×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Huku Umeme wa Maji ukisuasua, Tanzania yageukia gesi asilia

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Wednesday, 24 September 2014 12:00 GMT

A man inspects a tanker waiting to offload heavy furnace oil at the Independent Power Limited plant in Dar es Salaam in September 2014. THOMSON REUTERS FOUNDATION/Zuberi Mussa.

Image Caption and Rights Information

Country will end contracts with private energy suppliers used to meet shortfalls, and invest in natural gas electricity

Na Kizito Makoye

DAR ES SALAA, Tanzania, Septemba 24 (Thomson Reuters Foundation)—Baada ya miongo kadhaa ya kutegemea kampuni binafsi za uzalishaji umeme wa dharura, Tanzania imedhamiria kutumia mashine zinazotumia gesi kuzalisha umeme huku nchi hiyo ikinuia kutumia kiwango kikubwa cha gesi kuzalisha umeme rahisi.

Katikati ya ukame unaojirudia mara kwa mara uliodhoofisha mitambo ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji, taifa hili la Afrika Mashariki linajaribu kuongeza vyanzo vyake vya nishati-hata hivyo kwa gharama ya uchafuzi mkubwa wa mazingira.

Hatua ya kuzima mitambo inayotumia mafuta mazito huenda ikaokoa TANESCO, shirika la umeme la taifa, kiasi cha Shilingi za Tanzania 1.6 trillioni (dola 1 billioni) kila mwaka, serikali imesema.

Eliakim Maswi, katibu mkuu wizara ya Nishati na Madini amesema mpango huo unakusudia kupunguza gharama na kuruhusu Tanzania kutumia rasilimali gesi yake.

“Tunataka kuhakikisha kwamba tuna umeme wa kutosha kwa gharama nafuu ili uma ufurahie bei nafuu,” alisema.

Ingawa kiwango cha hewa ukaa kinachozalishwa Tanzania kingali ni kidogo sana, wataalam wanasema mikakati ya kuendeleza sekta ya nishati inayoendelea –kama vile matumizi ya makaa ya mawe na gesi asilia—pengine inaweza kuizingira nchi hii na kuifanya izalishe hewa chafu kwa wingi.

Kwa mujibu wa utafiti wa serikali kuhusu uchumi wa mabadiliko ya tabianchi, kiwango cha gesi ukaa kinachozalishwa Tanzania kwa mwaka huenda kikaongezeka maradufu kufikia tani za metriki 1.5 za gesi ukaa ya kaboni kufikia 2030.

Tanzania kwa miaka kadhaa sasa imesumbuka mno na ukame unaoendelea unaoathiri uzalishaji wa umeme wa maji kiasi cha kusababisha mgao wa umeme.

Ili kukabiliana na tatizo hilo, serikali ililazimika kuazima mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura kutoka kampuni binafsi kama vile Aggreko na Symbion Power LLC kufua megawati zaidi ya 300 kila siku kwa mkataba wa muda mfupi—kiasi cha moja ya tano ya uzalishaji wote.

Symbion imekuwa ikifanya upanuzi wa shughuli zake kuanzia mwaka 2012 kuzalisha takribani megawati 225 kila siku kwenye viwanda vyake vilivyopo Dar es salaam, Arusha na Dodoma.

 

Uwezo huo wa uzalishaji kwa sasa utasitishwa kwa kuwa Tanzania imejenga kiwanda cha kuzalisha umeme wa gesi, serikali imesema. Mradi huo wenye thamai ya shilingi bilioni 240 za kitanzania (Dola18 million) unajengwa huko Kinyerezi Dar es salaam, unategemewa kukidhi asilimia 20 ya mahitaji ya umeme.

TISHIO LA KUZIMA UMEME?

Wadadisi wa mambo hata hivyo wameonya kwamba kukurupuka kuzima mitambo ya mafuta huenda kukaathiri uchumi.

“Nijuavyo mimi, TANESCO imeingia makubaliano na kampuni hizo binafsi. Nina uhakika kampuni hizo hazita simama kando kuona mikataba yao minono inavunjwa. Ni lazima wataanzisha vita ya kisheria  dhidi ya hatua yoyote ya kusitisha mikataba yao,” alisema Evans Mzava, mtafiti na mtaalam mshauri wa mambo ya nishati wa Dar es salaam.

Hata hivyo, Maswi, wa wizara ya madini amesema serikali haitakiuka maelezo yaliyomo kwenye mikataba na kampuni hizo.

Tanzania ina gesi asilia kiasi cha futi za ujazo trillion 50—tosha kabisa kubadili mwenendo wa maendeleo ya nchi hii na kuondoa utegemezi katika nishati, serikali inasema.

Kwa sasa gesi asilia inatumika kuzalisha robo tu ya umeme wote Tanzania, huku umeme wa maji na nishati nyingine zikichangia kiasi kama hicho.

Ingawa wachambuzi wa mambo ya mazingira wanaonya kwamba matumizi makubwa ya vichocheo ukaa kuzalisha umeme huenda yakaongeza hewa ukaa na kuchangia kwenye mabadiliko ya tabia nchi, na hali mbaya ya hewa, serikali inaendelea na mipango yake kabambe.

Katika mkakati wake wa 2014-25 unaojulikana kama Electricity Supply Industry Reform Strategy, uliozinduliwa mapema mwaka huu, serikali imesema itatumia vyanzo mbadala kuzalisha umeme ikiwa ni pamoja na makaa ya mawe na gesi kuongeza uzalishaji kutoka megawati 1583 hadi megawati 10,800 miaka kumi ijayo.

Wateja wadogo na wakubwa wa nishati wanakabiliwa na ongezeko la gharama za umeme kwa asilimia 40 kuanzia mapema mwaka huu ikiwa ni matokeo ya kile serikali ilichokiita kuongezeka kwa gharama za uendeshaji.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Felchesmi Mramba, kuanza kwa miradi ya gesi kutapunguza maradufu gharama za umeme kwa kuwa shirika hilo la ugavi wa umeme litaweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kuzalisha nishati ya kutosha bila ya kununua kutoka kampuni binafsi.

Kwa sasa ni asilimia 24 tu ya watanzania wameunganishwa kwenye gridi ya taifa. Vijijini ni asilimia 7 tu ya wanavijiji wana umeme kutokana na kipato kidogo. Serikali imenuia kuongeza  uunganishwaji umeme mpaka asilimia 30 kufikia mwaka 2015.

(Mwandishi ni Kizito Makoye; Mhariri  Laurie Goering)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->