Source: http://www.trust.org/item/20131002155551-7mzy5/


Use of this content is subject to the following terms and conditions: http://www.trust.org/terms-and-conditions/



Tanzania yaruhusu wafugaji wa kimaasai kubaki kwenye korido ya wanyamapori


By Kizito Makoye | Wed, 2 Oct 2013 03:55 PM



DAR ES SALAAM, Tanzania (Thomson Reuters Foundation)- Serikali  ya  Tanzania  imetupilia mbali mpango wake wa kupora kilomita za mraba 1500(maili za mraba 580) za ardhi  kata ya Loliondo kaskazini mwa nchi kuanzisha korido ya wanyamapori katika eneo linalogombaniwa na maelfu ya wafugaji wa jamii ya kimaasai wanaolisha ng’ombe  wakati wa kiangazi.

  Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameagiza kwamba  wafugaji wa Kimaasai  waendelee kuishi ndani ya kilomita 1500 za mraba ( maili 580 za mraba) katika eneo hilo lililopo kaskazini mwa nchi, akibainisha kuondoka kwa  tangazo la serikali lililotolewa awali likiwataka watu hao kuondoka eneo hilo ili kupisha mpango wa uhifadhi wa wanyamapori na vyanzo vya maji.

 “Ardhi hii ingepaswa kuhifadhiwa, ni wazo zuri, hata hivyo, tumeamua kwamba wafugaji hawa wa Kimasai ambao wamekuwa wakiishi hapa kwa dahari ya miaka ni wahifadhi wazuri, wanaoweza kuzidi kutunza mazingira.” Alisema Pinda ambaye alisafiri hadi Loliondo kutoa tangazo hilo, huku akishangiliwa na mamia ya wafugaji waliojitokeza kumsikiliza.

Amri ya serikali iliyotolewa mwezi machi, ingalisababisha kuondolewa kwa maelfu ya wafugaji wa kimaasai katika maeneo ambaye serikali inayaelezea ni nyeti kwa uzalianaji wa wanyama na uhamaji maarufu wa wanyama aina ya nyumbu.

Baada ya mabadiliko ya tabia nchi kusababisha ukame, wafugaji wengi wa kimaasai wamepatwa na hali ngumu kukabiliana na upungufu wa maji na malisho ya ng’ombe bila ya kuingia maeneo ya hifadhi.

Serikali imekuwa ikiwatuhumu kuvamia vyanzo vya maji na mazalia ya wanyama pori.

“Watu hawa wamekuwa wakiishi hapa bila kibali,”Alisema waziri wa utalii na maliasili Khamis Kagasheki mwezi April. “Ardhi hii haikutolewa kwao katika mpango wowote wa serikali. Hata hivyo, ili kuwasaidia, serikali iliwaruhusu kuendelea kuishi hapo kwa miaka yote hiyo,”

Eneo la Loliondo limekuwa likigubikwa na migogoro ya ardhi tangu mwaka 1992, ambapo serikali iliamua kuanzisha shughuli za uwindaji kwenye eneo hilo na kukodisha sehemu ya ardhi kwa kampuni ya uwindaji ya Dubai Ortello Business Cooperation (OBC), inayojihusisha na shughuli za uwindaji.

Pori tengefu la loliondo linapakana na mbuga maarufu ya Maasai Mara upande wa kaskazini, hifadhi ya ngorongoro kusini na mbuga ya Serengeti magharibi. Ina zaidi ya watu 70,000 wengi wao wakiwa ni wafugaji wa kimaasai waliohamia hapo miaka ya 1950.

Chini ya sheria ya ardhi ya mwaka 1999, ardhi yote ya Loliondi ni ardhi ya kijiji. Mwaka 2008, serikali ilisaini makubaliano na kampuni ya OBC, kushawishi wafugaji wa kimaasai kuondoka eneo hilo kwa hiyari yao ili kupisha shughuli za uwindaji.

Wafugaji walikaidi ombi hilo na waliondolewa kwa nguvu na polisi mwezi July 2009. Takribani nyumba 350 zilichomwa na zaidi ya watu 20,000 waliachwa bila makazi. Zaidi ya asilimia 50 ya ng’ombe wao walikufa kwa kukosa maji na malisho.

 Mpaka sheria ya wanyamapori ya mwaka 2009 ilivyotungwa, kuanzishwa kwa pori tengefu hakukuwa na uhusiano na matumizi ya ardhi husika. Hata hivyo, sheria mpya inampa waziri wa maliasili na utalii mamlaka ya kuzuia shughuli za kilimo na ufugaji kwenye mapori tengefu.

 Maelfu ya wafugaji kaskazini mwa Tanzania wamekuwa wakipinga mpango wa serikali kupora ardhi yao, wakiishutumu kutumia uhifadhi wa wanyama pori kama kisingizio kuwaondoa kwenye ardhi ya mababu zao ambayo ni chanzo muhimu cha maji na malisho ya wanyama.

 Wafugaji hao wa wilaya ya Ngorongoro, wameeleza kwamba serikali ilikuwa imenuia kupora ardhi yao na kuiipa kampuni ya wawindaji ya OBC.

Amri iliyotolewa na waziri mkuu inaelekea kutoa suluhu ya mgogoro uliodumu kwa takribani miongo miwili.

“Naweza kukubaliana na watu hawa sasa, kuchukua ardhi ile huenda ikaathiri maisha yao na hilo si swala serikali inalolipenda.” Waziri mkuu Pinda alisema wakati akitembelea Loliondo

 Yannick Ndoinyo, diwani wa kata ya Ololosokwan huko Loliondo, alisema  kwamba wanavijiji hawatakesha tena bila usingizi wakihofia  kuhamishwa kwa nguvu.

Wanakarakati wa haki za binadamu wametoa tafsiri tofauti ya tangazo la serikali.

“ Nafikiri waziri mkuu ameonyesha mapenzi yake dhahiri kwa wafugaji wa kimaasai kwamba ardhi ile ni yao na vizazi vyao vijavyo, na kwamba hamna mtu hata mmoja  atawadhulumu tena” Alisema Susana NordLund, mwanaharakati  na blogu aliyewahi kuishi Tanzania, katika majibu wa barua pepe kwa swali aliloulizwa.

 Hata hivyo wengine walionya kwamba serikali haina msimamo wa pamoja katika kulinda maslahi ya wamaasai na hivyo huenda ikabadili mawazo muda wowote

“Tungependa kuwaeleza watu wa Loliondo kuhakikisha kwamba uamuzi wa serikali kupitia kwa waziri mkuu unawekwa kwa maandishi, kwa kumbukumbu za baadae,” alisema Onesmo Olengurumwa,  mratibu wa asasi ya utetezi wa haki za binadamu katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Waziri Mkuu ameagiza kwamba wenyeji wa eneo hilo na wawekezaji kuandaa mpango endelevu wa matumizi ya ardhi ili kuhakikisha uhifadhi wa mazingira, kinga kwa wanyamapori  na uhifadhi wa vyanzo muhimu vya maji.

Gazeti la Mwananchi lilimnukuu ofisa mtendaji wa OBC Isack Mollel akisema kwamba ingawa kampuni yake inakubaliana na maagizo ya serikali, kushindwa kulinda maeneo ya wanyamapori yasiharibiwe na shughuli za binadamu, ni pigo kuu katika mustakabali wa sekta ya utalii.

 Kizito Makoye ni mwandishi mwandamizi aliyepo Dar es Salaam.