×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Nyumba maalum zasaidia kuzuia magonjwa vijijini Kenya

by Kagondu Njagi | @DavidNjagi | Thomson Reuters Foundation
Thursday, 10 April 2014 14:14 GMT

Poor communities are hardest-hit by vector-borne diseases like leishmaniasis, and climate change could make things worse unless they get more help to adapt

BARINGO, Kenya (Thomson Reuters Foundation) – Nguvu za upepo zinazopepea kwa ukali huko nyumbani mwa Helen Chepkirilo ni ishara kwamba mvua haitanyesha au ukame unakaribia. Siku hizi, yeye amejua kwamba upepo pia unaweza kuleta magonjwa.

Mtoto wake Chepkirilo mwenye umri wa miaka saba, Kapoyon Richard, anatibiwa ugonjwa unaoitwa kwa kimombo visceral leishmaniasis, ama kala-Azar, katika hospitali ya Kimalel baada ya kuumwa na mdudu anayesababisha huu ugonjwa.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani (WHO), kala-Azar yaweza kuua kama haijatibiwa. Dalili zake ni kikohozi ya homa, kupoteza uzito, upanuzi wa wengu na ini, na upungufu wa damu. Inapatikana sana katika bara hindi na Afrika Mashariki, na inakadiriwa watu elfu mia mbili hadi elfu mia nne wanagonjeka kila mwaka.

“Wadudu hawa hutuvamia usiku kwa urahisi baada ya kuletwa na upepo kwa manyumba zetu,” alielezea Chepkirilo. “Hata tukilala chini ya chandarua, wadudu hawa bado hupita na kutuuma.”

Mama huyu mwenye umri wa miaka arobaini na watoto saba, si yeye pekee anayesumbuliwa na kala-Azar katika sehemu hii maskini ya Kenya. 

Mamia walikufa kutokana na maambukizi kabla ya madaktari kugundua kiwango cha maambukizi mwaka elfu mbili na nane, wakati wengi wao pia walishidwa kufika hospitali mapema kupata matibabu.

Hata hivyo, mapambano dhidi ya ugonjwa huu yameleta ubunifu katika jamii. Chepkirilo ni mmoja wa idadi kubwa ya jamaa yake katika kijiji cha Loruatu ambao wanajenga nyumba nadhifu kuzuia mdudu huyu, unaohusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hivi karibuni, wataalam waliambia Chepkirilo na wengine kwamba mdudu huyu anapenda kukaa mahali penye hali ya hewa inayobadilika kati ya joto na baridi. Mdudu huyu anapenda kuzaa wakati kuna joto lakini anapenda lishe wakati wa baridi, kwa mujibu wa shirika la taasisi la Kenya, KEMRI.

WHO nayo yaeleza kwamba ugonjwa huu unaweza kusababishwa na mabadiliko ya mvua, joto na unyevunyevu. Ongezeko la joto duniani na uharibifu wa ardhi unaweza kusababisha kuenea maeneo mbalimbali au kuharibu kinga ya mwili, yasema.

MBALI NA UPEPO, MCHWA HAKUNA

“Tunahamasisha (watu) kujenga nyumba mbali na njia ya upepo ili kuzuia wadudu kuletwa ndani na barugumu,” alisema Mark Rotich, afisa wa afya anayeshughulika na udhibiti wa mazingira ya mdudu huyu katika Marigat, mji ulio kata ya Baringo.

Ubunifu rahisi wa kimazingira pia unahusisha kubomoa mahali ambapo mdudu huyu anayeitwa Sandfly, anapenda kuzalia na kuanzisha miradi ya kilimo,” Rotich aliongeza.

Huko Kijiji cha Entebbes kama kilomita saba kutoka mjini Marigat, Johannes Makoko, aliye na umri wa miaka ishirini na mbili, ameamua kupambana na Sandfly.

Yeye ni miongoni mwa wanakijiji wanaotumia maji ya mto Perkerra kuanzisha mashamba katika maeneo ambayo yameathriwa na nyumba za wadudu hawa, ambazo zinaitwa kwa kimombo, anthills.

Katika kanda ambapo kulinda mifugo ni shughuli kuu ya kiuchumi, Makoko amefanya uadui kwa kuonyesha utamaduni wa jadi wa ufugaji kisogo. Lakini hana majuto.

“Wakati wavulana wanalinda mifugo jangwani wanaumwa na mdudu huyu,” Rotich Alisema. “Wasichana pia wanaadhirika wakati wanatembea umbali kuchota maji na kukusanya kuni. Hii ndio sababu kala-Azar inapatikana sana kwa vijana.”

WEKA NG’OMBE KARIBU

Madaktari wanaamini kwamba kudhibiti vyanzo vya magonjwa yanayotokana na wadudu ni hatua fanisi zaidi na kuyapunguza. Hata hivyo, watafiti wanazidi kupinga matumizi ya kemikali kama vile dawa ya wadudu, ambayo wanasema inaadhiri mazingira.

Mjini Nairobi katika kituo cha kimataifa cha utafiti wa wadudu, ICIPE, wanasayansi wanachunguza maeneo manne yanaoathirika na mabadiliko ya hali ya hewa: binadamu, mimea, mazingira, na afya ya mifugo.

Lengo lao ni kujaribu njia nafuu na zinazolinda mazingira kuzuia magonjwa katika maeneo pembezoni, mbinu inayoitwa kwa kimombo, Integrated Vector Management (IVM).

Kwa mfano, zooprophylaxis - mbinu ambayo hutumia wanyama kama ng’ombe kuzuia wadudu inaonekana kuwa maridadi, asema Clifford Mutero, mtafiti huko ICIPE.

“Baadhi ya wadudu hupenda kunyonya ng’ombe damu badala ya binadamu. Ng’ombe hawaathiriki na magonjwa ya zinaa ya wadudu hawa, hivyo vimelea katika wadudu watakufa wakiwa katika mwili wa ng’ombe,” Mutero alieleza.

Huko kijijini Chepkiriro, wenyeji kama Kepkong’en Birr wasema ujengaji wa wigo za mifugo ni utamaduni wa jadi. Lakini lengo lilikuwa kulinda wanyama kutoka ibiwa na wezi, badala ya watu kutokana na wadudu.

Mzee huyu mwenye umri wa miaka sitini sasa amejenga wigo linalozingira nyumbani kwake ambapo mbuzi na ng’ombe wake hupumzika usiku.

“Mimi nilifanya hivi kulinda familia yangu kutokana na Sandfly. Wanaafya wa jamii walikuja kijijini hiki na kutuonyesha njia hii. Nadhani inafanya kazi,” alisema Birr, huku akionyesha uso sugu ambao asema haujaumwa kwa wiki moja.

JAMII MASKINI ZAPAMBANA KATIKA KUKABILIANA

Licha ya matumaini haya, kuna baadhi ya wanaoshuku makabiliano haya yatafanya kazi bila ya serikali kushughulikia jamii maskini.

Jasmine Tibae, mwanaafya wa jamii, asema kuna wengi hawajasoma katika vijijini Kenya, ambapo yeye analaumu kwa umaskini.

WHO yasema ugonjwa huu huathiri watu maskini, na huhusishwa na utapiamlo, kufukuzwa makaazi, makaazi duni, kinga dhaifu na ukosefu wa rasilimali. Pia inahusishwa na mabadiliko ya mazingira kama vile ukataji miti, ujenzi wa mabwawa, miradi ya umwagiliaji kilimo, na ongezeko la watu mijini.

Asilimia themanini ya ardhi Kenya ni kame. Mwaka wa elfu mbili na kumi na mbili, serikali ilizindua chombo cha mabadiliko ya hali ya hewa kiitwacho T21, ili kuwezesha miradi ya kukabiliana na hali hii, hasa maeneo kame.

Kwa mujibu wa wizara ya mazingira na rasilimali za madini, lengo la T21 ni kuimarisha taasisi na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa hatari kupitia njia za kitaifa.

Itakuwa bora kama watu kama Chepkirilo watalindwa na T21 na vyombo vingine vya kukabiliana na hali ya hewa katika maeneo duni. Lakini kwa sasa, ukosefu wa barabara, umeme na mitandao ya simu ya mkononi, inazuia, maafisa wasema.

Kagondu Njagi ni mchangiaji wa kujitegemea kwa Thomson Reuters Foundation, mjini Nairobi na huandika juu ya maswala ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->