Wakulima wa eneo la Afrika Mashariki walima mkonge ili kukabili hali ya ukame

by Pius Sawa | Thomson Reuters Foundation
Monday, 10 March 2014 00:15 GMT

Alex Odundo demonstrates how a hand operated machine makes twine from sisal fiber. THOMSON REUTERS FOUNDATION/Pius Sawa

Image Caption and Rights Information
An innovative local machine that quickly processes sisal fibre is building resilience to drought for farmers in Kenya, Tanzania and Rwanda

KISUMU, Kenya – Mwanabiashara mhandisi nchini Kenya ametengeneza mashine ambayo inawezesha wakulima kukabiliana na hali ya kubadilika kwa hewa na kupata faida kwa kuanzisha ukuzaji wa mkonge, zao ambalo lina uwezo wa kunawiri katika maeneo yenye ukame, na halihitaji mbolea.

Alex Odundo, mwenye umri wa miaka 36, anakumbuka namna wazazi wake walishughulika kupata chakula kutoka shamba dogo ambalo lilikumbwa na ukosefu wa mvua, na hivyo kuwalazimu kukata miti ili kuchoma mkaa kwa ajili ya kujimudu kimaisha.

“Kipande kidogo cha shamba katika kaunti ya Migori, hakikuweza kuzalisha zaidi ya magunia mawili ya mahindi na maharagwe ambayo yalikuwa chakula pamoja na pato la pesa,” alisema Alex.

Hali imekuwa mbaya zaidi kwa wakati huu katika maeneo kame nchini Kenya ambapo miti imekatwa na kupelekea mmomonyoko wa udongo.

“Mvua inaweza kuwa nyingi zaidi na ukipanda, mbegu hazioti, na kukiwa na ukame, hali huwa mbaya na hakuna mmea unaoweza ota,” alisema James Marewa, anayemiliki ekari nne za shamba katika wilaya ya Game, kaunti ya Kisumu.

KUTOKA KWA KAMBA HADI KWA KUNI.

Zao moja ambalo limeweza kustawi hali ya ukame katika maeneo haya, ni mkonge. Familia nyingi zimekuwa zikitegemea mkonge kwa kiasi kidogo kama pato, kutengeneza vikapu na kamba. Mmea wa mkonge pia huzuia udongo kusafirishwa na maji wakati wa mvua, na mti wake hutumika kama kuni wakati zao hilo limezeeka.

Lakini uvumbuzi wa Odundo umebadilisha hali ya maisha ya jamii nyingi katika eneo hili, ambapo zao la mkonge limegeuzwa kuwa lenye faida kubwa kwa watu wa maeneo ya Nyanza, Kaskazini mashariki na pwani ya Kenya.

Mashine ya Odundo hugeuza majani ya mkonge na kuwa kamba kwa haraka zaidi ikilinganishwa na mbinu za kitamaduni. Mashine moja inaweza kuchanua tani moja ya kamba ndani ya siku tano, huduma ambayo ina uwezo wa kuwahudumia wakulima watano.

Odundo alianza uvumbuzi wake mwaka 1998 akiwa mwanafunzi katika chuo cha ufundi cha Kisumu na ni mwaka 2011 ndipo aliweza kuunda mtambo unaotumika sasa. Aina moja hutumia petroli na nyingine hutumia umeme.

Odundo ameuza mitambo 40 kwa wakulima nchini Kenya, Tanzania na Rwanda, wengi wakiwa makundi ya wanawake na vijana. Anasema wakulima wengi nchini Tanzania wameagiza mashine hiyo kwa sababu zao la mkonge linakuzwa kwa wingi huko, kufuatia ufadhili wa shirika la kimataifa la Oxfam.

“Nimeuza mashine katika maeneo ya Nyanza, Machakos, Mwingi, Nairobi na pwani ya Kenya,” alisema Oundo. Yeye huza mashine moja kwa shilingi elfu themanini, karibu dola elfu moja za Kimarekani, na anatumai kwamba bei itashuka pale atakapoanza kuunda mashine hizo kwa wingi.

“Nilianzisha hii ili kuitumia ardhi iliyolala katika maeneo yenye ukame. Niliona kuwa wakulima wengi hupanda mimea lakini hawapati mavuno ya kutosha kwa sababu ya ukosefu wa mvua,” alisema Odundo. “Nilifikiria juu ya mmea ambao ungewasaidia, kwa sababu mvua inapokosekana, wao hukata miti na kuchoma mkaa ili kupata pesa.”

Hadi sasa, ni zaidi ya wakulima 20,000 katika maeneo tofauti nchini Kenya wanaopanda mkonge na wanapata faida kubwa. Odundo asema takriban hekari 10,000 zinalimwa zao hili kote nchini, na idadi inazidi kuongezeka.

KUTOKA KWA WANYAMA WAHARIBIVU HADI UMAARUFU.

Marewa alikuwa na ekari moja ya mkonge kwa miaka mingi, na wakati mmoja jirani zake walimshtaki kwa chifu wakimtaka ang’oe shamba lote kwa msingi kuwa mkonge ulikuwa hifadhi ya wanyama wanaoharibu mimiea yao.

Na hapo ndipo Odundo alipeleka mtambo wake kwa bwana marewa.

“Nilimlipa shilingi elfu arubaini pesa taslimu kwa shamba lote la mkonge,” alisema Oundo, ambaye alikata makonge hayo na kutumia mtambo wake kuyachana na kusafirish hadi jijini Kisumu na kutumia mashine nyingine aliyo ibuni na inayo tenda kazi kwa kutumia mkono katika kugeuza nyuzi na kuwa Kamba.

Odundo anazidisha juhudi za kuwahamazsisha wakulima kununua mashine ya kutengeneza kamba inayotumia mikono kwa sababu kilo moja ya kamba zilizotengenezwa inauzwa kwa shilingi 140, ikilinganishwa na kamba mbichi ambayo huuzwa tu kwa shilingi 25 kwa kilo.

 Jirani zake Marewa, wameanza kulima mkonge baada ya kushuhudia akipata pesa nyingi. Mkonge huchukua miaka mitatu kukomaa na kila zao hukatwa mara tatu kwa mwaka, na mkulima hupata shilingi 150,000 na zao moja hudumu kwa miaka kumi.

Wakulima watano tayari wananunua makonge yaliyochanwa kutoka kwa wakulima wadogo na kuuza jijini Nairobi. Kila mmoja huuza tani mia moja ya kamba kwa mwezi.

Kwa kawaida makonge hutumika kutengeneza kamba, mifuko, vikapu, na hata viti, ilhali kimataifa, makonge hutumika kutengeneza makaratasi ya kuandikia, nguo, magari, na hata sarafu za makaratasi.

Wakulima Aska Dian’ga kutoka kaunti ya Siaya County, na Rose Nyawira Pesa pamoja na Reuben Okang’s, wote kutoka  Migori, ni miongoni mwa wakulima wanaopata faida kutokana na kilimo cha mkonge.

“Nilihudhuria mkutano ambapo bwana Alex alikuwa akiwashauri wakulima juu ya zao la mkonge. Wengi walidharau lakini mimi nilianza kupanda moja kwa moja, na sasa kila mtu ananiomba mbegu,” alisema Rose Nyawira ambaye sasa analima akeri mbili za mkonge, na hana shida za kuwaelimisha wanae na kununua chakula.

Odundo anasema kuwa mabadiliko ya tabianchi, yanamfanya mwanadamu abuni njia za kujimudu na anawashauri wakulima kutenga sehemu ya mashamba yao kwa chakula kwa sababu mvua inaweza ikarudi.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.