DAR ES SALAAM (Thomson Reuters Foundation)—Kampuni ya ARTI Energy ilipoleta taa zinazotumia mwanga wa jua kijijini Kiromo wilaya ya Bagamoyo miaka minane iliyopita, wenyeji walifurahi ila hawakujua iwapo watamudu kuzinunua.
“ Nilizipenda sana taa zile, lakini sikudhani wakati huo iwapo ningaliweza kumiliki moja,” alisema Salum Ali mkazi wa Kiromo.
Ikiongozwa na Imani kwamba mwanga ni hitaji la muhimu kwa binadamu, kampuni hiyo inayosambaza vifaa vya umeme wa jua iliamua kuuza taa hizo kwa mali kauli.
Kampuni hiyo inasema kwamba ilielewa kuwa wakazi wengi vijijini wasingaliweza kumudu kununua taa hizo moja kwa moja kutokana na ukweli kwamba uwezo wao kifedha ni mdogo.
Hata hivyo ndani ya miezi michache tu toka huduma hiyo ianzishwe kwa kutumia mfumo wa mali kauli, unaoruhusu wateja kununua bidhaa kwa mkopo na kulipia baadaye, kampuni hiyo iliuza taa nyingi sana na mfumo wa nishati jua majumbani kwenye wilaya hiyo masikini.
Ali- ambaye angali anatumia taa ya umeme jua aliyonunua miaka minane iliyopita, anasema ingali ikifanya kazi vizuri.
“ Sina cha kulalamika, naitumia taa hii nyumbani na kwenye shughuli zangu za uvuvi,” alisema mvuvi huyo mwenye umri wa miaka 48.
Mpango huo ambao sehemu ya mradi wa benki ya dunia uliojulikana kama Lighting Rural Tanzania, uliotekelezwa kwa pamoja na shirika la umeme vijijini yaani REA, uliwavutia mawakala wengi na wauza duka waliopenda kuziuza taa hizo kwa niaba ya kampuni ya ARTI.
Mfumo wa mali kauli unatumika sana vijijini kutokana na uaminifu wa wateja, na wauzaji na ushirikiano kati ya wauzaji na wasambazaji wa bidhaa.
Ni kwa kupitia mfumo huu Kampuni ya ARTI Energy iliweza kuleta taa ya umeme wa jua ya bei nafuu na kunufaisha zaidi ya familia 6000 kwenye wilaya hiyo kongwe.
Kwa mujibu wa Shirika la Takwimu la taifa, ni robo tu ya watanzania wana huduma ya umeme. Huku mahitaji ya umeme yakiongezeka kwa kasi ya kati ya asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka, serikali inasema familia nyingi vijijini huwa zinaachwa katika shughuli mbalimbali za uchumi kutokana na kukosa umeme.
Na huku umeme wa jua ukileta matumaini ya kuongeza idadi ya watu watakaopata huduma hii muhimu vijijini, kampuni nyingi zinazojuhusisha na usambazaji wa bidhaa ya umeme jua zinashindwa kupanuka kutokana na kukosa mtaji.