×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Je, fedheha itachangia Kenya kutozalisha kawi kutoka kinyesi cha binadamu?

by Justus Wanzala | Thomson Reuters Foundation
Monday, 24 November 2014 10:50 GMT

Biogas from human waste could be a big source of renewable energy – but it comes with some issues

NAIROBI (Thomson Reuters Foundation) – Huku Kenya ikitafuta njia mpya za kuzalisha nishati safi, imegeukia jua, upepo, joto la ardhini na gesi kutoka kinyesi cha wanyama.

Sasa inatupia jicho njia nyingine ya ziada ya kuzalisha kawi: kinyesi cha Binadamu.

Kikiwa kinapatikana kwa urahisi, kinyesi cha binadamu kinaweza kugeuzwa kuwa gesi, yaani biogas na kutumika kwa ajili ya kupikia au kuzalisha umeme.

Huku mamilioni ya watu wakiishi katika makazi duni nchini Kenya, na kuzalisha tani milioni nne  za kinyesi kwa mwaka, kulingana na makadirio na takwimu za wataalam, uwezekano wa kuzalisha gesi ya biogas ni mkubwa sana. Mbali na kuzalisha nishati safi, ukusanyaji na matumzi ya kinyesi hicho unaweza kusaidia kupunguza matatizo ya usafi wa mazingira nchini Kenya.

Lakini kampuni za nishati zinazonuia kuwekeza katika kinyesi cha binadamu zinakumbwa na  changamoto mbili kubwa: gharama na unyanyapaa.

Sanergy, ambayo ilianzishwa mwaka 2012, inamiliki mtandao wa vyoo vidogo katika mtaa wa makazi duni wa Mukuru jijini Nairobi.  Vyoo hivyo viliyoundwa kwa ajili ya matumizi ya watu  80-100 kwa siku, usimamizi wake umekabidhiwa wakazi.

Kinyesi hukusanywa kila mara na kubebewa kwenye ndoo maalum zinazozibwa na kupelekwa katika kituo kikuu. Taka hiyo huhifadhiwa katika vinu maalum au biodigesters ambapo hutoa gesi aina ya methane, inayoweza kutumika kama kawi.

Vinu hivyo pia huondoa viini vinavyoweza kusababisha maradhi na hivyo basi huwezesha mabaki ya kinyesi kutumika kama mbolea.

Tani moja ya kinyesi cha binadamu inaweza kuzalisha mita 0.6 za ujazo wa gesi ya biogas. Sanergy tayari imekusanya tani 2,700 za  kinyesi cha binadamu kutoka Mukuru, na kuzalisha nafasi 122 za ajira katika mtaa huo wa mabanda.

Wataalam wa nishati wanasema kwamba utakapokamilika mradi wa kuzalisha gesi ya biogas wa  kampuni ya Sanergy, utakuwa na uwezo wa kuzalisha kilowatts 250 za umeme.

"Mradi huo una uwezo mkubwa wa kuzalisha kawi ya kutumika na taa za kutoa mwangaza kwa  mtaa  huo duni na pia kawi ya bei nafuu kwa wake kwa ajili ya kupikia," alisema Edith Karimi, mkuu wa mawasiliano wa kampuni ya Sanergy. Kampuni hiyo pia inafanya majaribio ya kuzalisha umeme wa kutosha kuuza ili ujumuishwe  katika gridi ya taifa.

Miradi ya kuzalisha kawi kutoka kinyesi cha binadamu imekuwepo nchini Kenya na tayari inaendelea katika baadhi ya makaazi duni na maeneo mengine kama vile katika shule kadhaa; lakini miradi mikubwa kama vile ule wa Sanergy – imewekezwa fedha nyingi na kuwapa wananchi matarajio makubwa -  hivyo basi, inatumainiwa kuwa italeta faida zaidi.

'VYOO VYA KURUKA'

Wakazi wa mitaa duni nchini Kenya kwa mara nyingi hawapati huduma bora za usafi wa mazingira, huku wengi wakitegemea vyoo vya umma, ambayo ni adimu, au kuchimba vyoo vyao wenyewe huku mashimo yakieelekezwa  katika mitaro ya  maji ya mvua na mito na hivyo basi  kuchafua mito.

Njia nyingine inayotumiwa na wakazi hao ni  "vyoo vya kuruka" - mifuko ya plastiki ndogo inayojazwa kinyesi cha binadamu na hurusha nje ya madirisha na kutapakaa kila mahali .

Kwa kuangazia uzalishaji wa kawi kutoka kwa kinyesi,  Sanergy na kampuni zinginge zinalenga  pia kutatua tatizo la usafi wa mazingira nchini Kenya.

Kampuni ya Kawi ya Afrisol, yenye makao yake katika  Kituo cha Kubuni Teknolojia za Kukabiliana na Mabadiliko ya Hali Hewa nchini Kenya (KCIC) kilichoko kwenye  Chuo Kikuu cha Strathmore jijini Nairobi, kwa ushirikiano na kampuni ya nishati ya Marekani ya General Electric  inajenga maalum  choo cha kuzalisha gesi ya biogas katika shule ya Msingi ya Kwa Njenga iliyoko mtaani Mukuru.

Mradi huo ambao umepangiwa kukamilika mwezi Desemba, utagharimu Dola laki moja za Marekani na utawahudumia wanafunzi 2,000 wa shule hiyo na unapaswa kuzalisha mita za ujazo 4.5 za gesi ya biogas kwa siku. Gesi hiyo itatumika kuzalisha mvuke utakaoendesha mitambo ya kuzalisha umeme utakaotumika shuleni na pia kuwafaa wakazi wa eneo jirani.

Amos Nguru, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Afrisol, anaamini, kinyesi cha binadamu kinafaa kuchukuliwa kwa umakini zaidi katika sekta ya kawi endelevu.  Gesi inayotoka kwa kinyesi cha binadamu aina ya Methane hujumuisha gesi nyingi ya Kaboni ambayo huchangia  joto zaidi inapoingia angani, lakini iwapo itahifadhiwa vyema ili kuepuka uvujaji, inaweza kuwa  mbadala na safi ikilinganishwa na gesi yenye asili ya kaboni kama vile mafuta na makaa ya mawe.

"Kenya ina uwezo wa kuzalisha kilowatt elfu 10,000 kwa siku kutoka kwa gesi ya biogas inayotokana na kinyesi cha binadamu," alisema Nguru.

GHARAMA - NA UNYANYAPAA  WA KIJAMII

Mojawapo ya vikwazo vinayoathiri kusambaa kwa teknonojia ya kuzalisha gesi kutoka kinyesi cha binadamu ni gharama ya juu ya ujenzi wa vinu vya kuzalisha gesi hiyo kwa kiwango kikubwa.

Nguru anasema kuwa vyuo vikuu na taasisi za utafiti havijakuwa katika mstari wa mbele kukuza teknolojia ya kuzalisha gesi hiyo - “huku kampuni ndogondogo zikisongwa na ukosefu wa fedha."

Alisema kuwa taasisi za kifedha pia zinasita kuwafadhili wanaolenga kuwekeza katika uzalishaji wa gesi ya biogas kwa  dhana kuwa zitapata  hasara.

Lakini  Caesar  Mwangi, mkurugenzi wa Afrika wa kikanda wa Shirika la Global Village Energy Partnership (GVEP), ambalo linashiriki katika kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala katika nchi zinazoendelea, anaamini kinyesi cha binadamu kinaweza kutekeleza jukumu kubwa katika kusaidia nchi maskini kuafikia mahitaji yake ya nishati.

"Kinyesi cha binadamu hupuuzwa kutokana na unyanyapaa lakini ni bora kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya watu na maeneo ya watu wenye kipato kidogo ambao pia hawapokei  huduma za umeme kutoka gridi ya taifa," alisema.

Hata hivyo, wanaounga mkono kawi kutoka kinyeysi cha binadamu wangali na kibarua kizito cha kuondoa dhana potovu na unyanyapaa. Nguru wa kampuni ya Afrisol alisema kwamba alipoanza kukuza matumizi ya kinyesi cha binadamu katika uzalishaji wa gesi watu wengi walidhani ni utani. "Inaonekana nilikuwa ninajitoza katika swala haramu au kwenda kinyume na mwiko kutokana na mtazamo wa kitamaduni kuhusu kinyesi cha binadamu," alisema.

Lakini katika makao ya KCIC, wataalam wanakuza kukubalika kwa miradi ya kuzalisha gesi ya  biogas kutoka kinyesi cha  binadamu.  Hata hivyo, juhudi zao zote zitaangamia patupu iwapo hawataweza kuwashawishi Wakenya kwamba kinyesi hicho kina faida, asema  David Ngugi, mchanganuzi wa teknolojia kutoka  KCIC.  

"Mingi ya miradi hiyo inaendeshwa katika mitaa duni ambapo wakazi hutumia 'vyoo vya kuruka'," anasema. "Wao hawaoni kinyesi chao kuwa cha thamani."


(Taarifa ya Justus Wanzala, mhariri: Laurie Goering)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->