Source: http://www.trust.org/item/20140609105034-hw17n/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Mashule yaongoza kwa ongezeko la nishati mbadala vijijini Kenya


By Kagondu Njagi | Mon, 9 Jun 2014 12:00 PM



SAMBURU, Kenya (Thomson Reuters Foundation) - Kengele ya jioniinapolia, inawashiria kuisha kwa mafunzo katika shule ya Donyo Wasin. Hata hivyo, kwa wachache walio stadi kama Sotik Leleno, hii inabisha wakati wa masomo ya binafsi chini ya mwanga ulionaswa kutoka kwa jua.

Leleno ni miongoni ya idadi inayoongezeka ya vijana ambao wananufaika na mpango wa serikali wa kuwekeza nishati mbadala katika vijijini Kenya kupitia shule za msingi.

Huko Donyo Wasin, wanakijiji hupumzika chini ya vivuli vya miti kutokana na jua kali, mapema kama saa tatu ya asubuhi. Idara inayotabiri hali ya anga Kenya (KMD), yakadiria kuwa joto yaweza kuwa juu kama nyuzi thelathini na tano katika eneo hilo.

Lakini huko shule ya Leleno, jua ni baraka. Tume ya serikali inayodhibiti nishati (ERC), ikishirikiana na wadau imeweka umeme wa jua kwenye paa za shule.

Umeme huu unamwezesha Leleno kusoma hadi masaa ya mwisho jioni.

“Baada ya shule nilikuwa najiunga na wenzangu kwenda kutunza mifugo,” akumbuka kijana huyu wa umri wa miaka kumi na mbili. “Mimi sasa huendelea kusoma masaa ya jioni huku shuleni. Hii haingewezekana nyumbani.”

Kama maeneo mengine vijijini Kenya, Donyo Wasin iliyo katika kanda ya bonde la ufa, bado haina nguvu za umeme. Barabara mbovu na umbali kutoka mji mkuu – ambapo maamuzi kuhusu nishati hufanywa – huzuia starehe kama hizi kufika hapa.   

Taasisi ya Takwimu ya Kenya (KBS), yakadiria kwamba asilimia ishirini na nane tu ya Wakenya ndio wako na nguvu ya umeme. Na hawa wenye bahati huishi maeneo ya mijini ambapo kunapatikana rahisi miundomsingi, maafisa wasema.

Hata hivyo, serikali ikishirikiana na jamii imepitisha sera ambayo lengo lake ni kutoa asilimia sitini ya mahitaji ya jamii ya nishati kutoka kwa vyanzo mbadala kupitia shule za msingi - na ambazo huleta pamoja jamii - kama vituo vya kuwekeza nishati mbadala. Ya Leleno ni moja ya kama shule hizi.

Leleno asema kwamba upweke humjia wakati mwingine wakati anaposoma mbali na familia yake. Lakini hisia hizi zaweza kuwa za muda kama vituo hivi vya vianzo vitaweza kuhikimu nia yake ya kugawa nishati na jamii jirani na shule, hivi kuanzisha “vijiji vya hali ya hewa safi”.

“Lengo la vijiji hivi ni kuwekeza nishati ya jua, upepo na biogasi ili kutumika sio tu kwa masomo, lakini pia vihudumie jamii,” alieleza Peter Odhengo, afisa katika ofisi ya hazina rasmi.

Kwa mujibu wa Odhengo, megawati moja ya nishati ya jua yaweza kuwa na nguvu ya kuhudumia takriban vijiji mia moja hamsini kulingana na kiwango cha matumizi. Lakini pia gharama ni kubwa, megawati moja ikigharimu kama dola milioni mbili, asema.

Fedha za kimataifa zasaidia katika kulipia gharama hii. “Uwekezaji huu unatolewa kwa ajili ya mikataba ya kimataifa,” alisema. “Sisi tunashirikiana na nchi zilizoendelea kuwekeza mradi huu kwa sababu unasaidia kutatua shida ya mabadiliko ya hali ya hewa duiniani.”

Kituo cha mafunzo ya sera Afrika (ATPS), chasema Kenya ipo mpangoni wa ajenda ya maendeleo ambayo inatumia kiasi cha kaboni cha chini, ikiwa lengo lake ni kukidhi mahitaji ya nishati bila kuweka shinikizo kwa mazingira, ili vizazi vijavyo pia vifaidike.

KUPELEKANA NA UCHINA

Kulingana na maafisa wa serikali, Kenya ni moja ya nchi ambayo inakithiri kwa teknolojia mbadala, huku matumizi yake nyumbani yakiwa juu zaidi duniani, huku tu ikija nyuma ya Uchina kwa mahitaji. 

Nicholas Ozor, afisa anayefanya kazi na ATPS, asema hii imewezekana kwa sababu ya sera ya serikali ambayo haitozi kodi kwa teknolojia inayopunguza kuwachiliwa kwa kaboni.

Kwa hisia zake, iwapo serikali haitabadili sera hii inayokubaliwa na Wakenya wanaowekeza nishati mbadala, jamii inayoishi pembezoni ndio itafaidika zaidi kwa nishati ya jua, kwa sababu maeneo wanayoishi huwa na jua mwaka mzima.

“Watu wanaoishi pembezoni hawawezi kupata nguvu ya umeme inayosambazwa kitaifa, hivyo nishati mbadala ndio itawafaidi,” Ozor alisema.

Si wote wanaokubali. Wahakiki wanadai kwamba vifaa vya umeme wa jua ambavyo ni nafuu maeneo ya vijijini vyaweza tu kuhifadhi asilimia kumi hadi kumi na tano ya nishati ya jua inayonaswa, na kwamba haitoshi.

Kwa mujibu wa George Mwaniki, anayefanya kazi na kituo cha kitaifa cha mazingira, nishati ya jua haina faida kwa wawekezaji wadogo kwa sababu mifumo iliyopo inafaa kuzalisha mara kumi ya nishati ili kurudisha rasilimali iliyotumiwa kwa uwekezaji.

“Nadhani biogesi ni chaguo kamili la kuzalisha nishati mbadala,” alisema Mwaniki, ambaye pia ni mkurugenzi wa utafiti na machapisho katika shirika lake. “Lakini utafiti zaidi unafanywa ili kuzindua njia zilizo na faida kwa nishati mbadala.”

ERC yasema zaidi ya shule za msingi elfu moja zilizolengwa kwa mradi wa nishati vijijini zimewekewa vifaa vya nishati ya jua. Lakini maafisa wasema biogesi na nishati ya upepo zatarajiwa kuwekwa katika vituo hivi anzilishi.

Wengi kama Leleno wanategemea usambazaji wa nishati safi kutoka kwa serikali. Lakini hata kama kuna maendeleo, wachache wasema kwamba serikali haitafanikiwa bila msaada wa mashirika ya kimaendeleo kama vile Benki ya Maendeleo ya Afrika, Benki ya Dunia, na mashirika ya umoja wa mataifa.

“Tunaunga mkono jitihada za washirika wetu kwa sababu serikali peke yake haiwezi kuinua viwango vinavyotakiwa katika sehemu pembezoni mwa Kenya,” alisema Augustine Lembuonamati, mjumbe wa kamati ya maendeleo ya wilaya ya Samburu.

Kagondu Njagi ni mchangiaji wa kujitegemea kwa Thomson Reuters Foundation, mjini Nairobi na huandika juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa.