Source: http://www.trust.org/item/20140223235009-zcqin/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Ukadiriaji wa viwango vya gesi chafuzi shambani huenda ukawa na manufaa, wanasayansi wasema


By Geoffrey Kamadi | Mon, 24 Feb 2014 10:45 AM



BONDE LA NYANDO, Kenya (Thomson Reuters Foundation) - Utafiti utakaokadiria kiwango cha gesi chafuzi kutoka mashamba ya wakulima wadogo-ambao ni nguzo muhimu ya ukulima Africa - umeng’oa nanga. Inatarajiwa utafiti huu utawawezesha wanasayansi kubuni mbinu mwafaka za kutekeleza ukulima kwa njia rahisi na kupelekea kupunguza uzalishaji wa gesi hizi.

Mradi huu unatarajiwa kuziba pengo kubwa la ukosefu wa maarifa maalum kuhusu viwango vya gesi chafuzi, haswa kutoka kwa mashamba ya wakulima wadogo, hivyo kuwezesha wanasayansi kupendekeza mbinu zinazostahili na endelevu za utunzaji shamba. Hivyo basi, kuzidisha mapato ya wakulima.

Utafiti huu unatekelezwa katika Bonde la Nyando, magharibi mwa Kenya, eneo  linalotambulika kwa ukuzaji wa aina mbali  mbali ya mimea, uwepo mpana wa tofauti za mwinuko wa ardhi, mbali na kuwa na idadi kubwa ya watu - kwa kweli Bonde hili ni mojawapo ya maeneo yenye idadi kubwa ya watu nchini ambako wakulima wadogo huendesha kilimo kwa kina.

Mradi huu unahusisha muungano wa mashirika kadhaa za kitafiti zinazojumuuisha mashirika husika za utafiti wa kilimo ulimimwenguni (CGIAR) pamoja na Chuo Kikuu cha Maseno. Unafahamika kama kiwango cha kutathmini riziki na uwezekano wa kukabiliana na mifumo ya wakulima w adogo.

Bonde la Nyando hukumbwa na uhaba wa chakula kando na kuwa na rotba finyu pamoja na kukabiliwa na changamoto la mafuriko na ukame wa mara kwa mara. Bonde hili linahusisha maeneo tambarare ya Kisumu na nyanda za juu za Kericho, ambako ukuzaji wa chai huendeshwa.

Sababu hizi, mbali na mifumo aina tofauti za ukuzaji, yaifanya eneo hili kuwa mwafaka kwa utafiti. Haya ni kwa mujibu wa Mariana Rufino, mwansayansi mkuu katika kituo cha utafiti cha misitu ulimwenguni (CIFOR), ambalo ni shirika husika la CGIAR.

Wakulima wa Nyando hukuza mahindi, maharagwe, muwa na ndizi mbali na majani chai, nyasi aina ya napier ambayo ni lisho la mifugo. Mahindi na maharagwe ni mazao yanayohitaji shamba kutayarishwa kila mwaka, ilhali nyasi ya napier yahitaji shamba kulimwa kwa muda usiopungua miaka miwili. Kwa upande mwingine muwa hukuzwa kwa mzunguko wa kati ya miaka mitano na saba.

Ukuzaji wa aina hizi ya mazao yahitaji wakati tofauti ya utayarishaji wa ardhi na upanzi, hivyo kupelekea uzalishaji wa gesi kwa wakati tofauti tofauti, kuambatana na aina ya mazao shambani.

“Ingawaje eneo la utafiti ni mdogo, usiozidi kilomita kumi mraba, kwa upande mwingine twaweza pata ufahamu wa tathmini kamili la eneo lote,” kasema Rufino.

Ili kufahamu kuhusu gesi zinazotokana na upanzi wa aina fulani wa mmea, wakulima huulizwa maswali zinazoambatana na utumizi wa mbolea, kiasi cha mbolea kinachotumika, wakati wa upanzi na mara ngapi wao huondoa kwekwe shambani.

“Sababu hizi zote huathiri uzalishaji wa gesi kwa maana usumbufu wa mifumo ya mchanga huenda ukazidisha au ukapunguza uzalishaji wa gesi. Hivyo, twaweza tafuta njia za kupunguza gesi hizi,” aeleza Bernadette Nangira, mwanafunzi wa somo la mazingira za kikemikali katika Chuo Kikuu cha Maseno.

Emanuel Mambo Oduory, anayesomea somo sawia katika chuo hicho, aongeza kusema kuwa sampuli za gesi zinazotolewa katika eneo la utafiti hupelekwa kwa maabara ya chuo kwa uchambuzi.

Ufahamu wa aina ya mimea inayokuzwa, mwinuko wa ardhi na kiwango cha mvua katika Bonde la Nyando, huwawezesha wanasayansi kuchunguza aina tofauti ya mbinu za kukabiliana na mabadiliko za kitabianchi, mbali na njia mwafaka za usimamizi wa ardhi kama vile unyunyizi kwa matone na upanzi wa mazao na miti kwa pamoja, utumizi wa nyumba kitalu na uanzishi wa upanzi wa mazao yanayoweza kustahimili ukame, Rufino kasema.

Lengo kuu ni kutafuta mchanganyiko wa mimea inayoweza kupunguza uzalishaji wa gesi mbali na kulinda maisha na mapato pamoja na kutafiti jinsi wakulima wanavyosimamia ardhi, “kwa sababu wao ndio watakaoamua jinsi ya kusimamia ardhi,” asema Rufino.

John Obuom, baba ya watoto wanane kutoka kijiji cha Kowala, upande wa chini wa Bonde la Nyando, Kaunti ya Kisumu, ni mmoja wa wakulima ambaye amezidisha pato lake baada ya kufaidika na mafunzo ya kukabiliana na mabadiliko ya kitabianchi.

Sasa anafuga aina ya kondoo Nyekundu wa Kimaasai na mbuzi, wanaokuwa kwa upesi, kando na kupanda miti mbolea shambani pamoja na mimea mingine, ambayo imepunguza momonyoko wa udongo, haswa nyakati za mafuriko mbali na kuongeza rotba shambani.

Mbuzi wake wa maziwa, kasema Obuom, huzalisha hadi mara tatu zaidi ya maziwa ikilinganishwa na mbuzi asilia, hivyo kumuwezesha kuuza lita nne kwa siku na kunufaika na lita mbili ya matumizi ya kinyumbani.

Kondoo Nyekundu wa Kimaasai huuzwa kwa shilingi 15,000 (dola 176), ambayo ni bei zaidi ya mara tatu ukilinganisha na aina asili ya kondoo.

Mafunzo yaliyomnufanisha Obuom, ni moja ya mradi wa vijiji maalum ya kukabiliana na changamoto ya kitabianchi, yalioanzishwa Africa magharibi na mashariki pamoja na sehemu kadhaa bara Asia, chini ya mpango wa CGIAR wa madiliko ya kitabianchi, ukulima na chakula toshelezi (CCAFS) inayonuia kupima aina tofauti ya mazao, teknologia na mbinu za kilimo ili kuchanganua mbinu mwafaka zinazofaa.