×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Familia zilizofurushwa msituni Kenya zaweka kambi barabarani, maafisa wakanusha kuchoma nyumba

by Caleb Kemboi | Thomson Reuters Foundation
Friday, 31 January 2014 13:42 GMT

The Kenyan government has proceeded with evictions of indigenous people from the Embobut forest - hundreds are now camping on roadsides without basic necessities

ELGEIYO MARAKWET, Kenya (Thomson Reuters Foundation) - Mamia ya watu wa jamii ya Sengwer – wengi wao watoto, akinamama na wazee – wamepiga hema kwenye baridi, Magharibi mwa Kenya, nje ya msitu wa Embobut baada ya kufurushwa na walinzi wa misitu pamoja na maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami, na ambao walichoma zaidi ya nyumba elfu moja yapata majuma mawili yaliyopita.

Serikali ya Kenya inasema watu wanaoishi katika misitu ni sharti waondoke ili kutoa fursa ya harakati za kurejesha mazingira kuendelea, na inadumisha kuwa imewalipa fidia watu hao ili kuwasaidia kupata makao kwingineko.

Lakini familia mbazo zimepoteza mali zao, kwa sasa wanaishi bila bidhaa muhimu kwenye barabara karibu na msitu walimofurushwa. Mmoja wa waliofurushwa, Magret Chebor alisema hawana chakula wala maji ya kutosha. “Kwa sasa tunaishi kwa hofu ya kuambukizwa magonjwa ya kuambukizana – tunaendelea kusongamana zaidi katika eneo hili,” aliambia Thomson Reuters Foundation.

 “Hatuna mahali pa kuita nyumbani mbali na msitu – tumefurushwa na serikali yetu wenyewe, na sasa tunaishi katika mazingira ya kutamausha,” alisema.

Lakini hata nyumba zao za mda sio salama. Thomas Kiprono, mmoja wa waliofukuzwa msituni alisema maafisa wa kiusalama wamekuwa wakibomoa nyumba zao za mda. “Hatujui tufanye nini – wametishia pia kutukamata sisi iwapo tutajenga nyumba nyingine,” alisema huku akidondokwa na machozi.

Johnstone Kimtai alieleza jinsi maafisa waliojihami waliwasili asubuhi moja na kuchoma nyumba kadhaa kwa haraka kandokando mwa msitu hu. “Walipokaribia moja ya boma, mwanamke alipiga mayowe akisema, “acheni! Mwanamke mmoja alikuwa katika uchungu wa kujifungua kwenye moja ya nyumba hizo,” alisema.

Mkunga wa kitamaduni alikuwa ameamua kumsaidia mwanamke huyo kujifungua kwa sababu kituo cha afya kilikuwa mbali. Maafisa waliojihami waliendelea kuchoma nyumba karibu na eneo hilo, lakini waliacha nyumba ya mama huyo aliyekuwa anajifungua na kutokomea ndani ya msitu, aliyeshuhudia alisema.

Mmoja wa maafisa wa kiusalama aliyekuwa akishiriki shughuli ya kuwafurusha watu kwenye msitu, na ambaye alikataa kutajwa jina, alisema yeye na mwenzake walikuwa wamepewa amri ya kuchoma nyumba na kuwafurusha wale waliokataa kuondoka kwenye msitu.

 “Tulikuwa tukiamka saa tisa alfajiri kila siku ili kutekeleza jukumu hilo – huku kwenye mlima ni baridi sana, nawahurumia watu hawa waliofurushwa lakini inatulazimu kutekeleza jukumu letu,” alisema.

WITO WA MSAADA

Nyingi ya familia zilizofurushwa, wengi wao kutoka Jamii ya Sengwer, zinasisitiza kwamba hawakujumuishwa kwenye mpango wa serikali kuwafidia watu waliokuwa wakiishi kwenye msitu huo, na wameapa kuendelea kukita hema karibu na msitu hadi watakapopewa ardhi nyingine.

“Tuko tayari kwa lolole ili mradi ni kwa sababu ya ardhi yetu ya asili,” alisema mmoja wa waliofukuzwa kwenye msitu huo na aliyeomba jina lake kutotajwa. “Bado hatujashuhudia umwagikaji damu, lakini iwapo swala la Embobut halitashughulikiwa kwa njia inayohitajika, ni hatari sana. Utaniambia vipi niondoke msituni bila kunieleza nitakapoelekea kuanza maisha mapya.

Paul Kaptuga, baba wa watoto wawili, alisema maafisa wa kiusalama waliiba mali ya watu wakati wa shughuli ya kuwafurusha kutoka msituni. “Kondoo zangu kadhaa zilitoweka kwa njia isiyoeleweka – ashuku maafisa wa polisi waliokuwa wamejihami waliiba ili wale,” aliongeza.

Boma la familia yake na mali, ikiwemo vitabu vya watoto wake na sare za shule, zilichomwa. “Sasa hawana mavazi – bado hatujalipwa fidia,” alisema kwa hisia. “Hili ni janga mara mbili kwangu. Sijui nini kitakachofuata kwangu na familia yangu.”

Nyanyake Kaptuga mwenye umri wa miaka 81 kwa sasa anakikohozi kutokana na madhara ya kulala nje kwa baridi kali. “Tunahofia huenda akaambukizwa ugonjwa wa Pnemonia, hatuna chochote cha kumfunika wakati wa usiku,” alisema.

Stephen Cheboi, mratibu wa shirika la North Rift Human Rights Network, lenye makao yake katika mji jirani wa Eldoret, alitoa wito kwa mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu na megine kusaidia kutoa huduma za dharura kwa familia hizo.

 “Familia zilizofurushwa zinatumia ngozi na matawi kujisitiri kutokana na baridi. Hali huenda ikawa mbaya hata zaidi iwapo mvua itaanza kunyesha,” aliongeza.

VIONGOZI WA ENEO HILO WALALAMA

Wakati uo huo, viongozi wa eneo hilo wameishtmu serikali kwa kuruhusu nyumba kuchomwa. “Hii ni mbinu iliyopitwa na wakati ya kuwafukuza watu,” alisema Seneta wa Jimbo la Elgeiyo/marakwet Kipchumba Murokomen.

Baadhi ya wanasiasa wameitaka serikali kukoma kutumia nguvu wakati wa kuwaondoa watu kutoka kwenye msitu.

Lakini Inspekta Stephen Chessa,ambaye anaongoza shughuli ya kuwafukuza watu kutoka kwenye msitu, ametetea maafisa wake. “Hakuna nyumba ya familia yoyote tuliochoma – wao (Jamii ya Sengwer), walichoma nyumba zao wenyewe kabla ya kuondoka kwenye msitu,” alisema, akiongeza kwamba kwa wakati mwingine majirani walichomeana nyumba zao wenyewe.

Seneta Murkomen alisema viongozi wa eneo hilo wameitaka serikali kuwalipa familia ambazo hazikujumuishwa kwenye mpango wa awali. “Serikali inapaswa kuzisaidia familia hizi kupata makao katika maeneo mapya na kuhakikisha watoto walioathirika wanarejelea masomo,” alisema.

Kamishna wa Jimbo la Elgeiyo/Marakwet Arthur Osiya alisema watu lazima waondoke kwa sababu msitu huo umeharibiwa sana.

 “Familia zote zililipwa fidia na hazina budi ila kuondoka kutoka kwenye msitu huo ili kuruhusu mchakato wa kuurejesha na kuuhifhadhi kuanza.,” alisema katika mahojiano ya simu.

“Baadhi ya watu waliofukuzwa wanaondoka kwenye msitu mchana na wanarejea kule usiku, hali inayoipa kazi ngumu maafisa,” alidai Osiya.

Mnano Alhamisi, jamii zilipewa makataa ya siku saba kuwaondoa mifugo wao kutoka kwenye msitu la sivyo mifugo hao watanadiwa, Kamishna wa Jimbo alisema wakati alipozuru msitu huo.

KUKAIDI AGIZO LA MAHAKAMA

Msemaji wa Jamii ya Sengwer, Yator Kiptum alisema serikali ilichoma nyumba za watu wa Jamii hiyo licha ya kuwepo kwa agizo la mda la kusimamisha shughuli ya kuwafurusha kutoka msitu huo – agizo lililotolewa na mahakama ya mjini Eldoret. “Serikali ilitumia nguvu kutufurusha kutoka kwenye ardhi yetu ya asili hivyo kukiuka katiba ya Kenya na sheria za kimataifa,” alisema.

 “Tunapanga kuwasilisha mahakamani kesi ya kukiuka agizo la mahakama dhidi ya serikali na wote wanaohusika na shughuli inayoendelea na kuchoma nyumba na kutuhangaisha,” aliongeza.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->