×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Kuzuia wimbi la wahamiaji, Tanzania yatoa mikopo kwa wakulima

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Wednesday, 2 September 2015 06:25 GMT

In this file photo, a vendor carries his merchandise on a bycicle during a heavy rain in Dar es Salaam in 2008. REUTERS/Radu Sigheti

Image Caption and Rights Information

Aim is to help keep people on their land and stem the rush of jobless migrants to cities

DAR ES SALAAM Sept 2 (Thomson Reuters Foundation) - Katika makutano ya barabara katikati ya jiji la kibiashara la Tanzania, mkulima aliyegeuka kuwa mchuuzi Pascal Kipeta, anatembeza bidhaa mbali za kichina kwenye kitenga cha mbao kwa wateja wake huku akitupia jicho askari wa jiji wanaoweza kupora bidhaa hizo.

“Ni kazi ngumu sana hii. Ni lazima niwe macho muda wote ili kuepuka kugongwa na magari na kuhakikisha kwamba bidhaa zangu haziporwi na askari, kwa kuwa ni kinyume cha sharia kuuza hapa,” aliiambia Thomson Reuters Foundation.

Kipeta Mwenye umri wa miaka 39, alikuja Dar es Salaam mwaka 2011 kuanza maisha mapya baada ya mazao yake kuathiriwa na ukame mkali. Ni miongoni mwa maelfu ya watu wanaotekeleza shughuli za kilimo na kutiririka Dar es salaam—miongoni mwa majiji yanayokuwa kwa kasi sana barani Afrika, hata hivyo, kwa sasa anapata changamoto katika kupata njia mbadala ya kujikimu kimaisha.

Kila siku huamka mapema kwenye chumba alichopanga na kukimbia eneo la Kariakoo akachukue bidhaa kwa wauzaji wa jumla, ili aambulie asilimia 10 ya faida ya anachokiuza.

Serikali, katika harakati za kufufua sekta muhimu kwenye uchumi ya kilimo ambayo inasua sua na kuzuia wimbi la watu wanaokimbilia mijini, imezindua benki ya kilimo kufundisha wakulima mbinu za kisasa za kilimo pamoja na kuwapa mikopo wanayoihitaji.

Benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB) inanuia kuimarisha ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kusaidia wakulima kupata mbegu bora na mbolea, kupata teknolojia na kujifunza mbinu mbalimbali kukabiliana na madhara yanayo sababishwa na tabia nchi.

Kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, ikitoa ajira za moja kwa moja kwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wote na kuchangia asilimia 25 kwenye pato la taifa na asilimia 34 ya mauzo yote ya bidhaa nje, serikali imesema.

Benki kuu ya Tanzania inasema kuwa ni vigumu kwa wakulima kupata mikopo kutoka benki za kibiashara kwa kuwa maofisa wa mikopo wanaamini kilimo si sekta inayouzika hivyo basi, ni vigumu kwa wakulima kupitia biashara zao kupata mapato yanayo weza kulipa mikopo.

Chama cha Mabenki Tanzania kinasema sekta ya kilimo kwa sasa haiingizi pesa nyingi sana kuwezesha wakulima kulipa mikopo, na kwamba hamna mfumo madhubuti wa kutekeleza makubaliano kati ya wakopeshaji na wakulima.

Akiongea katika sherehe ya uzinduzi wa benki hiyo, Rais Jakaya Kikwete alisema serikali itawekeza shilingi Billion 800 ($380million) kwa miaka minane ijayo kutoa mikopo kwa wakulima na kuwasaidia wapate vifaa vya kisasa vya kilimo na kuimarisha uzalishaji na kuboresha maisha yao.

“Tumejizatiti kutatua matatizo mbalimbali yanayorudisha nyuma shughuli za uzalishaji katika kilimo,” Kikwete alisema.

Kuanzishwa kwa benki hiyo kumepokelewa kwa mshangao na Kipeta anayefikiria kuomba mkopo kununua vifaa vya umwagiliaji wa matone ili aanze biashara ya kuzalisha vitunguu.

“Natazamia kurejea kijijini na kuomba mkopo ili niwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji, naamini hilo ndilo litakuwa suluhisho la matatizo yangu” alisema.

Benki mpya ya kilimo, ikiwa ni sehemu ya mpango wa Kilimo Kwanza unaoweka mikakati ya kisera kupambana na mabadiliko ya tabia nchi na changamoto mbalimbali, imenuia kuongeza uzalishaji wa mahindi, miwa, mpunga, mboga za majani, mbegu za mafuta, nyama, maziwa, vitunguu, ufugaji wa kuku pamoja na kuongeza uzalishaji wa biashara ya maua na mbogamboga, uvuvi na ufugaji nyuki, serikali ilisema.

Tanzania ina ekari milioni 44 za ardhi nzuri ya kilimo, hata hivyo ni asilimia 23 tu inatumiwa kwa kilimo kutokana na uwekezaji hafifu katika teknolojia, madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na ukosefu wa wa rasilimali fedha, serikali imesema.

Shirika la Umoja wa Mataifa linasema linakusudia mabadiliko ya tabia nchi yatasababisha ongezeko kubwa sana la wahamiaji na ukosefu wa makazi Africa kusini mwa Sahara kwa miaka ya usoni kutokana na madhara yanayotokana na hali ya hewa.

Tanzania iko mbioni kuathiriwa na madhara ya tabia nchi, ambayo tayari yanaleta hali mbaya ya hewa na mazao hafifu mashambani hasa kwenye maeneo yenye asili ya ukame.

Mji wa Dar es Salaam pia uko hatarini kuathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi—hasa mafuriko na ungezeko kubwa la wahamiaji wanaoingia kukwepa hali mbaya ya maisha vijijini na kuongeza idadi ya maskini mijini, na kuongezeka wa matatizo jijini.

Kuongezeka kwa uwekezaji kwenye sekta ya kilimo kuna weza kubadili taswira ya madhara yaliyopo na kufungua fursa Zaidi kwa wakulima kufanya kazi za uzalishaji kwenye vijiji vyao, wachambuzi wanasema.

“Wakulima wengi wamekata tama. Wanahitaji usaidizi katika kujifunza mbinu za kujikimu kimaisha kwa kujifunza namna ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na haswa kuongeza uzalishaji,” alisema Edith Kija, mtaalamu wa maswala ya ukulima.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->