Source: http://www.trust.org/item/20130603103952-mba98/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Mabwawa ya Jumuiya yana lengo la kujenga usalama wa maji nchini Kenya


By Kagondu Njagi | Mon, 3 Jun 2013 11:45 AM



KATUTHIA, Kenya (Thomson Reuters Foundation) - Kabla ya kuwasili katika kijiji cha Katuthia huko Mashariki mwa Kenya, mgeni husafiri kupitia nchi kavu, ambayo ardhi yake yachipua mazao mapya lakini ambayo tayari yaonyesha unyonge baada ya siku tatu bila mvua.

Nao wafugaji wenye upweke wakiandamana na ng'ombe na mbuzi wanazofuga watazama mbinguni, wakitumaini mvua itanyesha tena hivi karibuni na kujaza mabwawa na maji.

Mpaka kutakaponyesha, baadhi yao watasafiri hadi kijiji cha Katuthia na kujiunga na makundi ya wanawake waliokusanyika katika bwawa la Kasomo, wote wakiletwa hapo na kitu kimoja: maji.

Katika bwawa hili, ambalo lamilikiwa na kuimarishwa na jamii hili kukabiliana na hali mbaya ya ukame, binadamu na mifugo hutumia rasilimali hii hadi pale maji yatakapoisha.

Hata hivyo, watumiaji wasema hawana wasiwasi - wakati msimu wa mvua utakapowadia, bwawa litajaa maji tena.

“Mimi sina wasiwasi sana kama hakuna maji kwa sababu wakati huo msimu ujao wa mvua utakuwa karibu,” asema mwanakijiji Rachel Mwangangi. “Mimi nitakuwa nimehifadhi maji ya kutosha nyumbani ambayo familia yangu itaweza kutumia kwa muda mfupi ufuatao wa kiangazi.”

Hali ya hewa nchini Kenya husababisha kiangazi katika sehemu kame za nchi, na kuleta mafuriko katika sehemu hizo mara msimu wa mvua unapoingia, hivi kufurusha maelfu ya watu kutoka manyumbani mwao kila mwaka.

Lakini baadhi ya Wakenya kama kundi la Kasomo kijijini Katuthia, wamegundua kwamba hawafai kuwa na wasiwasi kwa sababu ya hali ya hewa inayozidi kukithiri na kuhusishwa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Badala yake, wanaweza kuwekeza mvua kama maji ya kutumia wakati wa kiangazi. Kile tu wanahitaji ni ardhi inayofaa na usaidizi wa wanakijiji.

NJIA RAHISI YA KUHIFADHI MAJI

Shinikizo la kujenga mabwawa ya udongo ya kuhifadhi maji katika kanda hii ilitokana na juhudi za mashirika mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikundi kinachoshughulikia mabadiliko ya hali ya hewa ama KCCWG, shirika la kikatoliki la Caritas huko Kitui, na wanajiolojia wa serikali.

Wote walikuwa wakitafuta njia ya kuwekeza mafuriko kama maji ya kuhifadhi na kutumia kwa mahitaji ya nyumbani katika sehemu kame za Kenya.

Bwawa lililo kijiji cha Katuthia limekuwa likisaidia jamii kuishi wakati wa ukame kwa miaka miwili sasa.

Undo hili lililo na umbo la bakuli lilichukua siku karibu kumi na tano kujenga na lina ukubwa wa kiasi cha nusu ya uwanja wa kandanda.

Ikitegemea ni kiasi gani ya mvua itakayonyesha, bwawa la Kasomo laweza kushikilia maji ya kutosha na kutumika eneo hilo kwa muhula wa miezi mitatu.

Hii yote imewezeshwa na jiografia ya mashariki ya Kenya.

Kulingana na wanajiolojia, chini ya udongo kuna tabaka la mchanga ambalo lafuatiliwa na mwamba unaotambaa kwa maili nyingi.

Joseph Ndolo, mkuu mwanajiolojia katika Wizara ya Nishati, aelezea kwamba safu ya mchanga inaweza kuhifadhi na kuchuja uchafu kwenye maji, wakati jiwe nalo lazuia maji kutoweka chini ya ardhi.

“Hii ndio sababu kuna mafuriko katika sehemu hizi za Kenya kwa sababu inachukua muda kwa maji ya mvua kufyonzwa,” asema. “Badala yake maji huelekea katika mito ya msimu.”

Jiwe hili limewachanganya wengi waliojaribu kuchimba visima wakitafuta maji. Karibu na bwawa la Kasomo, shimo la mita ishirini lipo bure, huku likiogelewa na nyoka zilizotumbukia ndani na viumbe vingine.

“Tuliendelea kuchimba tukafikia jiwe na wengi wetu wakatoweka,” asema mwanakijiji Mwangangi, ambaye alisaidia kujenga bwawa la Kasomo. “Maafisa wa Caritas walituonyesha jinsi mabwawa ya udongo ni njia rahisi ya kuhifadhi maji.”

Kujenga bwawa, vikundi vya jamii huchangia kipande cha ardhi kilicho njiani mwa mtaro wa mvua, aelezea Florence Ndeti, mshiriki katika mradi katika Caritas Kitui.

Kisha wanakijiji huchota udongo na kufikia safu ya mchanga. Udongo hutumika kujenga kuta za bwawa na kuacha ghuba la kuingiza maji ya mvua.

“Wakati maji ya mvua inapoingia wanakijiji husubiri kwa siku chache ndio matope yaende chini,” asema Ndeti. “Kisha wanaweza kuanza kutumia maji.”

WIZI WA MCHANGA

 

Marafiki wa Kitui, ambalo ni shirika la kijamii, lasema kuna kama mabawa thelathini na tatu katika kanda hii.

Katika nchi ambapo, kulingana na taasisi ya takwimu ya Kenya, zaidi ya nusu ya idadi ya watu husafiri zaidi ya kilomita kumi na tano ili kupata maji, mabwawa ya udongo yafanya upatikanaji wa maji wepesi na rahisi.

Lakini matumaini kwamba mabwawa haya yanaweza kuwa suluhisho la matatizo ya maji mashariki mwa Kenya yana shinikizo kubwa: uvunaji haramu wa mchanga unaouzwa katika sekta ya ujenzi.

Kulingana na Henry Wafula, afisa mtawala mashariki mwa Kenya, mchanga husafirishwa hadi mji mkuu Nairobi kujenga manyumba.

Uchunguzi uliofanywa na ofisi yake waonyesha kwamba mawakala hulipwa mamilioni ya pesa ya Kenya kupeleka mchanga, lakini wao hulipa wanakijiji pesa kidogo kuokota mchanga.

“Wengi wa wanakijiji hawawezi kukataa kwa sababu wanatumia kiasi hiki kidogo cha fedha kununua chakula kwa siku chache,” asema Wafula. “Lakini hawana fahamu jinsi wanavyoharibu na kusababisha athari za mazingira.”

Shirika la taifa la usimamizi wa mazingira ama NEMA linalaumu uvunaji wa mchanga kwa upungufu wa maji katika sehemu kame nchini Kenya.

“Wakati mchanga umeondolewa, maji huenda pia,” asema Boniface Mutinda, ambaye anawakilisha NEMA katika mkoa.

Baadhi ya jamii katika Kasomo huamini mabawa haya ni jitihada kubwa katika kufikia usalama wa maji.

Lakini wengi wao hufikiri mradi mkubwa zaidi ambao waweza kuhifadhi maji mingi inayoweza kutumika katika kilimo ni suluhisho kamili.

Kagondu Njagi ni mwandishi wa mazingira mjini Nairobi.