×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Je, Kenya yaweza kunasa maji ili kuzalisha mahindi maradufu?

by Isaiah Esipisu | @Andebes | Thomson Reuters Foundation
Friday, 28 February 2014 07:15 GMT

A farmer stands with an irrigation rig in Kenya. THOMSON REUTERS FOUNDATION/Isaiah Esipisu

Image Caption and Rights Information

To improve food security in the face of climate change, Kenya has embarked on an ambitious irrigation farming project on one million acres of land, aiming to double its maize production in five years

NAIROBI, (Thomson Reuters Foundation) – Katika juhudi za kuimarisha uhakika wa chakula licha ya mabadiliko ya tabianchi, serikali ya Kenya imeanzisha mradi wa kunyunyiza maji kwa ekari milioni moja za arthi, jambo ambalo litawezesha nchi hiyo kuzalisha mahindi maradufu katika kipindi cha miaka mitano.

Huu ni msukumo wa makusudi ili kukabiliana na jitu ambalo ni mabadiliko ya tabianchi, asema James Nyoro, mshauri maalum wa serikali ya Kenya kwa maswala ya kilimo – katika mahojiano kwa mkutano ulioandaliwa na shirika la AGRA. Na ni bora kutenda hili mapema kwani hali ya hewa inazidi kubadilika kutoka ruwaza inayojulikana hadi ile isiyojulikana, hivi kwamba, hatuwezi kuitegemea, asema mshauri huyo.

Africa ya Mashariki kwa hivi sasa inakabiliwa na mvua kubwa iliyoanza mnamo mwezi wa pili bila kutarajiwa. Huu ni mwezi mmoja kabla msimu wa mvua wa kawaida. Hivyo basi, Nyoro anaamini kuwa mvua hiyo isiyofwata utaratibu yaweza kutatiza msimu wa mvua wa miezi za Machi na Aprili.

Nyoro asema kuwa, hakuna njia nyengine, ila kukabiliana na hali hiyo ya hewa inayozidi kubadilika. Na njia moja ya kukabiliana, asema bwana huyo, ni kuegeza katika kilimo cha kunyunyiza.

Mradi huo wa kunyunyiza katika hekari milioni moja, ambao unatarajiwa kugarimu shilingi bilioni 250 katika muda wa miaka mitano ulizinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mnamo mwezi wa Januari, ili kusuluhisha shida sugu ya upungufu wa chakula nchini Kenya.

Mradi huo utanyunyiza maji katika ardhi ya serikali katika sehemu kame ya jimbo la Tana River na lile la Kilifi katika pwani ya Kenya. Ardhi hiyo ilinunuliwa na serikali kutoka kampuni ya Galana Game and Trading Company mnamo mwaka wa 1989.

Kulingana na mpango wa serikali, ekari nusu milioni ya ardhi hiyo itatumiwa kuzalisha mahindi, ekari elfu mia mbili kukuza miwa, na ekari elfu mia tatu itatengewa mambo mengine kama vile kufuga ng’ombe wa nyama, wanyama wa porini, samaki na kadhalika.

Kulingana na Felix Koskei, waziri wa kilimo, mradi huo utaongeza uzalishaji wa mahindi hadi magunia milioni 45 kwa kila mwaka, badala ya magunia milioni 20 ambazo huzalishwa nchini humo kwa sasa.

Waziri huyo alisema kuwa maji ya kunyunyiza itatolewa katika mto Sabaki, ambao uchunguzi wa mapema uliofanywa na kampuni tatu zenye asili ya Israeli, umebainisha kuwa una maji ya kutosha kwa mradi huo.

Uchambuzi wa udongo uliofanywa na taasisi ya utafiti wa kilimo nchini Kenya unaonyesha kwamba sehemu hiyo ina uwezo wa kutoa mazao mengi, kati ya magunia 30 na 50 ya mahindi kwa kila hekari moja kila mwaka.

Kulingana na wizara ya kilimo, Wakenya hutumia wastani magunia milioni 3.72 ya mahindi kila mwezi, kwa jumla magunia milioni 44.64 kila mwaka kinyume na magunia milioni 20 ya mahindi yanayozalishwa nchini humo kila mwaka. Kiwango cha ulaji kinaongezeka kila mwaka kulingana na idadi ya watu inayoongezeka, ambayo kwa sasa ni watu milioni 40.

Upungufu wa mahindi kwa kawaida hujazwa kwa kununua mazao hayo kutoka soko la nje haswa Tanzania na Uganda.

Lakini kutokana na hali ya hewa inayozidi kubadilika, wataalam waonya kuwa nchi nyingi, haswa Afrika chini ya Sahara zitapata mazao duni mnamo siku zijazo. Hivyo basi, Asema Dennis Garrity, ambaye ni balozi wa sehemu kame katika Umoja wa Mataifa, ni lazima tutarajie mazingira magumu katika siku zijazo. Hiyo ndiyo sababu ya kuekeza katika miradi za kukabiliana na hali hii.

Mavuno kutoka kwa mradi wa kunyunyiza kwa ekari hizo milioni moja yatahifadhiwa katika hifadhi ya nafaka ya kitaifa, na kutolewa wakati yanahitajika, alisema Koskei.

Kulingana na Nyoro, Kenya ina sehemu zingine nyingi ambazo zinalengwa kuzalisha chakula kwa kunyunyiza.

Sehemu mpya zaidi, ambayo wataalam wasema ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kulisha nchi nzima ya Kenya ni sehemu kame ya jimbo la Turkana, ambayo wakaazi wake kwa sasa wanakabiliwa na njaa kubwa, huku wakitegemea vyakula vya misaada kutoka kwa serikali na mashirika ya kibinadamu.

Jimbo hilo limepatikana kuwa na maji chini ya arthi ambayo wataalam wasema yaweza kutumiwa na watu wote nchini Kenya kwa miaka 70, ikizingatiwa idadi ya watu inayozidi kuongezeka.

Serikali inapanga kuanzisha mradi mwingine wa kunyunyiza katika jimbo la Turkana kwa kutumia maji hayo yaliyo chini ya arthi, kama njia ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kutumia maliasili, asema Nyoro.

Kwa hivi sasa, serikali imefanya mkataba na Davis and Shirtliff, kampuni kubwa ya maji, ili kuchimba visima ndiposa maji hayo yatumike kwa kunyunyiza, asema John Nyaoro, Mkurugenzi wa Maji katika wizara ya mazingira.

Ingawa Kenya imeamua kunyunyiza kwa kiwango kikubwa katika majimbo ya Tana River na Kilifi, utafiti wa mwaka wa 2013 uliofanywa na Jennifer Burney kutoka Chuo Kikuu cha Stanford unaonyesha kuwa unyunyizaji katika sehemu ndogondogo una uwezo wa kupunguza njaa, kuimarisha mapato, na kuchochea maendeleo haswa katika nchi zinazoendelea.

Kulingana na shirika la umoja wa mataifa kwa chakula na kilimo, ni asili mia nne pekee ya ardhi ya kilimo chini ya Sahara barani Afrika inayonyunyiziwa. Hii ni kumaanisha kuwa ardhi zingine zote za kilimo zimo hatarini ya kutatizwa na madhara ya hali ya hewa kama vile kiangazi na mafuriko.

Isaiah Esipisu ni mwandishi wa kujitegemea, mkaazi wa Nairobi, na maalumu kwa kuripoti maswala ya kilimo na mazingira. Anaweza kupatikana kupitia esipisus@yahoo.com

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->