×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Serikali ya Tanzania kufungua ardhi zaidi kwa wafugaji

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Friday, 7 March 2014 10:15 GMT

Tanzania's government hopes new grazing land will improve access to water and pasture, reducing conflict between struggling pastoralists and farmers

DAR ES SALAAM, Tanzania (Thomson Reuters Foundation)- Serikali ya Tanzania imepanga kugawa ardhi ya malisho na maji kwa wafugaji ikiwa ni sehemu ya sera yake ya kuepuka migogoro ya mara kwa mara  na wakulima.

Mpango huo madhubuti utakaotekelezwa hivi karibuni utatoa fursa kwa wafugaji kupata maeneo ya malisho ili kukabiliana na ukame ulio athiri kwa kiasi kikubwa maeneo yao ya asili.  

Sanig’o Ole Tellele, naibu waziri wa mifugo na uvuvi ameiambia Thomson Reuters Foundation kwamba lengo ni kutafuta suluhu ya kudumu ya mizozo ya mara kwa mara inayohatarisha amani.

“Serikali imedhamiria kutatua mizozo hiyo,” alisema. “Tukiwapatia maji na malisho, hakutakuwa na matatizo tena na wakulima,” alisema.

Waziri alisema ufugaji ni mtindo wa maisha unaostahili kuendelezwa. “Tungependa wafugaji wawe na maisha bora yanayoendana na uchumi wa kisasa na rafiki kwa mazingira,” alisema.

Chini ya mpango huo ambao unatarajia kugharimu walipakodi shilingi billion 15 (US$9.3 million) kwa mwaka—zaidi ya hekari milion 10 za ardhi yenye maji itapimwa na kupewa wafugaji kama wataitaka. Hii ni ziada ya Kilomita za mraba 611,238 za ardhi ya malisho iilizopo, ambazo asilimia 72 tu ndiyo imetumika.

Mizozo imezuka hivi karibuni nchini Tanzania baada ya ukame kuathiri wafugaji. Wakigombea vyanzo vya maji vinavyokauka, wakulima wamewashutumu kwa kuharibu mazao yao baada ya kuruhusu ng’ombe kukanyaga mashamba.

Katika tukio moja la hivi karibuni, zaidi ya watu kumi waliuwawa mwezi January wilaya ya Kiteto, mkoa wa Manyara baada ya kuvamiwa na wafugaji wa kimaasai waliokuwa wakigombea hifadhi ya Embroi Murtangosi na kuchoma nyumba kadhaa.

Wafugaji wameiambia Thomson Reuters Foundation kuwa wana mtizamo mchanganyiko kuhusu sera ya serikali. Baadhi yao wanatumai itasaidia kuondoa mvutano na wakulima, wakati wengine wanahofia huenda ni jaribio lingine kuwaondoa kwenye ardhi asilia ya malisho ili kupisha shughuli za uwindaji.

Sehemu kubwa ya ardhi inayotumiwa na wafugaji kaskazini mwa nchi, inapakana na mbuga za wanyama, ambapo serikali imekodisha kwa wawekezaji wa nje.

“Nafikiri ni hatua nzuri kama kweli inatekelezwa, tatizo letu kubwa ni ukosefu wa maji- tunahitaji maeneo yenye maji. Sehemu zetu za malisho zimechoka kabisa,” alisema Saimon Ole Sinei, mchungaji wa kimaasai wilayani kilosa mkoa wa Morogoro.

Mwandu Kisesa, mfugaji wilaya ya Meatu alisema iwapo wafugaji watapewa maeneo, huenda tatizo la uharibifu wa ardhi na migogoro katika jamii zitafikia kikomo.

“Iwapo wafugaji watapewa shamba ya malisho kwa ng’ombe wao, migogoro ya ardhi itakwisha kabisa,” alisema. “Itapunguza pia mmomonyoko wa udongo kwenye ardhi ya malisho.”

Hata hivyo, Meshack Nangoro, mwakilishi wa Jamii ya kimaasai, wilayani Longido mkoani Arusha, hakuwa na matumaini.

“Sidhani kama haki itatendeka kwa wafugaji wa Kimaasai, zaidi ya kutufanya wakimbizi kwenye ardhi yetu wenyewe,” alisema. “ Kwa jinsi nijuavyo, kama tumeshawishiwa kuondoka kwenye ardhi yetu, kamwe hatutaipata.”

Nangoro ameiomba serikali kutoa vyeti vya miliki ardhi kuhakikisha kwamba wafugaji hawapotezi haki yao ya ardhi,” alisema.

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya kijiji ya mwaka 1999, jamii ina haki ya kuchagua juu ya matumizi ya ardhi kwenye maeneo yao, hata hivyo, ardhi yote inabaki kuwa ni miliki ya serikali. Hati za kimila ni za vijiji husika, hivyo mtu anapohama, huenda akapoteza haki yake kwenye eneo husika.

Baadhi ya wafugaji wanahofia huenda wakapelekwa kwenye maeneo yenye wadudu hatasi wa Mbung’o wanaoeneza ugonjwa wa nagana.

Japhet Ngilorit, mfugaji wilayani Kiteto mkoa wa Manyara amesema wafugaji waliozoea hali fulani ya kiikolojia huenda wasihimili changamoto za kuanza maisha mapya. “Nimeishi maisha yangu yote hapa- ukiniambia niondoke leo niende Morogoro sitajisikia vizuri, kwa sababu sijui kama ardhi mpya itanifaa.”

Kwa mujibu wa sensa iliyofanywa na shirika la ubora na viwango mwaka 2011, Tanzania ina jumla ya ng’ombe 22.8 millioni, wa tatu kwa wingi baada ya Ethiopia na Sudan.

Serikali inakadiria kuwa zaidi ya asilimia 70 ya mifugo inachungwa kwenye maeneo kame kaskazini mwa nchi, kati na magharibi yanayokabiliwa na ukame wa mara kwa mara kiasi cha kulazimu wafugaji kuhama kutafuta malisho.

Wanaharakati wa haki za kibinadamu na wadadisi wa mambo wamepokea mpango wa serikali kwa tahadhari. Baadhi yao wanahofu kwamba huenda isiwe mwisho wa migogoro kwa kuwa sheria na sera zilizopo ni ngumu kutekeleza.

Utatuzi wa migogoro ya ardhi unahitaji fikra pana, ikiwa ni pamoja na kuanzisha mpango utakaowezesha wafugaji kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, Ole Ngurumwa alisema

“Kuwahamisha wafugaji haita suluhisha tatizo - tunahitaji kukabiliana na uharibifu wa mazingira unaoathiri ufugaji,” alisema. Wafugaji pia ni lazima wafunzwe njia mbadala za kutafuta maisha,” aliongeza.

Sheria ya Malisho ya wanyama, kwa mfano inaelekeza ng’ombe wafugwe kulingana na uwezo wa eneo husika lakini si vile mambo yafanywavyo sasa. “Tumekuwa tukisikia hadithi ile ile kwa miaka lakini hatuoni chochote kikifanyika,” alisema. “Huu mpango mpya huenda ukafanikiwa iwapo sheria zitabadilishwa.

Onesmo Ole Ngurumwa, mtafiti na mtetezi wa haki za binadamu, amesema ugawaji wa ardhi si suluhisho la migororo ya ardhi.

Baadhi ya watu wanadhani mfumo mpya utaleta utata, kwa kuwa sheria ya malisho ya wanyama inazuia mzunguko holela wa ng’ombe, wakati huo huo serikali inasema wafugaji wanaweza kutafuta malisho sehemu nyingine.

Yefred Mnyenzi, mtaalam wa mambo ya ardhi anayeongoza taasisi ya Haki Ardhi, amesema mfumo wa ugawaji ardhi uliopo unawadhulumu wafugaji ambao hudhulumiwa haki zao na makundi mengine.

“Wafugaji hawakufikiriwa sana hapo nyuma kwakuwa hawakuwa na ardhi waliyotengewa kuendeleza shughuli zao.” Alisema Mnyenzi.

Makundi tofauti pia ni lazima yaelewe na kuheshimu mahitaji ya kila mmoja, aliongeza. “Ni lazima wakulima waheshimu ardhi iliyotengwa kwa ajili ya wafugaji na wafugaji nao wafanye vivyo hivyo.”

Kulingana na Mnyenzi, ukosefu wa elimu na uhusishaji hafifu wa uma katika utengenezaji wa sera ndio sababu kuu ya mivutano.

“Hata ambapo wananchi wanashirikishwa, maoni yao na matakwa yao, mara nyingi hayasikilizwi. Hivyo basi kuchangia katika kuongezeka kwa migogoro,” alisema.

Serikali na vyama vya kijamii ni lazima wafanye kazi kwa pamoja katika kuelimisha watu kuhusu sheria na sera zinazotawala mambo ya ardhi, aliongeza.

Rais wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Kikwete akiwaonyesha wafugaji wa kimaasai aina ya ng’ombe anaofuga kwenye shamba lake kijijini Msoga Bagamoyo.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->