Source: http://www.trust.org/item/20140326164355-aswmt/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Wawindaji haramu wa wanyama pori nchini Kenya washirikiana na al Shabaab kwa biashara ya makaa – polisi


By Kagondu Njagi | Thu, 27 Mar 2014 10:00 AM



NAIROBI ( Thomson Reuters Foundation) – Kutokana na ulinzi mkali wa wanyama pori Kenya, majangili wahusika sasa wanashirikiana na kundi aramu, al Shabaab, kwa biashara ya makaa, ambayo pia inaaminiwa kuwa chanzo cha fedha za ugaidi, maafisa wa polisi wa Kenya na wa kimataifa wasema.

“Biashara ya makaa inayodhibitiwa na al Shabaab ndio sasa tisho kubwa la usalama wa mali asili ya nchi,” Henry Wafula, mkuu wa wilaya ya mashariki ya Kenya alisema katika mahojiano na Thompson Reuters Foundation. 

Makaa yenye thamani ya shilingi milioni mia moja na arobaini ya Kenya (ama dola milioni moja elfu mia saba za marekani) husafirishwa nje ya mashariki mwa Kenya kila mwezi, kinyume cha sheria, Wafula alisema.

Biashara hii inahusisha ukataji na uchomaji wa miti mikubwa hasa katika maeneo ifadhi ya wanyama pori. Upotevu wa miti hupunguza maeneo asili ya wanyama pori na kusababisha mmomonyoko wa udongo.

Mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu, ripoti ya Umoja wa Mataifa inayolenga Somalia ilikadiria kuwa mauzo ya makaa kutoka mashariki mwa Afrika na al Shabaab yaweza kuwa juu ya magunia milioni ishirini na nne kwa mwaka.

Hii ni jumla ya thamani ya soko la kimataifa ya dola milioni mia tatu sitini hadi milioni mia tatu themanini na nne.

Sheria zilizopitishwa na Kenya mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu zatoa adhabu kali kwa uvunaji haramu wa misitu, lakini uwezekano wa al Shabaab kuhusika na biashara ya makaa imepelekea shirika la kimataifa la polisi, INTERPOL, kushiriki kuzuia hii baishara, ingawa bado kuna ushahidi duni kuwa fedha inatumika kwa shughuli za ugaidi.

“Tuna ripoti zinazohusisha biashara haramu ya makaa Afrika mashariki kwa shughuli za kigaidi. Lakini serikali hazionekani kukabiliana na tisho hili,” David Higgins, mkuu wa maswala ya uhalifu wa mazingira huko INTERPOL, aliambia waandishi wa habari hivi karibuni mjini Nairobi.

Hakuelezea zaidi, lakini alisema ako na habari, hasa kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, kwamba kuna uhusiano kati ya biashara ya makaa na maswala ya kigaidi katika kanda hili.

INTERPOL ilianza kushughulikia mswala ya biashara haramu ya makaa baada ya Kenya kupitisha sheria inayolinda wanyama pori, na ambayo inatoa adhabu ya kifungo cha maisha kwa yeyote atapatikana na hatia ya magogo, kukata ovyo au kuchoma mimea katika maeneo hifadhi ya wanyama pori.

“Uharibifu wa mazingira kupitia uchomaji wa makaa ni tisho kwa wanyama pori na usalama wa Kenya,” Paul Mbugua, msemaji wa kituo cha wanyama pori, KWS, aliambia Thompson Reuters Foundation.

Maafisa wa kituo cha ulindaji misitu, KFS, wakiri kwamba ukataji wa miti ni tatizo kubwa, lakini tisho hili halizidi majangili wanaolenga tembo na vifaru, swala ambalo limekuwa kilio kikuu kimataifa.

Wanausalama Kenya wasema kwamba shughuli za kupigana na majangili wanaolenga pembe za tembo zinafanikiwa, hivyo basi wawindaji haramu wa pori wanajiunga na al Shabaab kusafirisha makaa, biashara ambayo inahudumia soko la mashariki ya kati.  

‘WAHALIFU HUFANYA KAZI YOYOTE’

“Wahalifu hufanya kazi yoyote,” asema Paula Kahumbu mkuu wa shirika lisilo la kiserikali, ama WildlifeDirect linalolenga kukomesha uwindaji haramu ea ndovu. “Hakuna tofauti kati ya uhalifu wa wanyama pori na ule wa uharibifu wa misitu kwa sababu hatia hizi zote hutendwa kupitia mitandao ya uhalifu.”

Julius Lokinyi, ambaye alikuwa jamwindaji haramu wa pori kwa miaka ishirini na ambaye sasa amerekebisha tabia, alisema kuwa ilikuwa rahisi kuwinda wanyama pori huko Samburu na Turkana kwa miaka mingi bila kushikwa.

“Watu ambao hushiriki kwa uhalifu wa porini wamejipanga vizuri kupitia mitandao inayoanza vijijini na kuungana na matajiri na watu wakubwa serikalini,” alisema Lokinyi, ambaye sasa ni mwanabiashara wa mifugo mjini Isiolo, huko kaskazini mwa Kenya.

Maafisa wa serikali walikanusha madai yake.

Majangili wana njia za kujibadili ili kutoroka wanasheria, alisema katika mahojiano. “Mimi nilikuwa nabadilisha rangi ya mwili wangu kwa kutumia ngeu (ardhi iliyo na rangi nyingi) kukaa kama jangwa,” alisema. “ Nikiwa mgonjwa ningetumia dawa za kienyeji kujitibu ili nisiende hospitali.”

Lokinyi, ambaye alisema ametoroka maafisa wa usalama mara mingi, asema kuna mitandao ya jinai ya kutorokea nchini Tanzania, Somalia, Ethiopia na kusini mwa Sudan.

“Mimi ningeweza kuishi jangwani zaidi ya siku arobaini bila chakula na maji,” alisema. “Wakati walinda usalama walikuwa karibu kutushika, sisi tuligeukia shughuli zingine kama biashara ya makaa.”

Wanahifadhi wasema uchomaji makaa umeongezeka kwa sababu al Shabaab wanalipa fedha nzuri, na kwamba uwindaji wa wanyama pori umeongezeka kwa sababu ya vijana kukosa ajira na kupungukiwa kwa vyombo vya usalama kama vile askari wa jamii.

Shirika la kutetea wanyama pori, KUAPO, lasema wanausalama wanakabiliwa na shinkizo za kufanya kazi muda mrefu huku wakilipwa mishahara duni.

“Wao hawalipwi vizuri, hawana vyombo vya kazi, wanakaa chini ya miti, huku wengi wakiishi kwa lishe la mchele na maharagwe,” alisema Raabia Hawa wa KUAPO. “Kwa upande mwingine, al Shabaab inajulikana kulipa vizuri, na inauwezo wa kuwavutia wahalifu wawafanyie kazi.”

Kagondu Njagi ni mwandishi wa mazingira mjini Nairobi.