Huku ukame ukiathiri mahindi, Tanzania yapika viazi vitamu

by Kizito Makoye and Beatrice Rabachi | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 8 September 2015 05:44 GMT

A woman sells orange sweet potatoes in Uganda in 2013. TRF/Alfred Kabuchu

Image Caption and Rights Information
Farmers in Tanzania are switching to growing sweet potato as a strategy to cope with drought and improve food security

KISHAPU, Tanzania, Sept 8 (Thomson Reuters Foundation) - Katika tambarare zinazopulizwa na upepo huko Kishapu, mkoa wa Shinyanga uliopo kaskazini mwa Tanzania, Himelda amekuwa akihangaika kuzalisha mahindi shambani mwake miaka michache iliyopita.

“Nimepata hasara kubwa kutokana na ukame. Mvua za msimu hazitoshi na mazao yananyauka,” alilalamika. Awali mahindi yalistawi kwa urahisi,” alisema, hata hivyo kwa sasa “ni nadra mno kuzalisha chakula cha kutosha kulisha familia yangu.”

Mazao mengine anayozalisha mkulima huyo mwenye umri wa miaka 53, kama vile maharagwe, karanga na magimbi pia hayastawi. Hii ni sababu mojawapo ameamua kulima viazi vitamu vya samawati vinavyostahimili ukame.

Tofauti na mahindi, viazi vitamu vya samawati vinastahimili hali zote na pia ustahimili ugonjwa wa kutu,” alisema.

Tumbo ni miongoni mwa mamia ya wakulilima wilayani humo walioamua kuzalisha viazi vitamu kama mkakati wa kupambana na ukame na kuongeza usalama wa akiba ya chakula. Mikoa ya kanda ya ziwa nchini Tanzania, maelfu ya wakuliama sasa wanazalisha viazi vitamu, huku wakisaidiwa na wataalamu wa kilimo.

Viazi vitamu vya samawati tayari vimetawanyika nchini Uganda, ambapo familia 55,000 kwa sasa wanazalisha zao hilo na nyingine 237,000 zinatarajiwa kuzalisha kufikia 2018, kwa mujibu wa Mpango maalumu wa wizara ya mambo ya nje ya marekani unaojihusisha na maswala ya usalama wa chakula.

Mkoa wa Nyanza, nchini Kenya, pia unazalisha kwa wingi viazi vitamu samawati, baada ya wakulima kupoteza zaidi ya asilimia 80 ya mazao yao ya mahindi kutokana na ugonjwa hatari wa kutu mwaka 2012.

 

MBADALA MGUMU

Watafiti wanasema viazi vitamu samawati ni stahimilivu sana kwenye ukame na mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa ukilinganisha na mazao mengine, na vinaweza kukaa kwenye udongo kwa muda mrefu baada ya kuiva, na kutoa fursa zaidi kwa wakulima kuvuna kwa muda watakaopanga.

Zao hilo lililetwa Tanzania kwa mara ya kwanza mwaka 2002 na Kituo cha Kimataifa cha Viazi kama zao mbadala baada ya ongezeko kubwa la ukame ulioathiri sana zao la mahindi katika maeneo mengi ya nchi.

Zao hilo la viazi ni sehemu ya mkakati wa makusudi wa kupambana na ukame unaoungwa mkono na kituo cha utafiti wa kilimo cha Ukirigulu kilichopo Mwanza, Tanzania, ambacho kinafanya kazi ya kuzalisha na kutawanya marando bora.

Everina Lukonge, mtafiti mwandamizi wa kituo hicho amesema wakulima wadogo eneo hilo wanafunzwa kuzalisha mbegu bora za viazi kutumia na kuuza.

“Wakulima hao wanaopewa mafunzo huzalisha mbegu kwenye mashamba yao wakati wa kiangazi na kuuza wakati wa masika.” Alisema.

Kila rundo la marando, linalotosha kupanda robo ya eka linauzwa kwa shilingi za Kitanzania 5000 ($2.40) au zaidi, alisema Tumbo mkuzaji mmoja.

“Nilipopanda mbegu za marando kwa mara ya kwanza, ziliota vizuri na nikapata viazi vingi sana vilivyosaidia kulisha watoto wangu,” alisema. Kwa sasa, “napata kipato cha kutosha kutokana na mauzo ya marando na maisha yangu ni bora.

VIINI LISHE ZAIDI

Viazi vitamu vya samawati ni muhimu sana kuimarisha lishe na akiba ya chakula, watafiti wanasema, kwa kuwa mazao yake huwa tele, na vina vitamini muhimu zinazokosekana kwenye vyakula vingine asilia na pia ni stahimilivu sana kutokana na ukame. Baadhi ya mbegu huliwa, majani yake kama mboga za majani pia huliwa.

Pamoja na umaarufu wake, wachambuzi wanasema, jitihada za kupanua matumizi ya viazi vitamu samawati Afrika Mashariki zinakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile uhaba wa marando bora, na mfumo duni wa ugavi wa marando yasiyoathiriwa na wadudu na ukosefu wa utashi wa kisiasa.

“Watunga sera kwa ujumla wamedharau umuhimu wa zao hili kwa kuwa linachukuliwa ni zao la mtu masikini ambapo watu huligeukia tu pindi mahindi yanaposhindwa,” alisema Godfrey Pyumpa, mhandisi wa serikali za mitaa aliyepo Morogoro.

Hata hivyo, Maulid Ali, mkulima katika kijiji cha Itima wilayani Kishapu amesema uzalishaji wa viazi vitamu umeleta tofauti kwenye maisha ya familia yake –na ilikuwa rahisi mno kuanza kuzalisha zao hilo.

“Tangu nilipoanza kuzalisha na kula viazi vitamu samawati, afya ya familia yangu imeimarika zaidi, kwa kweli watoto wangu wanapenda zaidi viazi kuliko ugali,” alisema.

(Imeandikwa na Kizito Makoye na Beatrice Rabachi; imehaririwa na Laurie Goering: Tafadhali nukuu Thomson Reuters Foundatio, tawi la hisani la Thomson Reuters, wanaoshughulika na habari za majanga ya kibinadamu, mabadiliko ya tabia nchi, haki za wanawake, biashara haramu ya binadamu na ufisadi. Tembelea www.trust.org/climate)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.