Source: http://www.trust.org/item/20140417110316-z13bv/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Mfumo mgumu wazua tuhuma za uporaji ardhi Tanzania


By Kizito Makoye | Thu, 17 Apr 2014 11:03 AM



DAR ES SALAAM, Tanzania (Thomson Reuters Foundation) -Ari ya dunia ya kuanzisha mazao ya nishati imezua wimbi jipya la uporaji ardhi baada ya makampuni ya kigeni kunyemelea ardhi za kijiji zinazodaiwa kuwa ni za wakaazi wa maeneo hayo.

Makundi ya wanamaendeleo wamewashutumu wawekezaji wanaopewa jeuri na serikali kuwa wanapora ardhi ya kijiji kuanzisha miradi ya nishati Mkoa wa Pwani.

“Kusema waziwazi, ardhi kubwa sana serikali inayotaka kuwekeza itaporwa kutoka kwa wananchi na kupewa wawekezaji.” Alisema Douglas Hertzler, Mchambuzi mwandamizi wa sera, shilika la Action Aid, wakati akitoa mada kwenye mkutano wa mwaka wa ardhi na umaskini, Washington DC mwezi Machi Mwaka huu.

Migogoro ya ardhi nchini Tanzania inaashiria kwamba nchi haina ardhi ya kutosha iliyopo mikononi mwa serikali kwa ajili ya uwekezaji mkubwa wa kilimo, Hertzler aliongeza.

“Ukiangalia msukumo uliopo kushawishi vijiji kuacha ardhi yao iporwe na wawekezaji, kuna hatari kuu kuwa baadhi ya wakulima watanyang’anywa ardhi yao bila ya fidia.” Mchambuzi huyo wa Action Aid alisisitiza.

Watetezi wa mazao ya nishati wanahimiza kwamba nishati ya mazao itasaidia nchi kupambana na mabadiliko ya tabia nchi wakati huo huo kutatua tatizo la upungufu wa nishati huku ikiongeza kipato cha wananchi. Hata hivyo, wapinzani wanasema biofuel haina lolote zaidi ya kunyakua tonge kwenye midomo ya watu wenye njaa na kuziacha jamii zikiwa taabani.

“ Upanuzi wa miradi hii itaharibu misitu na uoto wa asili, pia itachukuwa ardhi ya kilimo inayomilikiwa na wenyeji, na kuzua migogoro ya ardhi na wenyeji kuhusu nani mwenye haki ya kumiliki.” Alisema Mariann Bassey, mwanaharakati kutoka kundi la Friends of the Earth wa Nigeria.

Sheria za ardhi za Tanzania zinasema wageni ni lazima wapate ardhi kupitia kituo cha uwekezaji (TIC). Hata hivyo, baadhi ya makampuni yameonekana kukwepa mlolongo rasmi na kughiribu wananchi vijijini, kwa mujibu wa mtafiti Atakilte Beyene, wa Stockholm Environmental Institute aliyeshiriki kwenye utafiti kuhusu biofuel Tanzania uliochapishwa mwaka uliopita.

Wilayani Rufiji na Bagamoyo, kampuni kadhaa za kigeni ikiwemo Eco Energy zimeingia kwenye mzozo wa ardhi na wakulima.

Wakulima wanalalamika kwamba viongozi wa kijiji wamewaamuru kuondoka kwenye mashamba yao ili kukaribisha uwekezaji bila hata ya kupata fidia yoyote. Wakulima wengi wanasema watu wengi wameacha mashamba yao ili kuruhusu uwekezaji na kupewa ardhi ndogo tena isiyo na rotuba.

Jumanne Kikumbi kutoka Nyamisati aliwashutumu viongozi wa wilaya kwa ubabe. “Wametuweka kwenye hali mbaya sana—hawa wawekezaji wamefikia hatua ya kufanya maamuzi juu ya matumizi ya ardhi yetu bila hata ya kuwasiliana nasi.”

“Nilikuwa na eka tatu za ardhi nilizokuwa nalima matunda, pia niliweza kupata ardhi zaidi nilipozalisha vyakual, hata hivyo, tangu makampuni haya yamekuja, sijaweza kulima tena, Riziki Mtongoni, mkaazi wa Kijiji cha Nyamwengwe aliiambia Thomson Reuters Foundation

Kwa mujibu wa sheria ya ardhi ya kijiji ya 1999, mabaraza ya kijiji yananguvu kuamua namna ardhi itakavyotumiwa. Sehemu ya ardhi inapotambuliwa na wawekezaji, serikali ya kijiji inalazimika kuomba kibali cha wananchi husika kuafikia kwamba ardhi hiyo iingizwe iwe ardhi ya umma na kukodishwa.

Wakulima wilayani Rufiji na Bagamoyo wanawatuhumu viongozi wa wilaya kwa kushirikiana na wawekezaji kupindua maamuzi ya mabaraza ya kijiji na kupora ardhi yao pasipo fidia.

Kampuni ya Africa Green Oil Company, kwa mfano ilienda kijiji cha Nyamatanga mwaka 2007 baada ya kuwasiliana na viongozi wa wilaya, iliomba ipewe eka 1500 za ardhi. Baadhi ya wanakijiji wamesema hiyo ilikuwa ni amri kutoka kwa viongozi wa wilaya.

Baada ya mkutano wa kijiji, kampuni iliruhusiwa kuchukua ardhi hiyo kwa makubaliano kwamba itajenga zahanati, shule na mfumo wa maji safi. Wanakijiji hao walivyolalamika kwa TIC Dar es salaam kwamba mwekezaji hajatekeleza ahadi yake, waliambiwa serikali haikuwa na habari juu ya uwekezaji uliokuwa unafanyika kijijini hapo. Walisema mwekezaji huyo aliamua kuachilia mbali mradi huo na wao kuweza kumiliki tena ardhi hiyo yao.

Afisa mkuu wa ardhi Rufiji Leo Rwegasira alikanusha tuhuma za uporaji ardhi. “Tatizo lililopo ni kwamba sera ya ardhi imeweka mfumo wa fidia wa mara moja bila ya kuzingatia ardhi huongezeka thamani kadiri muda unavyoongezeka,” alisema.

Wadadisi wanasema njia inayotumiwa na wawekezaji inawaondolea hadhi na kuaminika kwao licha ya kuzua mizozo isiyo na lazima baina yao na wakulima wanaohitaji ardhi kwa kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Kwenye hali ambayo matumizi ya ardhi hayafahamiki, na ambapo mwekezaji anagharimia matumizi ya ardhi, wakulima wanaweka ardhi yao rehani na huenda wasipate fidia stahili,” alisema Godfrey Massay, mtafiti anayefanya kazi na shirika la Haki Ardhi.

Massay aliiambia Thomson Reuters Foundation kwamba serikali isipoziba mapengo kwenye sera ya ardhi, tatizo litakuwa kubwa mno. “Sina shaka kutakuwa na unyakuaji wa ardhi kama serikali itaendelea kukumbatia wawekezaji wanaokiuka haki za msingi za binadamu.”

Mkurugenzi Mkuu wa Eco Energy Anders Bergfors, alikataa kuzungumzia tuhuma za uporaji ardhi, alimwelekeza mwandishi huyu kupitia maswali yanayo ulizwa mara kwa mara kwenye tovuti ya kampuni hiyo inayo sema kampuni hiyo imepata ardhi kwa uwekezaji wa miwa kwa uwazi, ambapo wananchi na serikali watamiliki asilimia 25 ya hisa kwenye mradi huo.

Nchini Tanzania ardhi yote ni mali ya Taifa, iliyokabidhiwa kwa Rais kwa niaba ya wananchi. Nchi ina asilimia 70 ya ardhi ya kijiji, asilimia 28 hifadhi za taifa na asilimia 2 ardhi ya umma. Watu wanaweza kumiliki ardhi kutokana na haki zinazotolea na nchi.

Kwa mujibu wa utaratibu wa uwekezaji za TIC, mwekezaji ni lazima aonyeshe mpango wake wa biashara. Kama utathibitishwa, watafanya maombi ya ardhi ambapo TIC inaweza kuwapa kutoka katika benki yake. Baada ya hapo, mwekezaji anapelekwa kwenye kijiji husika kupitia kwa afisa ardhi wa kijiji, ambapo atatoa pendekezo lake kwa baraza la kijiji, kama litakubaliwa hatua ya upimaji itafanyika na kuithaminisha ardhi tayari kwa kutoa fidia na kuichukua rasmi.

Wadadisi wa mambo wanasema tatizo ni kwamba ardhi ya kijiji inaporidhiwa kukodishwa kwa mwekezaji, wakulima hawana tena milki ya ardhi ile mpaka baada ya miaka 99.

Utafiti wa mwaka 2013, Biofuel Production and its Impacts on Local Livelihoods in Tanzania, uliochapishwa na taasisi ya mazingira ya Sweden unaonyesha kwamba mkanganyiko wa sera ya ardhi Tanzania umeleta vurumai inayoeza kutoa fursa kwa wawekezaji kupora ardhi.

Wakati makampuni yangali yanajua mipango ya kisheria, wakulima hawajui lolote kwamba ardhi inapopelekwa kwenye milki ya TIC huenda isirudi tena mikononi mwao kwa kipindi kirefu.

Kwenye mahojiano na Thomson Reuters Foundation, Adam Nyaruhuma, afisa mwandamizi wa Wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, alikanusha tuhuma za uporaji ardhi kama ni uvumi unaokuzwa na wanaharati.

Nyaruhuma alisema sera ya serikali kuhusu upatikanaji wa ardhi kwa uwekezaji ni wazi na inafuata taratibu.

“Hamna kitu kinachoitwa uporaji ardhi nchini mwetu, kila kipande cha ardhi kinachokodishwa kwa wawekezaji kinapatikana kwa kufuata utaratibu. Hamna namna yoyote ile serikali imetoa upendeleo kwa wawekezaji ili kukandamiza wananchi,” alisema.

Ardhi inaweza kumilikiwa Tanzania kupitia cheti cha umiliki au haki ya kimila kama ni ardhi ya kijiji. Wageni hawawezi kupewa haki ya kumiliki ardhi Tanzania, isipokuwa kwa ajili ya uwekezaji tu, ambapo TIC inatoa haki pendelevu (derivative rights) kwa mwekezaji,” Nyaruhuma Alisema.

“Ili kulinda wakulima an ardhi yao ya kijiji, hatua zozote za kubadilisha matumizi ya ardhi ni lazima iwashirikishe wao kupitia baraza la kijiji. Pia inahitaji idhini ya Kamishna wa ardhi, waziri na Rais,” Nyaruhuma alisema.

Kizito Makoye ni mwandishi aliyepo Dar es Salaam. Anaripoti kuhusu utawala bora, rushwa na mabadiliko ya tabia nchi.