Source: http://www.trust.org/item/20140221113428-oxrbh/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Chupa rahisi za nishati ya jua zaangaza mtaa wa mabanda nchini Kenya


By Pius Sawa | Fri, 21 Feb 2014 11:34 AM



NAIROBI (Thomson Reuters Foundation) –Ni adhuhuri yenye jua kali, lakini ndani ya chumba kidogo katika mtaa wa Kibera jijini Nairobi, Michael Matare mwenye umri wa miaka 32, ameketi huku chumba kikiwa na mwangaza mkubwa unaotakana na chupa mbili za maji zinazoninginia ndani kwenye paa la nyumba. Katikati ya chupa hizo za plastiki, kuna taa ya umeme yenye wati 100, na ambayo sasa haitumiki.

Matare ambaye hana ajira na wakati mwingi hushinda chumbani, anasema ni miezi nane sasa tangu aache kuiwasha taa ya umeme.

 Anasema taa ya umeme hutoa joto jingi na kukifanya chumba kuwa tatizo kukalika wakati wa mchana. Kabla ya kuanza kutumia chupa hizo za kutoa mwangaza, Matare anasema kulikuwa na giza na hivyo kumlazimu kuwasha mshumaa au koroboi.

"Chupa hizi za miale ya jua ni nzuri mno kwa sababu zinahifadhi nishati nyakati za mchana, na hazihitaji tena kununua mishumaa au mafuta ya taa ili kuleta mwangaza,” alisema Matare.

Matare, mwenye mke na watoto wanne, ni mmojo ya takribani watu milioni moja wanaoishi katika mtaa wa mabanda wa Kibera, chini ya dola moja kwa siku. Awali, alikuwa akilipia shilingi mia nne kila mwezi umeme haramu, na kodi ya kila mwezi ya nyumba ni karibu shilingi elfu tatu, gharama ambayo ni ghali zaidi kwa mtu kama Matare ambaye hutegemea kazi ya kibarua kama vile kuchimba mitaro ya maji akilipwa shilingi mia moja hamsini kwa siku.

Hii inafanya teknologia za nishati ya kijani kama hii, ya kutumia chupa za maji, kuwa muhimu nyumbani mwa Matare. Jitihada ambayo ilianzishwa Kibera mwezi Aprili mwaka 2013, inafadhiliwa na kundi la wanafunzi kutoka Chuo kikuu cha Durham nchini Uingereza, na sasa inaenea kwa kasi katika mitaa ya mabanda nchini Kenya.

CHUPA ZA SODA NA MAJI

Wazo hili liliibuniwa nchini Ufilipino, ambapo chupa za plastiki za soda hutumika tena. Chupa hizo hujazwa maji na kuacha sehemu ndogo ili chupa isijipinde wakati maji yanachemka kutokana na nguvu za jua.

Shimo hutobolewa kwenye mabati juu ya nyumba na chupa kuingizwa, sehemu ndogo ikisalia nje kwenye paa. Jua linapowaka, maji yaliomo kwenye chupa hutoa mwangaza mkubwa kama taa ndani ya nyumba. Kemikali ya kusafisha nguo kama Jik, huongezwa kwenye maji ili yasalie safi kwa muda mrefu kwa ajili ya kutoa mwangaza mweupe.

“Tulifanya utafiti mwanzoni mwa mwaka 2013, na tukagundua kwamba jamii ilihitaji mwanga huu lakini hawakuwa na uwezo wa kifedha,” alisema David Ochieng anayesimamia mradi huu nchini Kenya kupitia shirika lisilo la kiserikali la COVIT (Connecting Voices of Inspiration for a Better Tomorrow).

Shirika hilo lilifanya uzinduzi wa chupa 250, lakini mahitaji yakawa mengi, na kupelekea wanafunzi hao kupitia mtandao wao wa “Enactus” kuchanga pesa na kusambaza chupa 2,500 zaidi.

Gharama ya kutengeneza chupa moja ni karibu shilingi mia mbili za Kenya, na COVIT inafanya iwezavyo kuchanga pesa kutoka kwa wahisani.

 “Kufikia sasa tumeweka chupa 7,200 katika vijiji vine katika mtaa wa Kibera, na lengo letu ni kuweka kati ya chupa elfu hamsini na laki moja,” alisema Ochieng.

SHULE ZANUFAIKA.

Chupa hizi pia zimenufaisha taasisi za kijamii kukiwemo shule za msingi kama vile shule ya msingi ya Anajali na Hope Academy.

“Tuligundua kwamba hii inaokoa pesa na nishati, wakati wa mchana.badala ya kuwasha taa za umeme, tunatumia chupa hizi na madarasa yanakuwa na mwangaza wa kutosha na watoto wetu kusoma vizuri,” alisema mwalimu Valencia Otweche wa shule ya Anajali.

Awali, shule hiyo ilitumia shilingi elfu kumi kila mwezi kulipia umeme, na hivyo kupelekea umeme kukatwa mara kwa mara kwa sababu shule haingeweza kulipia, na wazazi pia hawana uwezo.

Mwalimu Valentine Mongoi wa shule ya Msingi ya Hope Academy, anasema chupa hizi ni baraka kubwa. “Hii imetusaidia kuwa na mwangaza kwenye madarasa. Wakati wa mvua madarasa yalikuwa na giza kikubwa, lakini sasa chupa zinatoa mwangaza na watoto wanaona vizuri wanaposoma,”alisema.

Kila shule iliwekewa karibu chupa 50, mbili au tatu kwa kila darasa kulingana na ukubwa wa darasa. Watoto wanaoishi katika mtaa huu wa mabanda sasa wanasoma hata wikendi.

 “Mwalimu Otweche anasema ni heri mradi huu uwafikie watu wengi kote nchini ili iwanufaishe, wazo ambalo linaungwa mkono na Matare anayesema kuwa chupa hizi zinaweza kuwasaidia watu wanaoishi sehemu za mashambani ambako hamna umeme, kukiwemo shule kwa sababu hutoa mwangaza mkubwa wakati wa mchana.

KUENEA NCHINI KENYA

Jitihada hiyo ambayo sasa inajulikana kama Mradi wa Jua nchini Kenya, umeenea sehemu kadhaa nchini Kenya kukiwemo kaunti za Mombasa, Busia, Kisumu, Migori na Kisii.

“Tunalenga jamii maskini na tunataka kuweka angalabu chupa 400 kwa kila Kaunti,” alisema Ochieng.

Chupa hizo zinaweza wekwa kwenye nyumba yoyote ile ikiwemo nyumba za majani, na chupa moja inatosha kumulika chumba chenye ukubwa wa futi kumi mraba, na inadumu kwa miaka kumi.

Kulingana na wataalamu, inakadiriwa kuwa chupa moja hutoa mwangaza sawa na taa ya umeme yenye wati 55, na inauwezo wa kupunguza gramu 575 za gesi ya carbon kwa siku kupitia ukataji wa matumizi ya umeme.

Jijini Mombasa, chupa 120 ziliwekwa siku ya kwanza, katikati ya mwezi Februari, na kufikia kesho yake, watu 600 walikuwa wamewasilisha ombi la kutaka chupa hizo ziwekwe kwenye paa za nyumba zao.

Ili kufanikisha kazi hiyo, mradi huo unatumia makundi ya vijana, ambapo vijana watatu kutoka kila kundi hupewa mafunzo juu ya kutengeneza na kuweka chupa hizo juu ya nyumba. Vijana hao pia, wanapaswa kuwafundisha wengine na inachukua takriban dakika tano kuweka chupa moja kwenye paa, alisema Ochieng.

Ochieng anasema kuwa jijini Mombasa, wahudumu wa afya wa kijamii pia wamehusishwa kwa sababu ni watu wa umri wa juu na wanaelewa watu wanaohitaji msaada huo. Jukumu lao ni kutaja wanaohitaji, ili vijana waweke chupa hizo.

CHANGAMOTO

Changamoto kubwa zaidi ni ukosefu wa pesa za kufadhili mradi huo, pamoja na dhana kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kutoa huduma za bure. Ochieng anasema kuwa maeneo mengi Mombasa yana maji ya chumvi ambayo si muhimu kutumika katika chupa, na hiyo hupelekea wao kutumia pesa zaidi kununua maji safi.

“Hatuwezi salia tukitegemea wahisani na watu wa kujitolea, alisema Ochieng, iwapo watu watajitolea na kuchangia katika gharama za kazi hii, bila shaka tutasaidia watu wengi katika jamii.”

Ochieng pia amefanya makubaliano na kampuni ya mafuta ya Ujerumani Total, ili kuwauzia taa za kutumia nishati ya jua, ili zitumike wakati wa usiku. Taa hizo zitanunuliwa kwa bei ya jumla ya shilingi 920 kila moja ili ziuzwe kwa shilingi 1,200, na faida ya shilingi 50, itawekwa kwenye hazina ya mradi wa chupa ili watu wengi wapate huduma hiyo.

Tatizo jingine ni kutoelewana kati ya wamiliki wa nyumba na wapangaji. Wamiliki wanahofia kwamba paa za nyumba zitaharibiwa iwapo mabati yatakatwa ili kuweka hizo chupa za mwanga wa jua, na hivyo, wanapaswa kupewa hakikisho kuwa, mradi huo ni safi na utaokoa gharama za maisha za kununua mishumaa na mafuta ya taa, ambavyo vimechangia ajali nyingi za moto katika mitaa ya mabanda.

Lakini Ochieng hakati tamaa. “Nina hakika mradi wetu huu wa chupa za mwangaza wa jua ni mojawapo ya juhudi zinazoweza kuokoa bara letu kutokana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa,” alisema.

“Tunaenda kijani, na natizama Kenya kuwa kijiji cha mradi wa jua, na pahala ambapo hapatakuwa tena na ajali za moto zinazotokana na matumizi ya mishumaa na koroboi,” aliongezea.