×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Bia ya kijani yaipunguzia kampunin ya bia gharama na mvuke wenye madhara

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 6 October 2015 11:51 GMT

Employees empty rice husks into a boiler to generate power at a Tanzania Breweries plant. PHOTO/Zuberi Mussa.

Image Caption and Rights Information

Company uses rice husks as fuel instead of oil, making beer cheaper and greener to produce

MWANZA, Tanzania (Thomson Reuters Foundation) – Bia ya kijani huenda si kitu la kuvutia kwa wanywaji, hata hivyo, mjini Mwanza, ni kitu cha kufurahisha. Bia ya ‘Kijani’ inayozalishwa hapa sio tu kwa ajili ya kukidhi kiu ya wanywaji, bali pia inapunguza uzalishaji wa hewa ukaa kwenye jiji la miambakama linavyojulikana nchini Tanzania.

Kampuni ya bia Tanzania imeanza kutumia pumba za mpunga kuzalisha nishati safi na endelevu, kupunguza gharama za kununua mafuta.

“Tumepata teknolojia mpya iliyotuwezesha kutumia pumba za mpunga kama mafuta kwa vichemshio vyetu badala ya kutumia mafuta mazito,” alisema Sunday Kidolezi, meneja wa nishati na maji wa TBL Mwanza.

Pumba za mpunga ambazo TBL inazitumia kuzalisha umeme huchukuliwa kama takataka. Mara nyingi wakulima huziacha zikirundikana au kuzichoma au kuzitupa msituni na kuzifanya kuwa chanzo cha uzalishaji wa hewa ukaa inayoangamiza mazingira.

Kwa mujibu wa Kidolezi, zaidi ya asilimia 60 ya umeme wa kampuni hiyo katika kiwanda cha Mwanza hutokana na pumba hizo za mpunga, ambazo TBL inazinunua kutoka kwa wakulima. Mafuta mazito yanachangia takribani asilimia 10 tu ya matumizi ya nishati, huku ziada inatokana na umeme wa gridi ya taifa.

Matokeo yake, TBL imepunguza uzalishaji wa hewa ukaa katika kiwanda chake cha Mwanza  kwa takribani asilimia 50 kutoka tani 8909 mwaka 2012 hadi tani 4,451 mwaka jana, na kuokoa takribani dola za marekani 400,000 kwa mwaka kwenye manunuzi ya mafuta.

Kampuni inapanga kutumia pumba za mpunga katika viwanda vyake vingine Dar es Salaam, Mbeya na Arusha.

Takataka za mashambani kwa kiasi kikubwa zingali chanzo cha umeme mzuri nchini Tanzania inayoweza kupunguza gharama kwa kiwango kikubwa na kusaidia kutatua tatizo la upungufu wa umeme linaloiandama sekta ya uzalishaji nchini, wataalam wanasema.

Tanzania ina vyanzo vingi vya nishati mbadala, ikiwemo upepo, jua, takataka, mabwawa, mvuke, mawimbi ya bahari na kadhalika. Serikali inajaribu kuhimiza matumizi ya teknolojia za nishati mbadala ili kuweka wigo mpana wa vyanzo vya nishati.

“Mabaki ya mashambani ni moja ya vyanzo vya nishati safi mbadala zinazoweza kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi ya mafuta kuzalisha nishati. Hata hivyo, ingali haijatumiwa ipasavyo,” alisema Julius Ningu mkurugenzi wa mazingira wa ofisi ya makamo wa Rais.

Sekta ya bia inachangia sana kwenye uchumi wa Tanzania, ikichangia shilingi za Tanzania billioni 41(191million dola) kwenye mapato ya serikali mwaka 2014-15 pekee, na kuzalisha maelfu ya ajira.

Hata hivyo, athari za mabadiliko ya tabia nchi zimefanya majaaliwa ya sekta hiyo iwe mashakani kwa kuwa ongezeko la joto, ukame na hali mbaya ya hewa vimeathiri uzalishaji wa mahindi, kiungo muhimu kwenye uzalishaji wa bia.

Huku serikali ikikuza maendeleo ya utafiti wa mbegu za mahindi stahimilivu kwa ukame, kampuni nyingi zinajaribu kukinga biashara zao kwa kuwekeza kwenye nishati mbadala na matumizi endelevu ya maji.

Kupitia kusindika na njia nyingine za uhifadhi, Kampuni ya bia Tanzania imepunguza matumizi yake ya maji mjini mwanza kwa asilimia 40, kutoka mita za ujazo 2,000 kwa siku hadi 1,200 kwa kipindi cha miaka mitano.

Kampuni hiyo ya bia ni miongoni mwa makampuni 35 katika ukanda wa ziwa yanayohimiza mpango endelevu wa utunzaji wa mazingira unaojulikana kama “rasilimali-bora na uzalishaji safi,” wenye lengo la kupunguza gharama za nishati na kutunza mazingira ya ziwa Victoria, linalopakana na mji wa mwanza kwa kaskazini.

 MIWA NA MKONGE

Kutokana na ongezeko la gharama za uzalishaji inayokumbana na sekta ya uzalishaji, viwanda vingi  vinaelekea kutumia nishati mbadala kuzalisha umeme.

Kwa mujibu wa shirikisho la wenye viwanda Tanzania, gharama za nishati zinachangia asilimia 20 ya uzalishaji viwandani,hata hivyo kama njia bora zikitumika wazalishaji wanaweza kuokoa hadi asilimia 40 za gharama za nishati.

Wazalishaji wengi wa sukari Tanzania tayari hutumia mabaki ya miwa kuzalisha joto na umeme kwa viwanda vyao, na wakati mwingine kuuza umeme wa ziada kwa kampuni ya ugavi wa umeme Tanesco.

Viwanda vya sukari vya Mtibwa, Kilombero na Kagera hutumia zaidi ya tani 455,000 ya mabaki ya miwa kwa mwaka kuzalisha takribani gitawati 99 kwa saa za umeme, na kugawa zaidi ya asilimia 64 ya mahitaji yake ya uzalishaji wa viwanda

Mabaki ya miwa huchomwa kuzalisha mvuke kwenye vichemshio vyenye shinikizo la juu, na mvuke huo hubadilishwa kuwa umeme unaotumika kuzalisha sukari.

Katani Limited, kampuni ya kutengeneza makonge iliyopo Tanga, pia imeanzisha tuknolojia mpya ya kubadilisha takataka za katani kuwa gesi anuai na kuzalisha umeme kwa matumizi yake yenyewe, pamoja na gesi gandamizi kwa matumizi ya kupikia. Wanasayansi wanasema gesi ya kupikia inayotokana na mkonge ni bora zaidi na ni nafuu kuliko mkaa.

Kabla ya ubunifu huo, kampuni hiyo ilikuwa ikiteketeza takribani asilimia 90 ya mabaki ya mkonge wakati wa mchakato wa uzalishaji.

Imeandikwa na Kizito Makoye; imehaririwa na James Baer na Laurie Goering. Tafadhali tambua chanzo cha habari hii ni Thomson Reuters Foundation, tawi la hisani la Thomson Reuters linaloandika habari kuhusu majanga, haki za wanawake, biashara ya binadamu, rushwa na mabadiliko ya tabia nchi. Tembelea www.trust.org 

 

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->