Maziwa yafurika Kenya na kutatiza masomo, mamba nao wakaribia vijiji

by Caleb Kemboi | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 10 June 2014 11:50 GMT

Rift Valley lakes have been rising due to heavy rains and deforestation, flooding villages

BARINGO, Kenya – Katika shule ya msingi ya Salabani ufuoni mwa Ziwa
Baringo, magharibi mwa Kenya, mwalimu Rehema Lewer anaendesha somo la
Kiswahili chini ya mti. Lakini wanafunzi hawako nje ili kufurahia
upepo mwanana – wamelazimishwa kwa sababu ya maji ya ziwa ambayo yamefurika na kushinikizwa kuacha shule yao na kuhamia eneo la muinuko ambako maji
hayo hayajafika.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Maziwa yaliyoko Magharibi
mwa Kenya – ziwa la maji safi la Baringo na lile la maji ya chumvi la
Bogoria – yamekuwa yakishuhudia ongezeko lisilo la kawaida la maji, na
kupelekea mafuriko makubwa ambayo yameathiri vijiji viliyoko karibu.
Baada ya mvua iliyoshuhudiwa katika eneo hilo mwezi wa Aprili, maziwa
hayo yaliyofurika na kusomba vituo vitatu vya matibabu, hoteli kadhaa
za watalii na shule 10, ikiwemo ile ya Salabani.

“kufunza chini ya mti ni salama,” alisema mwalimu Lewer. “Lakini kuna
changamoto chungu nzima.” Ikiwemo mamba.”

Huku maji ya Ziwa yakikaribia vijiji, mamba nao wanaogelea na
kusogelea karibu na nchi kavu. Mamba hao wanaweza wakaonekana
wakitambaa kwenye barabara vijijini na wengine hata wanalala mbele ya
milango ya nyumba za wenyeji.

Mmoja wa wenyeji hao alisema mamba hao walikuwa wamekula mbuzi wake
wawili wakipekee, naye mvuvi alisema yeye pamoja na kundi lake tayari
wamewahi ponea mashambulizi kadhaa walipokuwa wakiendesha shughuli zao
za uvuvi kwenye ufuo wa ziwa.

“Wanafunzi wanaotoka mbali na shule, wanalazimika kutumia mitumbwi,
hivyo wako kweye hatari kubwa ya kuvamiwa na mamba,” alisema Lewer.
“Hali hii inafanya kuwa vigumu sana kwa watoto waliombali na shule
kuhudhuria masomo kila siku.”

Serikali ya kaunti ya Baringo imebuni kitengo cha kushughulikia
majanga ili kusaidia kukabili athari zinazotokana na mafuriko, lakini
Gavana Benjamin Cheboi alisema kitengo hicho kinakumbwa na uhaba wa
fedha. “ Tunahitaji fedha zaidi ili kusaidia kurejesha mali
iliyoharibiwa na mafuriko, na kutoa msaada wa chakula na mavazi kwa
waathiriwa,” alisema.

Nyingi ya shule zilizoathirika zimeamua kutumia maeneo ya mda kama
hema ama kutoa mafunzo kwa wanafunzi kwenye eneo wazi, alisema. “Kwa
sasa tuko kwenye mchakato wa kuhamisha hadi maeneo ya juu shule husika
na taasisi zingine za umma, shughuli hii inahitaji fedha,” aliongeza.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi ya Salabani, Moses Longochila, alieleza
jinsi alivyofika shuleni humo siku moja na kupata sehemu ya madarasa
na afisi zikiwa zimefurika maji. “Tuliona kiwango cha maji katika ziwa
kikiongezeka polepole sikui baada ya siku,” alisema. “Hatuna habari
kuhusiana na kwa nini hili linatokea. Jamii ya eneo hili
imechanganyikiwa, na hatujui kile kitatokea baada ya hapa.”

UKATAJI MITI

Karibu na ziwa Baringo, kuna ziwa Bogoria ambalo pia limekuwa
likishuhudia ongezeko la kiwango cha maji yake katika miaka michache
ya hivi karibuni na kutatiza shughuli za binadamu na wanyama.

Ziwa hilo lenye maji ya chumvi, ambalo ni mojawapo ya maeneo sita
nchini Kenya yaliyoorodheshwa na shirika la umoja wa mataifa la Elimu,
sayansi na Teknolojia-UNESCO, ni makao kwa ndege aina ya Flamingo
mbali na kuwa na umaarufu kwa chemichemi yenye moto na gesi.

James Kimaru, afisa mkuu msimamizi katika hifadhi ya kitaifa ya
wanyama ya Ziwa Bogoria, alisema idadi kubwa ya mvua na mafuriko
yanayotokea baadaye imeathiri pakubwa utalii.

“Ziwa hili hapo awali lilikuwa na upana wa kilomita 32 mraba lakini
kwa sasa ni kilomita 41 mraba,” alisema. “Kiwango cha chumvi katika
ziwa hili kimepungua, na kulifanya karibu kuwa na maji safi, hili
limesababisha kupungua kwa idadi ya ndege aina ya Flamingo.” Mafuriko pia
yameharibu barabara zinazoelekea kwenye chemichemi za moto na kufanya
kuwa vigumu kwa watalii kuzifikia.

Wataalam bado hawana uhakika wa kinachosababisha maji kwenye Maziwa
magharibi mwa Kenya kuongezeka, lakini wanazungumzia mchanganyiko wa
mabo mbalimbali ikiwemo kusonga kwa miamba iliyoko chini ya ardhi,
ongezeko la mvua, matope na kupungua kwa mimea katika ardhi.

Kwa mujibu wa mwanajiolojia mkuu katika eneo la Rift Valley Enock
Kipseba, kiwango cha mvua isiyokuwa yua kawaida na kupungua kwa eneo
la misitu ndio baadhi ya mambo ya kulaumiwa. “Kutokana na ukataji miti
kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo, kumekuwepo na mmomonyoko wa
udongo na kupotea kwa mawe kandokando mwa Maziwa yanayobebwa na maji
ya mito na kusafirishwa hadi kwenye ziwa,” alisema. Wakati udongo na
mawe vinavyojikusanya, inasukuma juu maji hivyo kupelekea hali
inayoshuhudiwa kwa sasa.

Alfred Kurgat, afisa mkuu wa uhifadhi mazingira katika shirika la
huduma za misitu nchini Kenya, anaamini kwamba suluhu ni kupanda miti
zaidi, ili mizizi ya miti hiyo izuie kusafirishwa kwa udongo na mawe
yanayobebwa na maji hadi kwenye Maziwa.

Gavana wa Baringo Benjamin Cheboi alisema serikali yake inapanga
kuzindua mradi mkubwa wa upanzi wa miti kwneye vilima vya Tugen na
Msitu wa Chemosusu kwenye eneo la Rift Valley, kama sehemu ya kampeini
inayolenga kulinda mazingira dhidi ya kuharibiwa.

WITO WA MSAADA WA KIMATAIFA

Kwa David Kimosop, mkurugenzi mkuu wa halmashauri ya maendeleo katika
eneo la Kerio Valley, kipaumbele ni kubainisha chanzo cha
mafuriko hayo. Alitoa wioto kwa watafiti wa maswala ya hali ya anga na
mashirika husika kutenga mda zaidi kuchunguza kinachosababisha
kuongezeka kwa kiwango cha maji katika maziwa ya Rift Valley.

“Kama njia ya kukabili hali hii, kuchimba mitaro kandokando mwa Maziwa
kutasaidia kuzuia mafuriko kuharibu mali na nyumba za wenyeji,”
aliongeza.

Moses Ole Mpaka, mwanaharakati wa haki za kibinadamu mwenye makao yake
katika kaunti ya Baringo, anaamini kwamba njia bora ya kukabili
mafuriko katika eneo hilo ni kwa hali hiyo kuangaziwa katika ngazi ya
kimataifa. Anataka wenyeji na wataalam kutoka maeneo hayo kualikwa
kwenye mazungumzo ya umoja wa mataifa kuhusu mabadiliko ya anga kule
Peru mwezi Desemba mwaka huu, ambako watatafuta usaidizi wa kubuni
sera itakayosaidia kukabili hali hiyo siku za usoni.

“Kumekuwepo na majadiliano mengi kimataifa kuhusu mabadiliko ya hali
ya anga, na kwa sasa ni sisi tuhuathirika,” alisema. “ Tunaomba tupewe
nafasi ya kuwa sehemu ya kongamano zinazoangazia maswala ambayo
yanatuathiri. Hicho ndicho kilio chetu.”

Gavana Cheboi pia anatumai wataalam wa kimataifa watasaidia kutegua
kitendawili cha kinachopelekea Maziwa ya eneo hilo kufurika.
“Inatupasa tushirikiane ili kutafuta suluhu,” alisema. “Tatizo hili
haliwezi likapuuzwa.”

Wakati hayo yakijiri, kadiri mafuriko katika eneo la Rift Valley mwa
Kenya yanapoendelea bila suluhu kupatikana, ndivyo maisha yanazidi
kuwa magumu hata zaidi kwa wanaoishi katika maeneo hayo. “Hali tayari
ni mbaya zaidi,” alisema mkaazi wa Baringo, Fancy Lorien. “Lakini
tunahofu mabaya zaidi yako njiani.”

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.