Msitu wa Mau ambao unapatikana eneo la Magharibi mwa Kenya ndio msitu mkubwa zaidi asili ya maeneo ya milima katika kanda ya Afrika Mashariki. Ni chanzo muhimu cha mito na umeshuhudia uharibifu mkubwa tangu miaka ya 1980 kutokana na ardhi ya msitu huo kutengewa shughuli za kilimo na makazi ya binadamu. Kulingana na Mpango wa Mazingira wa Umoja wa Mataifa (UNEP), takriban ekari laki moja za msitu huo zimenyakuliwa tangu mwaka 2000. 

Lesingo anasema jamii ya Ogiek imekuwa tayari siku zote kushirikiana na makundi ya kuhifadhi mazingira, asasi za serikali na kampuni ambazo zimezindua jitihada za kuufufua msitu huo, lakini azma hiyo  haijakuwa rahisi kuafikia. “Tumeishi hapa kwa karne nyingi na tuna maarifa ya kiasili kuhusu matumizi yanayofaa ya msitu huu, lakini kando na kuathirika na uharibifu wake, tumetengwa katika shughuli za kuufufua  na  haki zetu zinaendelea kukiukwa,” anasema.

Mzee huyo anasema lengo hasa la  kutiliwa mkazo harakati za kuufufua msitu huo ni hofu kuwa mto Mara ambao unategemewa  na wanyama na uoto kwenye mbuga ya Kitaifa  ya Mara – yenye kuvutia watalii wengi  kutokana na kuwepo kwa wanyama wengi na uoto wa aina tofauti ulikuwa katika tisho la kukauka.

LENGO LA KUJIFAIDI

Mnamo mwaka 2008, jopo kazi la viongozi wa ngazi ya juu serikalini, watafiti na wataalam kutoka mashirika yasiokuwa ya serikali  lilibuniwa kutafuta mbinu za kuokoa msitu huo huku athari za  mabadiliko ya hali ya hewa zikianza kudhirika kama vile kukauka kwa baadhi  ya  mito 12 ambayo chanzo chake ni msitu huo nayo mvua ikipungua na kutatiza kilimo katika maeneo yaliyoko karibu na msitu huo. Mnamo mwaka 2009, jopo kazi hilo bila kushauriana na jamii zinazoishi katika eneo hilo la Mau lilipendekeza kufufuliwa kwa msitu huo kupitia upanzi wa miti na kufurushwa kwa watu wanaoishi katika ardhi iliotengewa msitu huo. 

Takriban Dola za Marekani milioni 2.5 (kiasi cha shilingi billion mbili za Kenya) zilitengewa utekelezaji wa mapendekezo ya jopo kazi hilo. Baada ya kugundua kwamba mpango wa ufufuaji wa msitu wa Mau ulitoa fursa nzuri ya kupata ufadhili chini ya mpango unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wa kupunguza gesi ya kaboni kupitia upanzi wa miti na uhifadhi wa misitu (REDD), washikadau wengi walijiunga na mpango huo.

Lakini kulingana na Lesingo, ni hatua chache tu ambazo zimepigwa. Baada ya kunusa pesa, wanasiasa walijiingiza kwenye mpango huo wa kufufua msitu wa Mau, huku wakitumia fursa hiyo kujinufaisha kibnafsi, aliongeza. Kwa mfano aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliunga mkono kauli ya serikali ya kuwaondoa watu waliokuwa wakiishi katika msitu huo, lakini wanasiasa wa eneo hilo walipogundua kwamba hatua hiyo ingeathiri idadi ya watu katika maeneo hayo na kupunguza wale ambao wangewapigia kura, waliipinga vikali uamuzi huo.  

Zaidi ya kunadi mipango inayozua matumani makubwa, nia ya makundi yanayomiminika kuendesha miradi katika Msitu wa Mau haieleweki, Lesingo alisisitiza. Makundi mengi huajiri watu kutoka jamii ya Waogiek kupitia mashirika ya kijamii (CBOs) kupanda miti ya kigeni kwa lengo la kushiriki biashara ya kuuza gesi ya kaboni, alisema. "Jamii haishirikishwi kuhusu namna na faida ya miradi ya biashara ya kaboni ila inapashwa tu habari kwamba upandaji miti utazalisha fedha," alisema.

Gatundu Mwendwa, ambaye ni mwanachama wa shirika la kijamii la Kitunga, ambalo linashiriki shughuli ya kupanda miti ili kuufufua msitu wa Mau pia alieleza umuhimu wake. "Iwapo unaona  mafanikio yoyote katika ufufuaji wa Msitu wa Mau, kuwa na uhakika kwa hali ingeweza kuwa  bora zaidi," alisema.

UKOSEFU WA SHERIA

Hali inayokumba miradi ya uhifadhi wa msitu wa Mau ni mithili ya matatizo yanayokumba miradi mingine ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali hewa nchini Kenya. Sababu kuu ya matatizo hayo ni udhaifu katika usimaizi wa shughuli hizo, wanasema wataalam.

Benson Ochieng, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Sheria na Usimamizi wa Maswala ya Mazingira (ILEG), yenye makao yake jijini Nairobi anasema kuwa miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa  inakabiliwa na ukosefu wa uwazi na kutotolewa  taarifa kwa umma kuhusu michakato ya kufanya maamuzi, na pia migogoro ya kimaslahi.

Kulingana na Ochieng, jamii zinatapeliwa na makampuni yanayoshiriki katika biashara ya kaboni. Lengo halisi hasa kwenye baadhi ya mikataba ya ukodishaji ardhi kwa muda mrefu sio upanzi wa miti,” aliliambia shirika la habari la Thomson Reuters Foundation.

Alitaja mfano wa eneo la Dakicha, wilayani Malindi katika eneo la Pwani ambapo jamii ya eneo hilo ilihadaiwa na kampuni moja ya kigeni ambayo ilisingizia kuwekeza katika mradi wa kukuza mmea wa kuzalisha mafuta ya kutumika kama kawi kwa minajili ya biashara ya gesi ya kaboni, lakini ikatumia  mradi huo kwa shughuli za kitalii kwa njia ya faragha huku maslahi ya jamii hiyo yakipuuzwa. 

Raia wengi hawaelewi kiasi na jinsi ya kunufaika na ufadhili uliopo wa miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa na jinsi makundi ya kijamii yanaweza kunufaika nao, aliongeza.  

Ochieng anasema ufisadi pia unahujumu usimamizi wa miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa nchini Kenya, ikiwemo ufujaji  na wizi wa fedha. Hata hivyo, Kenya haina sheria za kukabiliana na makosa yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa hali inayochangia washukiwa kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.  

Mfumo wa kisheria unahitajika kwa ajili ya mipango kama REDD ili uweke  wazi maslahi mbalimbali na majukumu ya washiriki tofauti na kufichua muundo wa uwekezaji, Ochieng alisema. "Huku nchi  ikijitoza  zaidi katika masuala ya hali ya hewa, sheria lazima ziandaliwe ili  kukabiliana na makosa yanayohusiana na mabadiliko  ya  hali ya hewa," alisema

KUSALIA NYUMA

Mkurugenzi huyo wa taasisi ya  ILEG aliongeza kuwa Kenya imesalia  nyuma katika   matumizi ya  masoko ya gesi ya Kaboni kama chanzo cha mapato kutokana na viwango vya chini vya teknolojia, urasimu na ukosefu wa miradi kubwa kwani iliyopo  ni  ndogo muno. Kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi ya Taifa ya Mazingira (NEMA), Kenya  ilikuwa na miradi 16 ya kupunguza uzalishaji wa gesi ya Kaboni iliyoidhinishwa chini ya Utaratibu wa Umoja wa Mataifa wa  Matumizi ya Kawi Safi  (CDM) mnamo mwezi Juni 2013, ikilinganishwa na 22  nchini Misri na 24 katika Afrika Kusini.

Tawi la Kenya la Shirika la kukabiliana na ufisadi duniani la Transparency International (TI-Kenya) pia linasema kuwa jamii hazipokei fidia inayofaa. Linasema kuwa uhamasishaji wa kina unahitajika ili kuwawezesha watu mashinani kuelewa mikataba wanayoafikia na makundi yanayohusika katika ununuzi wa gesi ya kaboni.

Huku kiasi kikubwa cha fedha kikielekezwa katika mipango ya mabadiliko ya hali hewa, ufuatiliaji bora, uwazi na uwajibikaji ni muhimu, anasema Jacob Otachi, afisa wa miradi katika tawi la Kenya la shirika la Transparency International. Ufadhili wa miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa hauleweki kwa urahisi kwani unahusisha maswala na sekta mbalimbali, alisema. “Kwa mfano ukabilianaji na maradhi ya Malaria ni swala la afya na  kwa upande mwingine  pia ni  swala la mabadiliko ya hali  ya hewa,” aliwambia wanahabari kwenye kongamanao katika mji wa Nakuru ulioko nchini Kenya mwezi Oktoba mwaka uliopita.  

Wataalam wanakubaliana kuwa sera mwafaka na uadilifu ni muhimu katika kuhakikisha mfumo bora wa utaratibu wa kufadhili miradi ya mabadiliko ya hali ya hewa. 

“Kenya – jinsi yalivyo mataifa mengine ya bara Afrika imo katika hatari ya kuathirika na  mabadiliko ya hali ya hewa na jitihada zinahitajika  kuhakikisha uwazi, haki na kujitolea kwa washikadau  kutumia teknolojia   inayofaa ili kutumia fursa zilizopo ndipo taifa linufaike na miradi hiyo,” asema Ochieng wa shirika la ILEG.

Justus Bahati Wanzala ni Mwanahabari anayeishi jijini Nairobi.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.