×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Huku mabwawa ya umeme yakikauka, Tanzania kuzalisha umeme kutumia vyanzo vyenye hewa ukaa

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 29 December 2015 11:06 GMT

Drought has reduced levels of water in Kidatu hydropower dam, in Tanzania's Morogoro region. TRF/Muhidin Issa Michuzi

Image Caption and Rights Information

"Many countries still produce their electricity almost entirely from coal. So why not Tanzania?" asks one official

DAR ES SALAAM December 29 (Thomson Reuters Foundation)—Huku ukame ukiendelea kudhoofisha nguvu ya umeme wa maji, Tanzania imenuia kuzalisha umeme wa kutosha kwa kutumia gesi asilia na mafuta kuziba upungufu.

Mitambo ya umeme wa maji kwa kawaida huzalisha asilimia 35 ya mahitaji yote ya Umeme Tanzania, huku gesi asilia na mafuta hujazia asilimia zinazobaki. Hata hivyo, kwa kuwa mahitaji ya umeme yanaongezeka na maji yanapungua kwenye mitambo ya umeme wa maji, Tanesco - shirika la ugavi wa umeme la taifa- linawekeza zaidi kwenye mitambo ya kuzalisha umeme ya gesi inayotoa hewa ukaa ili kuziba upungufu.

Mwezi Oktoba mwaka huu, nchi hii ya Afrika Mashariki ililazimika kuzima mitambo yake ya umeme wa kutumia maji kwa takribani mwezi mzima kwa kuwa wastani wa maji ya uzalishaji ulikuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kusukuma mitambo, serikali iliesema. Hadi kufikia mwezi December, mitambo ya umeme wa maji ambayo huweza kuzalisha hadi megawati 561, ilizalisha megawati 110 pekee, kwa mujibu wa Tanesco.

“Changamoto kubwa ambayo tunakabiliana nayo ni utegemezi kwenye mitambo ya umeme wa maji kama chanzo kikuu cha umeme, ambacho si endelevu kutokana na kutotabirika kwa hali ya hewa,” alisema Felchesmi Mramba, mkurugenzi mkuu wa Tanesco kwenye mahojiano.

 

UMEME WA JUA, UPEPO HAUJATUMIWA

Huku Tanzania ikiwa na hazina kubwa ya nishati mbadala kwenye vyanzo kama vile umeme wa jua, mvuke na upepo, serikali kwa kiwango kikubwa imeshindwa kutumia rasilimali hiyo kama tiba mbadala kwa umeme wa maji unaosua sua, alisema Agnes Mwakaje, Mtaalam wa mabadiliko ya tabia nchi katika Taasisi ya utathmini wa rasilimali Chuo Kikuu cha Dar es salaam.

Hata hivyo, Sospeter Muhongo, Waziri wa nishati na madini amesema serikali iko makini kuwekeza kwenye umeme mbadala kwa kutumia upepo na jua ili kukidhi mahitaji na kupunguza utegemezi kwenye umeme wa maji. “Uzalishaji wa umeme mbadala utaleta ufanisi na kutoa afueni kwa mabwawa ya maji kujaa maji ili kuendelea na uzalishaji.” Muhongo alisema hivi karibuni kwenye ziara yake kwenye bwawa la Mtera lililopo mkoani Morogoro December 15.

Bwawa la Kidatu na Mtera yaliyopo kwenye mto Ruaha yalilazimika kufungwa kwa muda kwa takribani wiki tatu kwa kuwa usawa wa maji haukukidhi vigezo vya uzalishaji, serikali ilisema. “Kiwango cha maji kwenye mabwawa yetu mengi ya uzalishaji hakitoshelezi kuzalisha umeme. Hata hivyo, hamna tunaloweza kufanya zaidi ila kusubiri mvua inyeshe,” Mramba aliiambia Thomson Reuters Foundation.

Upungufu wa umeme wa maji umesababisha Tanesco kupata hasara inayofikia shilingi milioni 500 kwa mwezi ($230,000, Mramba alisema. Ili kutafuta uvumbuzi wa vyanzo vinavyoaminika vya uzalishaji, Tanesco kwa sasa inajenga mitambo zaidi ya umeme wa gesi, na kuangalia uwezekano wa vyanzo vya umeme mbadala kuongeza kwenye gridi. “Tunategemea kupunguza utegemezi wa umeme wa maji kwa asilimia 15 pindi mitambo yetu ya gesi ikianza kufanya kazi,” Alisema Mramba. Kwa mujibu wa Tanesco, mitambo ya gesi inaweza kuzalisha zaidi ya asilimia 60 ya mahitaji yote ya umeme.

Mwaka jana Serikali ya Tanzania ilizindua mpango wake mkubwa wa uzalishaji umeme ‘roadmap’ unaolenga kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka megawati 1,590 zinazozalishwa sasa hadi kufikia megawati10,800 ndani ya miaka kumi ijayo, hasa kwa kujenga mitambo ya gesi na makaa ya mawe. Wadadisi wa mambo wanasema kuwa na mbadala wa vyanzo vya uzalishaji ni muhimu ili kuepuka upungufu wa mara kwa mara unaosababishwa na ukame.

“Tanesco lazima itumia mchanganyiko wa nishati kulingana na vipaumbele ikijumuisha gesi asilia, makaa ya mawe, umeme wa maji na vyanzo vingine mbadala, kama kweli inataka kufanya uzalishaji kuwa endelevu,” alisema Haji Semboja, mkufunzi wa uchumi chuo kikuu cha Dar es salaam.

“Gesi asilia inaweza kuufanya umeme uje wakati jua halichomozi na upepo unashindwa kuvuma. Na unaweza kuuwasha au kuuzima kwa haraka,” alisema msomi huyo.

Tanzania pia inatarajia kununua umeme wa bei nafuu kutoka kwenye mradi mkubwa wa umeme wa maji wa Ethiopia, Muhongo alisema.

 

CHAFU LAKINI NI NAFUU

Ingawa Tanzania imetegemea sana umeme wa maji kwa miaka mingi, uzalishaji wa umeme nchini kwa sasa unalenga zaidi kutumia gesi asilia tangu ugunduzi wa gesi hiyo kwenye pwani ya Mtwara, kwenye pwani ya kusini mashariki.

Kwa sasa mitambo ya gesi na mafuta inachangia takribani asilimia 63 ya uzalishaji wote nchini, ukilinganishwa na asilimia 36 ya umeme wa maji, serikali imesema. Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo 58 trilioni za gesi asilia, sawa sawa na mapipa billion 1.9 ya mafuta, kwa mujibu wa wizara ya nishati na madini. Nchi hiyo pia ina tani 1.9 bilioni za makaa ya mawe ambayo huenda yakatumika kuzalisha umeme, hata hivyo, kuchoma makaa ya mawe ni kichocheo kikubwa cha mabadiliko ya tabia nchi.

“Yanaharibu sana mazingira lakini ni chanzo rahisi cha nishati, nchi nyingi zingali zinazalisha umeme wake kwa kutumia makaa ya mawe. Hivyo kwa nini tusiwe sisi?’ Alisema Mbise kamishina wa nishati na petroli wizara ya nishati na madini.

Hata hivyo serikali ina mipango ya kutumia umeme wa jua, upepo na mvuke ili kuweka uwiano wa uzalishaji. Mradi wa umeme wa upepo unaogharimu dola za kimarekani million 132 unajengwa, Mbise alisema, na nchi ina tarajia kupata fedha kutoka benki ya maendeleo ya African kuendeleza mradi wa umeme wa mvuke.

Takribani asilimia 36 ya watanzania wana huduma ya umeme, na asilimia 7 miongoni mwao wako vijijini, kwa mujibu wa wizara. Ilisema mahitaji ya umeme yanaongezeka kati ya asilimia 10 na 15 kwa mwaka.

(Imeandikwa na Kizito Makoye; imehaririwa na Laurie Goering; Tafadhali nukuu Thomson Reuters Foundation, tawi la hisani la Thomson Reuters, shirika la habari linalojihusisha na habari za majanga, mabadiliko ya tabia nchi, haki za wanawake, biashara ya binadamu na rushwa. Tembelea www. Trust.org/climate)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->