Source: http://www.trust.org/item/20140127172943-pi2bu/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Wakazi wa Dar wapambana kukabiliana na gharama za umeme


By Kizito Makoye | Tue, 28 Jan 2014 10:00 AM



DAR ES SALAAM, Tanzania (Thomson Reuters Foundation) — Siku Omar Mganga alivyonunua kuponi ya umeme kadiri unavyotumia kupitia simu yake ya mkono, ujumbe uliotokea kuhakikisha muamala ulimtia kiwewe. Tarehe moja January, shirika la ugavi wa umeme liliongeza gharama zake kwa asilimia 40, ilikuwa na maana kuwa Mganga alipata nishati pungufu kuliko alivyotarajia.

“Huu ni wizi  kweupe! Wanawezaje kupandisha umeme kiwango chote hicho ndani ya muda mfupi? Siwezi kumudu,” Alilalama kinyozi huyo mwenye umri wa miaka 37.

Kutokana na upungufu mkubwa wa mvua kwenye mitambo ya uzalishaji, TANESCO, Shirika la ugavi wa umeme Tanzania, limeongeza viwango vya umeme, swala ambalo wadadisi wa mambo wanahofia  huenda ikachochea ukatajiholela wa misitu kwa kuwa watumiaji wengi wa huduma hiyo huenda wakaongeza matumizi ya kuni na mkaa kwa kupikia.

Uvumbuzi wa gesi asilia nchini Tanzania huenda ukasaidia kuziba pengo la upungufu wa nishati ya umeme na kupunguza matumizi ya mitambo ya kuzalisha nishati inayotumia mafuta. Hatahivyo, upungufu wa nguvu za umeme wa kutumia maji unahatarisha ongezeko la hewa ukaa, wakati huo huo ukifanya maisha yawe magumu sana kwa walaji.

Mganga, ambaye duka lake lipo barabara ya Shekilango katika kitongoji cha Sinza, ni miongoni mwa maelfu ya wateja wa umeme Tanzania wanaobeba mzigo mzito wa gharama ya umeme, unaoathiri takribani sekta zote za uchumi.

Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (EWURA), ilitangaza ongezeko la asilimia 40 ya gharama ya umeme tangu tarehe mosi January 2014, ikiwa na lengo la kulinusuru shirika la ugavi wa umeme linalopata hasara kutokana na gharama kubwa ya uzalishaji.

 “Marekebisho ya gharama zinazopendekezwa zitaliwezesha shirika kumudu gharama za uendeshaji na kuongeza uwezo unaohitajika kukidhi matakwa ya kimfumo,” Alisema Felix Ngalamgosi, Mkurugenzi wa uchumi wa Ewura.

Kwa mujibu wa EWURA, wateja wa kawaida watakuwa wakilipa shilingi 100 kwa uniti, ikiongezeka kutoka shilling 60 walizokuwa wakilipa awali. Hii inamaana kwamba mfanyakazi wa chini wa serikali anayelipwa kima cha chini cha mshahara cha shillingi 150,000 kwa mwezi atalazimika kutenga zaidi ya asilimia 30 ya mshahara wake kwa ajili ya huduma ya nishati.

Kwa mujibu wa EWURA, wateja wa matumizi ya kati, wazalishaji ambao matumizi yao hayazidi uniti 7,500 kwa mwezi sasa wanalipa shilingi 205 kwa uniti, ongezeko la asilimia 55.

Wateja wa TANESCO waliounganishwa kwenye msongo mkubwa wa umeme, pamoja na wale wanaoendesha viwanda na migodi inayotumia uniti 66,000 na Zaidi, watalipa shilling 159 ongezeko kw a asilimia hamsini.

Kukabiliana na ongezeko la gharama ya uendeshaji, Mganga hakuwa na jinsi ila kupandisha bei ya kunyoa kwenye saluni yake. Kwa sasa, anachaji shilling elf tano kunyoa kichwa na ndevu, ongezeko la shilingi 2000. Bei za huduma zingine kama vile kusafisha uso na ngozi pia zimeongezeka.

“Sina maana ya kuwaadhibu wateja wangu, hamna jinsi. Baba mwenye nyumba ameongeza kodi, tusipofanya hivi tutamlipaje,” alihoji Mganga.

Hata hivyo, tayari amepoteza wateja wake wengi, kwa kuwa ongezeko la gharama ya maisha imewaathiri watu wengi. Hata hivyo Mganga angali na matumaini.

 “Ni hali halisi ya maisha inayoumiza sana, pengine wateja wangu watarudi,” alisema.

Wakazi wengi wa Dar wameonyesha hasira zao kutokana na ongezeko holela la bei ya umeme, wakiiomba serikali kuivunja EWURA kwa kuwa imeshindwa kusimamia wajibu wake wa kulinda walaji kutokana na ongezeko holela la huduza za nishati.

“Livunjwe tu, tumechoka,” Alisema Daniel Kabati, Mkazi wa Kawe Dar es Salaam.“ Tunaadhibiwa kwa kutozwa gharama kubwa sana ya umeme kila mwaka.”

Wadadisi wa mambo wanasema ongezeko la gharama ya nishati huenda ikaathiri sekta mbalimbali za uchumi, ikiwa ni pamoja na kuongeza kwa mfumko wa bei.

Kwa mujibu wa shirikisho la wenye viwanda CTI, ongezeko hilo litaathiri biashara ndogondogo za wajasiriamali kwa umeme ni sehemu ya uzalishaji wa bidhaa zao.

“Ni mapema mno kuzungumzia nini hasa kitatokea kwa wazalishaji, hata hivyo, kwa vyovyote, athari itakuwa kubwa kwa kuwa gharama ya uzalishaji itaongezeka sana,” alisema Hussein Kamote, Mkurugenzi wa sera na utafiti.

TANESCO imelazimika kuongeza matumizi ya mitambo ya uzalishaji wa dharura yenye gharama kubwa mno, hatua ambayo imeliweka shirika katika hali mbaya ya kifedha. TANESCO inatumia takribani dola milioni 3.3 kwa siku kununua mafuta ya kuzalisha megawati 365 ya umeme wa dharura, hata hivyo, mapato yake ya siku ni dola milioni 1.4 tu. Serikali inagharimia tofauti inayobaki.

Licha ya rekodi mbovu, serikali inadai kwamba gharama ya matumizi ya umeme Tanzania iko chini ukilinganisha na Kenya na Uganda wanaotoza senti za dola 0.19 na 0.18 (Tanzania0.16.)

“Watanzania wanalipa pungufu kwa kuwa serikali inajazia kwenye pengo la ongezeko la gharama.” Alisema Sospeter Muhongo, waziri wa nishati na madini, kwenye mahojiano na radio One.

Tanzania ilivumbua gesi asilia hivi karibuni, zaidi ya futi za ujazo 43.7 trillioni zenye uwezo wa kutatua kabisa tatizo la umeme, gesi hiyo itakapoanza kuzalishwa.  Kwa mujibu wa wizara ya nishati na madini, uzalishaji huenda ukaanza miaka 10 ijayo.

“Kwa hii gesi tuliyonayo, tunaweza kuzalisha zaidi ya megawati 3,500 za umeme. Matatizo ya umeme yatakuwa historia,” Muhongo alisema kwenye mjadala wa wazi uliofanyika Dar es Salaam.

Wataalam wa mazingira, hata hivyo, wanashaka huenda ongezeko la gharama ya umeme na gesi ya kupikia huenda ikaongeza kiwango cha ukataji holela wa misitu kwa kuwa watu wengi watarudi kwenye matumizi ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia.

“Ongezeko la gharama ya umeme na gesi ya kupikia, utaweka msukumo mkubwa kwenye misitu kwa kuwa watu watatumia makaa na kuni kwa ajili ya nishati, alisema Felician Kilahama, afisa mstaafu mwandamizi na muhifadhi wa wizara ya utalii na maliasili.

Taarifa za vyombo vya habari zinaonyesha kwamba matumizi ya makaa yalipungua sana miaka ya hivi karibuni kwa kuwa wakaazi wengi wa mjini walikuwa wakitumia umeme na gesi. Hata hivyo, wachambuzi wanasema ongezeko la gharama ya nishati huenda ikarejesha matumizi makubwa ya makaa.

“Kama tunadhamira ya kulinda misitu, serikali ni lazima iweke kipaumbele kwenye ulinzi wa bioanuai na uhifadhi, na itakapobidi kutoa ruzuku kuwezesha familia nyingi kutumia nishati mbadala za kupikia” alisema Kilahama.

 Tanzania inatumia tani million moja za makaa kila mwaka, nusu ya hizo zinatumiwa na wakaazi wa Dar es Salaam. Kuni zaidi ya milioni 30 uhitajika kila mwaka kuchomea makaa. Kuni na mkaa huchangia zaidi ya asilimia 90 ya nishati ya kupikia nchini.