Source: http://www.trust.org/item/20140616160634-sxybn/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Majengo ya 'kijani' yakita mizizi Kenya


By Justus Bahati Wanzala | Tue, 17 Jun 2014 07:15 AM



NAIROBI, Kenya (Thomson Reuters Foundation) –Hata kwenye joto kali la adhuhuri, maktaba mpya wa Chuo Kikuu cha Katoliki cha  Afrika Mashariki (CUEA) mjini Nairobi husalia baridi – bila  vifaa vya kupunguza au kuongeza viwango vya  joto.

Mawe yaliowekwa chini ya sakafu hunyonya unyevu kutoka ardhini na kuchangia hali ya baridi huku madirisha na milango mikubwa ya jengo hilo ikilindwa dhidi ya joto kupitia vivuli.

Jengo hilo hutumia kiwango cha chini cha nishati na lilishinda tuzo la mwaka huu la Chama cha wenye Viwanda Nchini, kwa kuwa jengo linalozingatia zaidi kanuni za uhifadhi wa mazingira nchini-yaani linaafikia vigezo vya kuwa jengo la ‘kijani.’

Wakati huo huo,  Idara ya Michoro ya Mijengo na Ujenzi  ya Chuo Kikuu cha Nairobi ilipata tuzo kwa kukuza ujenzi wa mijengo ya kijani.

Wanamazingira na mashirika ya wachoraji ramani za nyumba wanajizatiti kukuza  ujenzi wa nyumba za kijani ili kuliweka mbele taifa la Kenya katika ujenzi wa mijengo ya aina hiyo huku wakikariri kuwa  wawekezaji hawajakumbatia wazo hilo kwa wingi. 

"Jengo hili lina hewa safi na  hutumia  mwanga wa kawaida wakati wa mchana. Limejengwa  kwa kuzingatia  mwelekeo wa jua  ili lipate mwangaza wa kutosha hali ambayo inaruhusu  mwangaza wa  asili, na hivyo kupunguza mahitaji ya nishati, "alisema Hiab Gebreselasie, ambaye ni msimamizi wa  maktaba ya CUEA.

Maktaba hiyo hufunguliwa saa mbili asubuhi hadi saa kumi na moja jioni  (8:00-05:00)  na haihitaji kutumia taa. Inapokea hewa safi kutokana na upepo unaoingia ndani huku maji ya mvua yakikusanywa ili kutumika kwenye jengo hilo.  

Majengo ya kijani hujengwa kwa kutumia vifaa vya asili endelevu, na pia hutumia kiwango kidogo cha maji na nishati.

VIWANGO VYA MAJENGO YA KIJANI

Green Africa Foundation, (GAF) ambalo ni shirika lisilokuwa la kiserikali, limebuni kigezo cha kutathmini  iwapo jengo limetimiza vigezo vya kuwa jengo la kijani   kwa kimombo  "Green Mark" na linatoa  mwongozo kuhusu ujenzi wa majengo yanayoafikia viwango bora vya uhufadhi wa mazingira.

Viwango hivyo vipya vinahusisha uendelevu wa maeneo ya ujenzi, uhifadhi wa maji, matumizi bora ya kawi, vifaa vya ujenzi, usafi wa hewa ndani ya jengo,ubunifu na utunzi. Shirika la GAF linalenga kuanza kutoa vyeti kwa majengo yatakayoafikia vigezo hivyo mnamo siku za usoni. 

"Huwezi kuongea kuhusu uhifadhi wa kawi huku ukipuuza majengo, kwa sababu watu wanatumia asilimia 90 ya muda wao kila siku katika majengo, ambayo kuzalisha asilimia 40 ya gesi ya carbon," alisema Nickson Otieno, mchoraji wa ramani za nyumba na mmiliki wa kampuni ya ujenzi .

Shirika la GAF hushirikiana na shirika la kukuza ujenzi wa mijengo inayozingatia uhifadhi wa mazingira nchini Kenya {Kenya Green Buildings Society (KGBS)} ambapo viwango vyake vinafanana na vile vya taifa la Afrika Kusini. KGBS pia husaidia wamiliki wa majengo ya kale kuyakarabati ili kuboresha ufanisi wa matumizi ya nishati na uhifadhi wa maji.

Taifa la Afrika Kusini, Otieno anaelezea, lilikuwa taifa la kwanza la Kusini mwa Jangwa la Sahara kuendeleza viwango vya majengo ya kijani.

Mutua Mweu, ambaye ni mchora ramani wa majengo na mwenye kampuni ya kujenga majengo ya kijani, anasema kuwa kutathmini majengo ya kijani  kunahitaji kuzingatiwa kwa masuala kama vile matumizi ya ardhi, mazingira, viwango vya uzalishaji wa gesi na utunzaji wa maji taka kando na ufanisi wa matumizi ya kawi.

Anakubaliana na Otieno kwamba ari ya umma kukubali ujenzi wa majengo ya kijani inakuwa kwa kasi na kusema kuwa kozi zote za ujenzi na uchoraji wa ramani za majengo katika Vyuo vikuu vya Kenya sasa sharti zihusishe teknolojia ya kijani katika mitaala yao.

"Wakati wa majengo ya kijani umewadia na hakuna mtaalam wa ujenzi anaweza kupuuza," Mweu anasema.

Peterson Karumi, mchoaraji ramani wa majengo mkuu katika Wizara ya Ujenzi  nchini Kenya ambayo ina wajibu wa kuchora na kujenga majengo ya umma, anasema serikali tayari iliandaa rasimu ya sera kuhusu viwango vya majengo ya kijani mnamo mwaka 2013 na huenda ikapitishwa ifikapo mwaka 2015.

Kwa mujibu wa Karumi, sera hiyo itawezesha sekta ya kibinafsi kuwa na jukumu muhimu katika kukuza ujenzi wa majengo ya kijani kwani itatoa vihimizo na miongozo ya wazi. Anaamini Kenya ina uwezo wa kiufundi wa kufanikisha na kukuza ujenzi wa majengo ya kijani.

Mpango wa Umoja wa Kimataifa kuhusu Makaazi (UN-Habitat) umekuwa ukishirikiana na chama cha wachora ramani za majengo nchini Kenya na washikadau wengine tangu 2011 chini ya mpango wa miaka minne wa kukuza ufanisi wa nishati/kawi kwenye majengo katika kanda ya Afrika Mashariki.

AFRIKA KUSINI YAONGOZA

Ruth Maina, mratibu wa miradi ya mpango huo nchini  Kenya, anasema kuwa hakuna takwimu kuhusu idadi ya majengo yanayohitimu kuwa ya kijani nchini, lakini anaamini kwamba kwenye mataifa ya Kusini mwa jangwa la Sahara Kenya  ni ya pili katika suala hili, huku Afrika Kusini ikiongoza nayo Kenya ikichukua nafasi ya kwanza katika kanda ya Afrika Mashariki.

"Kumekuwepo na mabadiliko ya mawazo ya watu, ingawa kwa mwendo wa  kujikokota,  hata hivyo hali ya usoni ni ya kuvutia," anasema.

Majengo ya kijani hutekeleza jukumu pana zaidi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Vincent Kitio, mchoraji ramani wa nyumba anayehudumu kwenye afisi ya Nairobi ya Mpango wa Umoja wa Mataifa kuhusu Makao anasema majengo ya kijani huchangia kuwepo kwa hewa safi ndani yake  na hivyo basi husaidia kupunguza magonjwa ya kupumua.

"Mpango wetu wa ufanisi wa matumizi ya kawi unalenga kushughulikia masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa na kulinda afya ya wakaazi wa majengo," anasema.

Kupitia mpango wake wa Afrika Mashariki, ambao unashughulikia  mataifa ya Kenya, Uganda na Tanzania,  mpango huo wa makaazi unashirikiana na serikali kukuza matumizi bora ya rasilimali kama sehemu ya kanuni za ujenzi wa majengo.  Mpango huo umetoa mafunzo kwa wataalam 300  wa ujenzi wakiwemo wahandisi na pia watungaji sera. Mpango huo unanuia kuyahusisha mataifa ya Kusini,  Kati na Magharibi mwa Afrika.

CHANGAMOTO

Hata hivyo, Kitio anaona changamoto kadhaa kuhusiana na kukuwa kwa ujenzi wa majengo ya kijani nchini Kenya na Afrika Mashariki. Kwanza ni kwamba wawekezaji wakuu katika sekta ya ujenzi hawaoni haja ya kuafikia viwango vya ujenzi wa majengo ya kijani. "Pamoja na kwamba serikali imeonyesha nia, hakuna ushirikiano imara na wadau wengine," anasema.

Kwa mujibu wa Otieno, sekta ya kibinafsi inaonekana kujikokota kuzingatia viwango vya ujenzi wa majengo ya kijani licha ya kwamba inaweza kuokoa rasilimali kwa kufanya hivyo.

Kwa  upande wake Karumi, moja ya sababu inayodhoofisha ujenzi wa majengo ya kijani ni gharama ya vifaa. Vifaa vya kawi ya jua na ujenzi wa majengo ya kijani huwa ghali na kufafanua kuwa ingawa baada ya muda mrefu gharama hiyo nafuu huonekana kuwa ya chini ikilinganishwa na manufaa ya majengo hayo.

Ushuru, anasema Mweu, ni kizuizi kingine. Anasema kuwa serikali inapaswa  kupunguza gharama ya vifaa vya kuzalisha nishati mbadala, ambayo kwa sasa huvutia ushuru wa forodha, ili kukuza uwekezaji katika nishati hiyo.

Hatimaye, Otieno anasema kuna haja ya kutathmini ubora wa vifaa vya ujenzi wa   majengo ya kijani kutoka nchini Kenya. Kwa sasa, baadhi ya vifaa huagizwa kutoka mbali huku vikiwa vimetengezwa kwa njia duni.

"Kama tutaendelea kuagiza vifaa, gharama itazidi kupanda," anasema Otieno, na kuongeza kwamba iwapo vifaa vitatengezwa nchini, basi nafasi za ajira na utaalamu wa ndani vitapatikana.