×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Uzalishaji wa kahawa Tanzania waporomoka kutokana na ongezeko la joto

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Monday, 27 April 2015 05:37 GMT

Without effective adaptation efforts, production could halve by 2060, study says

DAR ES SALAAM (Thomson Reuters Foundation) — Ongezeko la hali ya joto lina maana kwamba Tanzania itakuwa ikizalisha kahawa pungufu kwa kuwa joto linadhuru uzalishaji, kiasi cha kuathiri wazalishaji wa zao hilo na wanywaji wa kahawa ambao huenda  wakalipa zaidi kwa kila kikombe, utafiti uliofanywa na chuo kikuu cha Afrika Kusini wabaini.

Kwa mujibu wa andiko lililofanywa na chuo kikuu cha Witwatersrand, watafiti kwa mara ya kwanza wamejua kwamba ongezeko la joto nyakati za usiku ni sababu kuu ya kuporomoka kwa zao la kahawa aina ya Arabica nchini Tanzania.

Kahawa ni zao muhimu la biashara; kwa wastani nchi inazalisha tani za ujazo 50,000 za kahawa kila mwaka kati yake takribani asilimia 70 ni aina ya Arabica. Mauzo ya kahawa huliingizia taifa  zaidi ya dola za kimarekani milioni 100 kwa mwaka, kwa mujibu wa takwimu kutoka bodi ya kahawa.

Uzalishaji kahawa pia huajiri karibu watu million 2.4 Tanzania na mamilioni wengine kutoka nchi za jirani zenye hali ya hewa inayofanana. Kwa sasa, Tanzania inazalisha asilimia 0.6 ya kahawa yote ya Arabica duniani.

Hata hivyo, toka mwaka 1966 uzalishaji wa kahawa umezorota kwa asilimia 46 nchini Tanzania—utafiti huo unatabiri mtiririko huo huenda ukaendelea. Kwa kipindi chote hicho, ongezeko la joto nyakati za usiku umepanda kwa nyuzi 1.42 centigrade.

ONGEZEKO NYUZI 1, LAPUNGUZA UZALISHAJI MARADUFU

Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapishwa kwenye jarida maarufu la kilimo na hali ya hewa, kwa kila ongezeko la nyuzi joto 1 la joto nyakati za usiku wakulima nchini Tanzania huenda wakapata hasara ya takribani kilo 137 za kahawa kwa hekari. Kiwango hicho ni takribani nusu ya uzalishaji wa wastani wa mkulima mdogo, ambao ni kilo225 kwa ekari.

Wanasiasa katika mazungumzo ya hali ya hewa umoja wa mataifa (UN) wanajaribu kushawishi kupata suluhu ya namna ya kuzuia ongezeko la joto la dunia kufikia nyuzi joto 2 za Celsius—hata hivyo dunia inaelekea kwenye ongezeko la nyuzi 4 mpaka kufikia mwisho wa karne hii, wanasayansi wanasema.

“Utabiri wetu umeonyesha kwamba kama mwenendo utaendelea kama tulivyodadisi katika miongo ya hivi karibuni, uzalishaji wa kahawa ya Arabica nchini Tanzania utaporomoka kufukia kilo 145 kwa ekari kufikia mwaka 2060, utafiti huo umeonyesha.

Watafiti wamesema tishio katika uzalishaji wa Kahawa Tanzania huenda ikatoa angalizo kwa mamlaka husika za nchi kuweka mikakati ya kukabiliana na tabia nchi zitakazo saidia kupunguza hasara kwa wakulima.

Utafiti huo, unaoangalia matokeo ya mabadiliko ya tabia nchi kwenye uzalishaji wa kahawa ya Arabica nchini Tanzania kwa kipindi cha miongo mitano, umeonya kwamba upungufu wa uzalishaji wa kahawa utaathiri vipato na kazi sio tu kwa watanzania bali pia kwa nchi nyingine zinazozalisha kahawa kama vile Kenya, Ethiopia, Brazil, Colombia na Costa Rica.

Nchini Tanzania, kahawa ya Arabica inalimwa sehemu za nyanda za juu kaskazini na kusini hasa kwenye safu za mlima Kilimanjaro na mkoa wa mbeya, ambapo wakulima wadogo wadogo ni wengi.

Alessandro Craparo, mtafiti mkuu ameiambia Thomson Reuters Foundation kwamba kama joto litaendelea kuongezeka kwa kasi ile ile kama ilivyobainika miongo michache iliyopita, uzalishaji wa kahawa nyanda za juu Tanzania utashuka kwa kilo 200 kwa heka kufikia mwaka 2030.

“Uzalishaji wa kahawa umeporomoka hadi kiwango cha chini kabisa, huku wakulima wengi nchini Tanzania wamenawa mikono kujihusisha na zao hilo,” alisema Craparo.

Hata hivyo, ameongeza kusema mabadiliko ya joto huenda yasiathiri aina nyingine za kahawa kama vile Robusta inayolimwa kwenye nyanda za chini na inauwezo mkubwa wa kustahimili hali mbaya ya hewa kuliko Arabica, alisema.

Akitoa maoni yake kwenye utafiti huo, Godsteven Maro, mtaalamu wa udongo anayefanya kazi taasisi ya utafiti wa kahawa TACRI amesema kuporomoka kwa uzalishaji wa kahawa ya Arabika huenda pia umechangiwa na sababu nyingine kama vile kuzeeka kwa miti ya mibuni, na matatizo ya sera.

“Kusema kwamba mdondoko huo umesababishwa na ongezeko la joto pekee kuna walakini,” aliiambia Thomson Reuters Foundation.

AJIRA MASHAKANI

Kwa mujibu wa utafiti huo, ingawa serikali kwenye nchi zinazozalisha kahawa zimewekeza kwenye sekta ya kahawa nyingi hazijaweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kiasi cha kuiweka sekta hiyo nyeti na ajira za mamilioni ya wazalishaji wadogo wadogo mashakani.

James Teri, mkuu wa taasisi ya utafiti wa zao la Kahawa TACRI amesema serikali imechukua hatua kadhaa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa ikiwemo kushauri wakulima wahamia maeneo ya juu ili kuendeleza uzalishaji wa kahawa bora na kwa kiwango kikubwa

“Tumeleta mbegu bora zinazostahimili hali ya hewa, na hivi sasa, wakulima wanatumia katika maeneo mbalimbali yanayozalisha kahawa.”

Haji Semboja Mkufunzi wa uchumi chuo kikuu cha Dar es Salaam  ameonya kwamba endapo mikakati madhubuti ya kukabiliana na tabia nchi haitawekwa “ athari kwa wakulima na ajira zitakuwa kubwa”.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->