×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Kampuni za umeme wa jua zapata mikopo kuangaza vijiji vya Tanzania

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Wednesday, 13 July 2016 10:00 GMT

A woman and her child use a solar light to study at night, provided by Greenlight Planet, a client of solar energy financing company SunFunder. CREDIT/Greenlight Planet

Image Caption and Rights Information

Specialist lender links investors with businesses promoting off-grid solar power

DAR ES SALAAM (Thomson Reuters Foundation)—Kampuni ya ARTI Energy ilipoleta taa zinazotumia mwanga wa jua kijijini Kiromo  wilaya ya Bagamoyo miaka minane iliyopita, wenyeji walifurahi ila hawakujua iwapo watamudu kuzinunua.

 “ Nilizipenda sana taa zile, lakini sikudhani wakati huo iwapo ningaliweza kumiliki moja,” alisema Salum Ali mkazi wa Kiromo.

Ikiongozwa na Imani kwamba mwanga ni hitaji la muhimu kwa binadamu, kampuni hiyo  inayosambaza vifaa vya umeme wa jua iliamua kuuza taa hizo kwa mali kauli.

Kampuni hiyo inasema kwamba ilielewa kuwa  wakazi wengi vijijini wasingaliweza kumudu kununua taa hizo moja kwa moja kutokana na ukweli kwamba uwezo wao kifedha  ni mdogo.

Hata hivyo ndani ya miezi michache tu toka huduma hiyo ianzishwe  kwa kutumia mfumo wa  mali kauli, unaoruhusu wateja  kununua bidhaa kwa mkopo na kulipia baadaye, kampuni hiyo iliuza taa nyingi sana  na mfumo wa nishati jua  majumbani kwenye wilaya hiyo masikini.

Ali- ambaye angali anatumia taa ya umeme jua aliyonunua miaka minane iliyopita, anasema ingali ikifanya kazi vizuri.

“ Sina cha kulalamika, naitumia taa hii nyumbani na kwenye shughuli zangu za uvuvi,” alisema mvuvi huyo mwenye umri wa miaka 48.

 Mpango huo ambao sehemu ya mradi wa benki  ya dunia uliojulikana kama Lighting Rural Tanzania, uliotekelezwa kwa pamoja na  shirika la umeme vijijini yaani REA, uliwavutia mawakala wengi na wauza duka  waliopenda kuziuza taa hizo kwa niaba ya  kampuni ya ARTI.

 Mfumo wa mali kauli  unatumika sana vijijini kutokana na uaminifu wa wateja, na wauzaji na ushirikiano kati ya wauzaji na wasambazaji wa bidhaa.

 Ni kwa kupitia mfumo huu Kampuni ya ARTI Energy iliweza  kuleta taa ya umeme wa jua ya bei nafuu na kunufaisha zaidi ya familia  6000 kwenye wilaya hiyo kongwe.

Kwa mujibu wa  Shirika la Takwimu la taifa, ni robo tu ya watanzania wana huduma ya umeme. Huku mahitaji ya umeme yakiongezeka kwa kasi ya kati ya asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, serikali inasema familia nyingi vijijini huwa zinaachwa  katika shughuli mbalimbali za uchumi kutokana na kukosa umeme.

 Na huku umeme wa jua ukileta matumaini ya kuongeza idadi ya watu watakaopata huduma hii muhimu vijijini,  kampuni nyingi zinazojuhusisha na usambazaji wa bidhaa ya umeme jua  zinashindwa kupanuka kutokana na kukosa mtaji.

A technician installs a solar panel on the roof of a house in Uganda for Solar Now, a client of solar energy financing company SunFunder. CREDIT/Solar Now

 UWEKEZAJI BUNIFU

Mabenki mara nyingi  huwa yanasua sua kukopesha  pesa bila ya kujua namna  sekta hiyo  inavyofanya kazi, alisema Lais Lona, afisa mwendelezaji wa biashara wa kampuni ya SunFunder, iliyopo Marekani na Tanzania.

Inajaribi kuziba pengo lililopo kati ya wawekezaji na kampuni zinazojihusisha na nishati ya jua  kwa kuwapa mikopo ya muda mfupi.

 “ Kama si Sunfunder, tungalikuwa bado tukiagiza mzigo kidogo kidogo na kulipia gharama za usafiri na forodha,” Alisema Dennis Tessier, mkurugenzi wa program wa ARTI, iliyopata mkopo pia.

“ Mkopo huo umetuwezesha kupanua biashara yetu, na kuwarudishia bakshishi wateja wetu,” alisema

Sunfunder imetengeneza mbinu ambayo wawekezaji kwenye nishati ya jua wanaweza kutoa mikopo kwa kampuni za nishati ya jua kwa kutumia ujuzi maalum na uzoefu kwenye sekta hiyo, Lona alisema.

“ Tunazitathmini kampuni binafsi za nishati jua  kwa makini, na kupata uelewa  wa muktadha mpana  wa kibiashara,” alisema

Mikopo ya SunFunder inalenga kukidhi mahitaji ya biashara maalum na kupunguza hatari ya kushindwa kulipa.

 Wawekezaji hawakopeshi moja kwa moja bali wanaweka pesa kwenye fungu maalum, ambalo hukopeshwa kwa kampuni kadhaa, na kupanua hatari ya mteja kushindwa kulipa, Lona alisema.

SunFunder ambaye ni miongoni mwa washindi wa tuzo ya ubunifu wa kifedha ya Ashden, inakusudia kusambaza mabilioni ya dola  kwenye uwekezaji wa sekta ya nishati vijijini.

Mpaka sasa imeshatoa mikopo 71 yenye thamani ya $8.6 million kwa zaidi ya kampuni 20  kwenye nchi 10 zinazolipa kwa uhakika wa asilimia 99, Lona  alisema.

 Mikopo hiyo inaweza kuanzia dola  za kimarekani 50,000 hadi millioni moja au zaidi. Kampuni nyingi kwa kawaida huanza kwa kupewa mkopo mdogo kwa miezi michache kununulia bidhaa zake, na baadae huongezewa na kupewa mkopo mkubwa kulingana na rekodi ya ulipaji.

 “ Tunajivunia kuweza kufanya kazi nzuri na wateja wetu, na kuwa wawazi na wepesi kuleta utatuzi wa mambo ya kifedha wanao uhitaji,” Lona alisema.

 Zaidi ya familia 300,000 zimefikiwa  na teknolojia ya umeme jua inayofadhiliwa na SunFunder, kampuni hiyo imesema.

 Familia hizo kwa sasa  zina vyanzo safi vya umeme vinavyowarahisishia shughuli za kila siku, na kupunguza gharama za kununua mafuta ya taa na gharama ya kuchaji simu.

 Kuondoa matumizi ya mafuta taa kunapunguza hatari ya moto na athari kwenye afya ya binadamu kutokana na hewa ukaa . Pamoja na hayo mtaji wa fedha wa  SunFunder hupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na hewa ukaa kwa takribani tani 50,000 kwa mwaka, kampuni imesema.

 Imeandikwa na Kizito  Makoye; uhariri na Megan Rowling. Tafadhali tambua Thomson Reuters Foundation, tawi la hisani na Thomson Reuters, linaloandika habari za majanga, haki za wanawake, biashara haramu ya binadamu  na mabadiliko ya tabia nchi. Tembelea http://news.trust.org)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->