×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Wakulima Kenya waunga mswada wa kura ya maoni ili kuitisha msaada zaidi

by Kagondu Njagi | @DavidNjagi | Thomson Reuters Foundation
Monday, 20 October 2014 08:26 GMT

Miriam Kinyua prepares a meal in Rukindu village in Eastern Kenya using an energy-saving cooker. TRF/Kagondu Njagi

Image Caption and Rights Information

Referendum supporters want government to hand down more aid for communities tackling climate change, poverty

RUKINDU, Kenya (Thomson Reuters Foundation) – Haijawahi kuwa kawaida kwa Miriam Kinyua kupinga mamlaka, lakini siku hizi, mama huyu wa watoto sita hawezi kujizuia. Yeye ni mojawapo wa idadi inayoongezeka ya wakulima maskini ambao wanatoa wito wa kura ya maoni ili kuboresha maisha yao chini ya mfumo wa serikali ya Kenya ya Kaunti.

Wengi wajihisi wameachwa nyuma wakati nchi inakabiliana na kuendeleza miundombinu, huku ikijaribu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kijijini mwake, Rukindu, katika mashariki mwa Kenya, Kinyua lazima aamue kama ni kulinda miti iliyo shambani mwake ya hekari tatu, ama ni kuhakikisha ako na kuni za kutosha za kuandaa chakula kwa familia yake inayozidi kupanuliwa na wategemeaji.  

“Siwezi kukata miti ili niweze kuwa na kuni za kutosha,” alisema Kinyua. “Nikifanya hivyo mimi nitakamatwa na Chifu kwa sababu ni kinyume cha sheria hata kama mti uko kwangu.”

Kinyua ahisi serikali haijamuhudumia. Lakini anapotafuta ushauri kutoka kwa wazee wa kijiji, wao humwambia si jukumu la mwanamke kujihusisha na masuala ya ardhi. Yeye akilalamika kwa Chifu wa kijiji, utawala wa ndani wasisitiza kuwa unafuata sheria.

Huko ofisini mwa Kaunti ya Tharaka Nithi, yeye hushawishiwa kwamba lazima angojee sheria iliyo wazi kwa masuala ya wakulima, kilimo na mabadiliko ya hali ya hewa. Lakini subira yake inaisha.

‘SISI HATUNA CHOCHOTE’

Kinyua aunga kura ya maoni ambayo inaungwa mkono pia na baadhi ya wanasiasa, ili kubadilisha Katiba ya Nchi ambayo ilipitishwa mwezi wa Agosti mwaka wa elfu mbili na kumi. Baadhi ya upigaji kura ni kuhakikisha serikali ya kitaifa imewajibika zaidi jinsi fedha ya maendeleo na mabadiliko ya hali ya hewa inagawa.

“Katiba ilipatia watu sauti, lakini iliwapa wenye nguvu katika jamii njia rahisi ya kutumia rasilimali ya umma. Sisi hatuna chochote.” Kinyua alisema.

Katiba ya ugatuzi iliwezesha serikali za Kaunti kukusanya fedha kupitia ushuru wa wao wenyewe, lakini serikali kuu bado yasimamia jinsi fedha inavyotumika, mashirika ya utetezi yasema.

Zaidi ya hayo, Katiba haina uwazi kuhusu kama ni jukumu la serikali ya kitaifa ama ya Kaunti kusimamia rasilimali ya jamii kama ardhi, maji na misitu, wanadai.

Asilimia arobaini na tano ya shillingi bilioni mia tatu na hamsini za Kenya, (dola zipatazo bilioni tatu nukta tisa,) zilizotengewa serikali za Kaunti kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuboresha usalama wa lishe, maji na miundombinu, bado haijatolewa na serikali ya kitaifa tangu ilipoingia madarakani mwezi Aprili mwaka wa elfu mbili kumi na tatu, waliongeza.

Sheria ya mabadiliko ya hali ya hewa iliyopitishwa mwaka wa elfu mbili kumi na mbili ilikataliwa na Rais, huku ikidaiwa mchakato wa kuunda hii sheria ulikosa ushiriki wa wananchi. Sheria hii ingekuwa na nguvu ya kutafuta fedha kwa ajili ya miradi ya kukabiliana na hali ya hewa katika ngazi za kitaifa na jamii. Pia ingekuwa na mamlaka ya kisheria kwa jamii zilizotengwa kwa miradi ya maendeleo na mazingira.

“Wito wa kura ya maoni ni kwa sababu rasilimali hazifikii Wakenya katika sehemu mbalimbali za nchi,” alieleza Isaac Ruto, mwenyekiti wa baraza la tawala la kanda, ambalo linaunga kampeni ya kura ya maoni.

Pia inahusisha wanasiasa kutoka chama tawala na vyama vya upinzani. Saini zakusanywa ikitumainiwa zitachochea mjadala Bungeni. Pande ile itashinda itaamua kama itaitisha kura ya maoni juu ya katiba.

SERA KUTOLEWA KUTOKA JUU

Ruto, mbunge kutoka kijiji cha Bomet huko bonde la ufa, baadhi kilomita mia tano ama maili mia tatu na kumi kutoka nyumbani mwa Kinyua huko Rukindu, aelewa malalamishi ya mama huyu.

Eneo la Bomet lina mito mingi, lakini mpango wa serikali ya kitaifa wa kuchimba visima huko ili zitumiwe kwa kilimo cha maji na matumizi ya nyumbani haitakidhi mahitaji ya watu, alisema.

“Tunachohitaji hapa ni kuwekewa mabomba ya maji kutoka kwenye mito,” alisema. “Serikali ya kitaifa haina fahamu ni nini kinachotendeka katika jamii, lakini wao ni kutuwekea tu sera.”

Kulingana na Ruto, mama ishirini na moja hufa Kenya kila siku kutokana na ukosefu wa chakula na maji.  Hali duni ya barabara, ambayo hufurika wakati wa mvua, inafanya kuwa vigumu kwa wakulima kupeleka mazao yao kwa soko, na kwa watu kupata huduma za afya.

“Tunataka kulinda madaraka ili yaweze kuwahudumia watu wanaoishi pembezoni,” alisema Ruto.

Si kila mtu anakubali.

Wakosoaji wa kura ya maoni wasema hii ni njama ya kisiasa ya kuvuruga utendaji wa serikali na kusambaratisha amani Kenya.

“Kushinikiza kwa kura ya maoni ni njama na vikosi mbaya kuvunja utulivu Kenya,” alisema Seneta Kipchumba Murkomen. “Maskini ndio wanateseka kutokana na siasa za kuendeleza vita.”

Migogoro juu ya usimamizi wa rasilimali ni vita kati ya serikali kuu na Tume ya Taifa ya Ardhi, maalumu, aliongeza.

Kwa sasa, maskini Wakenya vijijini hawana imani katika uwezo wa serikali kuwasaidia. Wengine watafuta msaada kupitia miradi inayoongozwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, ama NGOs.

NJIA ZA KIJAMII ZAHITAJIKA

Asubuhi ya baadaye katika Rukindu humpata Kinyua akiandaa mlo wa siku. Huku akijiimbia anapoendelea na shughuli zake, yeye achukua vijiti viwili vya kuni na kutumbukiza kwa jiko linalookoa nishati, ambalo alinunua hivi karibuni kutoka kikundi cha Carbon Two Balance, na ambalo si la kiserikali.

Kuni hizi zitawaka muda wa kutosha na kuandaa chakula cha mchana na jioni, alieleza. Kabla ya hapo, yeye hangeweza kukusanya kuni ya kutosha ya kutumia kwa jiko la jadi.

“(Jiko hili jipya) ni safi, lina haraka na huokoa kuni,” alisema mmewe, Joseph Kinyua Mung’ori, huku akiongeza kuwa halitoi moshi hivi kusaidia watoto kuepukana na maambukizi ya macho.

Mung'ori anataka serikali ya Kaunti kufanya miradi zaidi ambayo inabadili maisha, huku ikinufaisha kila mtu. Lakini bado haina huu uwezo, anaamini.

Kuboresha maisha ya watu ingeleta faida ya kiuchumi kwa serikali za mitaa kwa sababu hakungekuwa na tatizo la chakula cha msaada wakati ukame unapoingia, alisema.

(Imesahihishwa na James Baer na Megan Rowling)

Kagondu Njagi ni mchangiaji wa kujitegemea kwa Thomson Reuters Foundation, mjini Nairobi na huandika juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->