×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Upungufu wa ardhi ya ufugaji wa kuhamahama watoza wanawake wa Kimaasai kwenye ufugaji

by Justus Wanzala | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 26 July 2016 05:00 GMT

Maasai pastoralists Mary Nkaru, Susan Tonui and Charity Kokwai use a hay baling machine at Einabosho in Kajiado East, Kajiado County, Kenya. Thomson Reuters Foundation/Justus Wanzala

Image Caption and Rights Information

ENAIBOSHO, Kenya, Julai 26 (Thomson Reuters Foundation) – Ni alasiri yenye baridi na wanawake watatu wanakusanya nyasi kavu na kuiingiza ndani ya mashine ya kutengeza robota. Muda mfupi baadaye kunaibuka robota la nyasi kavu  ambalo linawekwa kwenye rundiko la marobota mengine ya nyasi kavu ambayo yamefunikwa upande kwa karatasi ya plastik.

Wanawake hao watatu wa Kimaasai - Mary Nkaru, Susan Tonuo na Charity Kokwai – walikuwa na nyasi ya kutosheleza mifugo wao na ya jamii kwa jumla kwenye ardhi yao ya kijamii Kusini mwa Kenya.

Lakini malisho ya kijamii katika Kaunti ya Kajiado County, ambapo wanaishi, inatoweka kwa kasi kutokana na mauzo, mgawanyo wa ardhi na ukuaji wa miji wa haraka ikikumbukwa kwamba mji mkuu wa Kenya, Nairobi, hauko mbali na eneo hilo.

Hali hiyo na ukame unaozidi imelazimisha familia za wafugaji kuyapa kisogo maisha ya ufugaji wa kuhamahama hali ambayo imewapa wanawake nafasi kubwa ya kushiriki shughuli ya ufugaji ambayo tangu jadi imekuwa ikitekelezwa na wanaume.

“Miongo kadhaa iliyopita, utafutaji wa malisho ya mifugo ilikuwa kazi ya wanaume, lakini kwa sasa wanawake pia wanashiriki ufugaji,” asema Kokwai.

Mabadiliko hayo yametokea huku umiliki wa ardhi ukibadilika kutoka mfumo wa kijamii hadi wa watu binafsi, Nkaru alisema.
"Watu waliambiwa kwamba ili kutumia ardhi vyema ni lazima igawanywe katika vipande vinavyomilikiwa kinbnafsi,” anakumbuka. “Hii ilileta hali ya watu kukimbilia hati za umiliki wa ardhi na kuibuka kwa mtindo wa kuweka ua kuzingira  vipande hivyo.”

"Ghafla tulianza kuambiwa kuwa mifugo kuingia katika kipande cha ardhi cha jirani wako ni hatia ambayo inaweza kuchangia utozwe faini. Lilikuwa jambo la kushangaza," alisema.

Lakini kugawa ardhi ya kijamii kumewafaidi mabwenyenye  huku wafugaji wa kuhamahama wakigandamizwa na kuchangia kuongezeka kukosekana kwa usawa, katika jamii, Nkaru alisema.

"Ghafla kuliibuka watu wenye maelfu ya ekari za ardhi huku wengine wakimiliki mia chache au chini ya kiwango hicho," alisema.

Katika jamii ya Wamaasai, ugawaji wa ardhi pia ulimaanisha kuwa ilisajiliwa kwa majina ya wanaume - ambao waligundua kwa haraka kwamba ilikuwa na faida kubwa. Kwa mujibu wa Tonuo, familia nyingi ziliteseka huku wanaume kwa siri wakiuza vipande vya ardhi ya familia.

Huku ardhi ya malisho ya mifugo ikipungua, ufukara  unazidi kuongezeka, alisema. "Hali hii imesababisha kuvunjika kwa familia na kuongezeka kwa ubinafsi, huku watoto wakikumbwa na utapiamlo nao wengine wakiacha shule," Tonuo alisema.

Hay stored under a shed at Einabosho in Kajiado East, Kajiado County, Kenya. Thomson Reuters Foundation/Justus Wanzala

ARDHI NDOGO, NYASI ZAIDI YA KULISHA MIFUGO

Ili kuendeleza maisha yao, wanawake wa jamii hiyo wametafuta njia mbadala za kupata fedha, ambazo baadhi yake zinapinga majukumu ya jadi ya kijinsia.

Wanawake hao watatu wanaotengeza marobota ya nyasi kavu ya kulisha mifugo ni wanachama wa kikundi cha Wafugaji cha Enkusero, ambacho wengi wa wanachama wake ni wanawake. Wakiwa wakazi wa Kajiado Mashariki, wanatafuta njia mpya za kulisha mifugo wao ambao sasa wanakosa ardhi kubwa ya malisho kinyume na ilivyokuwa zamani.

Wanachama wa kikundi hicho wakishirikiana na shirika lisilokuwa la kiserikali la Neighbours Initiative Alliance (NIA), linalosaidia watu wanyonge katika jamii za wafugaji, wameanza kupanda nyasi inayokuwa kwa kasi ambayo hukatwa na kisha kukaushwa na baadaye huhifadhiwa baada ya kutengeneza marobota ili kulisha mifugo, pia wanapanda miti aina ya Caliandra ambayo majani yake ni lishe muhimu ya mifugo.

Lishe hiyo mpya ya mifugo hutumika kulisha wanyama katika vipindi vya ukame, wakati malisho yaliyopo hayatoshi huku ikiwa vigumu kuendeleza uhamiaji wa jadi, na pia kuuzwa kuleta fedha.

Wanachama wa kikundi hicho pia hununua mifugo katika vipindi vya ukame, wakati wafugaji wengi huuza mifugo wao kisha kuwalisha vizuri na kuwauza kwa vichinjio.

Tonuo anasema shirika la NIA kwa ushirikiano na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limewasaidia kujenga ghala la kuhifadhi marobota ya nyasi kavu.

Kundi hilo la zaidi ya wanachama 30 pia limenunua ng'ombe wa maziwa na sasa wanazalisha maziwa ambayo huuzwa kwa kampuni ya Kenya Cooperative Creameries.

"Sisi huendesha ubia wa kibiashara na fedha tunazozalisha zinaweza kukidhi mahitaji yetu na kununua lishe ya ziada ya mifugo wetu," alisema Tonua, ambaye anaongoza kikundi hicho cha wafugaji cha Enkusero.

Licha ya kujiushughulisha na ufugaji ikiwemo ufugaji wa kuku pia, kundi hilo limengeteza dari la kuvuna maji ya mvua ambayo linatumia kuzalisha mboga kwa kunyunyunyuzia maji shamba.

"Tunahisi kupewa uwezo na sisi pia hufundisha watoto wetu kujitegemea," Tonua alisema.

Joyce Saiko, afisa wa mipango ya NIA, alisema jamii ya Wamaasai imekuwa ikisita kuachana na ufugaji wa kuhamahama, licha ya changamoto zinazoongezeka.

Mabadiliko yanayoletwa na kundi hilo la wanawake, hata hivyo, yanaonyesha kwamba baadhi ya masuala ya maisha ya Wamaasai yanaweza kuendelezwa katika nafasi ndogo ya aradhi kwa kutafuta njia mpya za kupata fedha, alisema.

Shughuli hizo ni kama vile ufugaji nyuki na kilimo cha mboga kupitia unyunyuziaji mashamba maji.


Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Tegemeo ya Chuo Kikuu cha Egerton, cha Kenya ambachoo hutafiti sera, ilisema jamii za wafugaji ambazo hutegemea mifumo ya pamoja ya umiliki wa pamoja wa ardhi zitakumbwa na changamoto nyingi mnamo siku za usoni.

Utafiti huo unapendekeza ushirikishaji wa kanuni za kitamaduni katika mfumo wa kitaifa wa kisheria ili kuruhusu mahakama za kitaifa kutekeleza sheria za kitamaduni katika usimamizi wa ardhi ya jamii. Pia unatoa wito wa uimarishaji wa taratibu za kijamii za kusimamia ardhi.

(Taarifa na Justus Wanzala; imehaririwa na Laurie Goering:;. Tafadhali tambua haki miliki ya Wakfu wa Thomson Reuters, Kitengo cha utoaji misaada cha Thomson Reuters, ambacho hushughulikia habari kuhusu maswala ya kibinadamu, mabadiliko ya hali ya hewa, haki za wanawake, ulanguzi wa binadamu na umiliki wa mali. Zuru http://news.trust.org/climate)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->