×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Maofisa wa Tanzania, wakulima walaumiana kwa kunyauka mazao

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Monday, 29 April 2013 13:13 GMT

Farmers resist adopting unfamiliar drought-hit crops, arguing that government must come up with other responses to worsening drought

Na Kizito Makoye

SINGIDA, Tanzania (Thomson Reuters Foundation) –  Katika kijiji kilicho mbali cha Misigiri, kila mkulima ana hadithi ya kusimulia kuhusu ukame uliowasukuma pembezoni mwa baa la njaa.

Majaliwa Mrisho, mkulima mdogo, alitanabahi ukweli mchungu kuona zao lake la mahindi likinyauka kabisa licha ya jitihada zake kufufua baadhi ya mimea kwa kutumia maji ya kisima.  Anaamini kwamba wakulima wanaonishi kwenye bonde la ufa la Tanzania wana kila sababu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ili kuweza kuishi.

‘‘Nimeshtushwa sana. Hili ni jambo jipya kabisa. Mvua kwa kawaida huwa ya kutosha kutuwezesha kuwa na zao nzuri, lakini mwaka huu mambo yameenda mrama,” alisema.

Ukame umekuwa tatizo sugu katika eneo la bonde la ufa na viongozi wa serikali wanasema wamekuwa wakijaribu kuelimisha wakulima kulima mazao yanayostahimili ukame, hata hivyo bila mafanikio. Wakulima wanadai kwamba ni lazima serikali iweke mpango kabambe na endelevu kukabiliana na ukame.

Katika ukame uliolikumba eneo hili hivi karibuni, zao la mahindi, ambalo ni zao la chakula limeshambuliwa mno, huenda maelfu ya wakulima wakakabiliwa na njaa kiasi cha kuhitaji msaada wa chakula hadi msimu ujao.

‘‘Hatukuileta hali hii. Tumeambulia kuwa wahanga wa hali halisi...sasa tunahitaji msaada ili tuziepushe familia zetu na njaa,” alisema Mwajuma Zakayo, mkulima mwingine wa Misigiri.

Wilaya ya Iramba ni miongoni mwa wilaya nyingi zilizoathiriwa na ukame, uliosababisha uhaba mkuu wa chakula  huku ukipaisha bei za nafaka.

Mahojiano na wachuuzi 242 na wakulima huko Singida, wilaya za Iramba na Kiomboi yanaonyesha wakaazi wengi wangali wakihangaika kununua chakula kinachouzwa kwa bei kubwa.

Bei ya mahindi imeongezeka maradufu tangu mwaka jana, mchele na maharagwe navyo vimeongezeka sana tangu ukame uanze.

Wakulima wanakiri kuwa hawakusikiliza maelekezo ya serikali kuzalisha mazao mbadala, kama vile mhogo, ili kuzilinda familia zao na tishio la baa la njaa.

Mrisho, mathalani, amekuwa akizalisha mahindi, maharagwe na karanga kwa miongo kadhaa sasa, hakuona umuhimu wa kulima uwele na mtama. ‘‘Kamwe sijawahi lima mtama, sikuona umuhimu mpaka ukame ulivyo tukumba...niliona ni hatari kuzalisha zao nililo na uzoefu nalo.”

Wakulima wengine wanasema familia zao hupenda mahindi zaidi ya mazao mengine yastahimiliyo ukame, kama vile muhogo.

Wakulima kadhaa wameiambia Shirika la Thomson Reuters huko Singida kwamba wasingependa kulima na kula chakula wasichokipenda, wakiongeza kuwa mahindi ndiyo zao wanalolipenda kwa kuwa familia zao zimekuwa zikilizalisha tangu vizazi.

‘‘Watoto wangu hupenda ugali zaidi ya kitu chochote, kwa kuwa unawapa nguvu. Nawezaje kuwapa ugali wa mtama?’’ Alihoji Jaka Naligia, mkulima mwenye miaka 47 huko Iramba.

Boniphace Temba, mhazili katika maswala ya utawala wa mkoa wa Singida amesema jitihada za kushawishi wakulima walime mazao mbadala zimeshindwa.

‘‘Tumejitahidi kadiri ya uwezo wetu kushawishi wakulima wabadili mtazamo na kuanza kuzalisha mazao yanayostahimili ukame, hata hivyo mwitiko si mzuri...unapowaambia kuhusu mtama wanadharau tu” Temba aliiambia Shirika.

Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imesema zaidi ya kaya 37,000 wilaya ya Iramba zinakabiliwa na upungufu wa chakula, na familia maskini hushindwa kumudu chakula cha kununua.

Wakati mahitaji ya kila mwaka ya nafaka kwa wilaya hiyo ni tani 58,360, msimu wa 2011/12 zilizalishwa tani 14,380 tu, wizara imesema. Tathmini ya wizara hii wilayani Iramba inaonyesha zaidi ya kaya 16,000 zinakabiliwa na njaa.

Mkuu wa mkoa Singida Parsekpo Kone, amesema mgao wa chakula utafidia upungufu uliopo mpaka msimu ujao.

Takwimu za mamlaka ya hali ya hewa zinaonyesha kwamba mkoa wa Singida ulipata milimita za mvua 580 msimu uliopita, kiwango cha chini kabisa kuwahi kunukuliwa.

Wakati wakulima wakilaumu ukame kama ni chanzo cha njaa, serikali inalaumu wakulima kutozingatia namna bora ya kutunza mazao. ” Baadhi ya wakulima walipata mazao mazuri lakini hawakuyatumia ipasavyo. Baadhi ya watu waliamua kutengeneza pombe kwa kutumia mahindi” alisema Kone.

Hata hivyo wakulima wamesema serikali ndiyo ya kulaumiwa kwa kushindwa kuweka sera maridhawa katika kukabiliana na ukame. Baadhi ya familia ya wakulima wamekuwa wakila matunda ya mbuyu, na baadhi ya wanaume wametoroka kwenda mijini kutafuta riziki.

Wachambuzi wanasema kwamba iwapo wakulima wanagoma kuzalisha mtama, ni vyema wakipewa mbegu za mahindi zinazostahimili ukame na zinazokuwa kwa muda mfupi. Serikali imeshindwa kutumia tafiti kama vile Water Efficient Maize for Africa (WEMA) ambazo zingesaidia sana kupunguza hasara kwa wakulima.

”Kuna aina mbalimbali ya mahindi yanayostahimili ukame ambayo huenda yakasaidia sana  wakulima wakati wa ukame. Sielewi ni kwa nini  serikali isipeleke mbegu hizo kwa wakulima hawa maskini ili wakabiliane na kizungumkuti cha kulima mazao wasiyoyapenda,” Alisema Prosper Ngowi, mtaalam wa uchumi na mhadhiri katika Chuo kikuu cha Mzumbe Dar es salaam.

Mwaka jana, wakulima katika kijiji cha Makutupora, huko Dodoma walisema kwa kutumia mahindi yanayostahimili ukame  wameweza kuongeza mavuno kwa asilimia 50.

Kizito Makoye ni mwandishi mwandamizi aliyepo Dar es Salaam

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->