Haja ya kunyunyuzia mashamba maji inaongezeka lakini, haki ya wanawake kumiliki ardhi, kupatikana kwa kawi safi, mikopo pamoja na mafunzo vinahitajika
Na Justus Wanzala
STOCKHOLM, Septemba 9 (Wakfu wa Thomson Reuters) – Mataifa ya Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara yanashuhudia ongezeko la wakulima wanaomiliki viapande vidogo vya ardhi wanaotaka kunyunyuzia mashamba yao maji kutokana na hali ya anga isiotabirika. Wataalam wa kilimo na maji wanadokeza pia kuwa haja ya kunyunyuzia mashamba maji inatokana na ongezeko la haraka la idadi ya watu kwenye mataifa kama vile Nigeria na Kenya, hali inayochangia haja ya kuzalisha chakula zaidi.
Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti kuhusu sera za Chakula (IFPRI) inakadiria kuwa zaidi ya hekari milioni moja zinazomilikiwa na wakulima wenye vipande vidogo vya ardhi zinanyunyuziwa maji katika kanda hii, kwa mujibu wa takwimu za serikali na picha za Satelite.
Nchini Tanzania, eneo la ardhi lenye mashamba madogo madogo yanayonyunyuziwa maji limeongezeka kutoka hekari 33,500 mnamo mwaka 2010 kufikia takriban hekari 150,000 kwa sasa, kulingana na IFPRI. Hata hivyo, mtafiti wa taasisi hiyo Ruth Meinzen-Dick, anasema hekari milioni 29 kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki zinaweza kunyunyuziwa maji.
Kuimarika kwa unyunyuziaji mashamba maji kunaweza kuchangia usalama wa chakula katika mataifa yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara hasa ikikumbukwa kuwa eneo hilo linazidi kuathirika na mabadiliko ya hali ya hewa. Hali hiyo pia inaweza kuchochea ustawi, Ruth na wenzake waliohudhuria kongamano la Kimataifa kuhusu Maji mjini Stockholm nchini Sweden walisema hayo.
"Unyunyuziaji maji kwenye mashamba madogo madogo ni njia moja ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa," alisema Dawit Mekonnen, Mtafiti wa IFPRI aliyeko nchini Ethiopia.
UPANUZI
Ongezeko la idadi ya wakulima wanaonyunyuzia mashamba maji limetokana sio tu na hali mbaya ya hewa lakini pia limechangiwa na kupatikana kwa pampu za nafuu kutoka China katika mwongo mmoja uliopita. Hayo ni kwa mujibu wa Jennie Barron, Mtafiti wa matumizi ya maji katika Taasisi ya Kimataifa kuhusu usimamizi wa maji (IWMI).
Hata hivyo ili kuongeza zaidi idadi ya wakulima wanaonyunyuzia vipande vya ardhi maji, kutahitaji mabadiliko mengi. Mabadiliko hayo ni kama vile kupunguzwa kwa ushuru unaotozwa pampu zinazoagizwa kutoka nje pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wakulima hasa wanawake kuhusu ujuzi wa kisasa wa kunyunyuzia maji mashamba, watafiti walisema.
Kuhakikisha wanawake ambao ni nusu ya idadi ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo wanamiliki ardhi kisheria ni muhimu katika kuhakikisha wanawekeza fedha zaidi kwenye kilimo kupitia unyunyuziaji mashamba yao maji, walidokeza wataalam hao. "Wanawake hugandamizwa zaidi kwani hawamiliki ardhi au mali," alisema Barron.
Mekonnen alisema unyunyuziaji mashamba maji unazidi kuwa njia muhimu ya kuwasaidia wakulima kwenye mataifa kama vile Ethiopia, Ghana na Tanzania kukuza chakula cha kutosheleza mahitaji ya jamaa wao kwa mwaka mzima na pia kupata fedha kwa kuuza chakula cha ziada wakati bei imeongezeka.
VIKWAZO
Shida moja aliotaja ni kwamba mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara hayajatengeneza ramani ya rasili-mali yake ya maji yalioko chini ya ardhi, hali ambayo inachangia wakulima wenye vipande vidogo vya ardhi kutofahamu yaliko maji.
Uimarishaji wa uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa mabwawa madogo madogo ili kuyakusanya maji ya mvua ardhini unaweza kuwasaidia wakulima hasa kwenye maeneo ambayo hayana maji ya chini ya ardhi, walisema wataalam.
Kutokana kwamba kusambaza maji kunahitaji kawi, kuwasaidia wakulima wenye vipande vidogo vya ardhi kupata kawi safi kama vile kawi ya jua na ile inayotoka kwa upepo pia kutawawezesha kunyunyuzia mashamba yao maji, alisema, Mekonnen.
Kuwepo kwa fedha kutoka hazina za vilabu vya kuchanga fedha za akiba ili kuweza kutolewa kama mikopo ikiwemo taasisi za kifedha za kutoa mikopo ndogo ndogo, pia kutachangia wakulima wenye vipande vidogo vya ardhi kumudu gharama ya vifaa vya kunyunyuzia mashamba yao maji, walisema wataalam.
Hata hivyo, Tim Prewitt, Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika la kimataifa la kutoa Misaada (IDE), alisema utoaji wa ufadhili kwa wakulima wenye mashamba madogo madogo bado ni changamoto na hii ni kwa mujibu wa hali ambazo shirika lake limekumbana nazo.
"Nchini Ghana tulianza kushirikiana na mashirika 12 ya kifedha madogo madogo, lakini kwa sasa tumesalia na mashirika mawili tu," alisema na kueleza kuwa hali hiyo inatokana na wakulima kushindwa kulipa fedha wanazokopa pamoja na gharama ya juu kwa mashirika ya fedha kushughulikia mikopo hiyo.
Kulingana na IWMI, ni asili mia saba pekee ya mashamba kwenye mataifa ya Afrika yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara ambayo yananyunyuziwa maji, kiwango ambacho ni cha chini zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.
(Uandishi ulitekelezwa na Justus Wanzala; Mhairi ni Laurie Goering :; Tafadhali unapochapisha makala haya tambua Wakfu wa Thomson Reuters, Kitengo cha misaada cha kampuni ya Thomson Reuters, kinachochapisha habari kuhusu huduma za kibinadamu, mabadiliko ya hali ya hewa, haki za wanawake, ulanguzi na haki za umiliki wa mali. Tembelea: http://news.trust.org/climate)
Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.