×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Wavunaji haramu wa misitu wenye silaha waangamiza misitu pwani ya Tanzania

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 13 January 2015 00:00 GMT

Mahmood Hamis, a resident of the village of Mafia, trims a plank of wood at his dhow-making factory on Mafia island, in Tanzania's Coast region in November 2014. THOMSON REUTERS FOUNDATION/Kizito Makoye

Image Caption and Rights Information

“Guards do not have the capacity to confront” armed loggers working at night, authorities say

DAR ES SALAAM, Tanzania Jan 13 (Thomson Reuters Foundation) - Ongezeko kubwa la ukataji haramu wa misitu linaharibu miti ya asili kwenye pwani ya Rufiji nchini Tanzania licha ya jitihada zinazofanywa na mamlaka husika kupunguza tatizo hilo, wamesema maofisa misitu.

Mamia ya tani za mbao yanatoroshwa nje ya wilaya kila mwezi na wafanyabiashara wakubwa wa mbao na kusafirishwa hadi kwenye viwanda vya samani na ujenzi ndani na nje ya nchi, walisema maafisa wa wilaya ya misitu.

Rekodi ya wilaya inaonyesha, wakataji haramu wa misitu, ambao mara nyingi huvamia misitu nyakati za usiku, hukata aina ya miti adimui kama vile mninga na mpodo, ambazo kwa sasa zinatoweka kutokana na mahitaji makubwa ya mbao zake kwenye viwanda vya samani.

“Wavamizi hao wanaonekana kuwa na maandalizi ya kutosha pia wana silaha. Kwa bahati mbaya walinzi wetu wa misitu hawana uwezo wa kuwakabili,” alisema Shamte Mawawa, afisa mtendaji wa kijiji  cha Mangwi huko Rufiji.

Misitu ina nafasi muhimu sana  kupunguza joto la dunia kwa kuondoa hewa ukaa kwenye anga inayoweza kupunguza ongezeko la joto la dunia.

Tathmini iliyofanywa na chama cha Waandishi wa habari kuhusu mazingira - Journalist Environmental Association of Tanzania (JET) Novemba ilisema ukataji holela wa misitu inakolezwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya mbao na uchomaji wa mkaa pamoja na ukosefu wa mikakati ya maksudi kudhibiti uharibifu wa misitu wilayani humo.

Nurdeen Babu, mkuu wa wilaya ya Rufiji ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya uvunaji misitu,  ameiambia Thomson Reuters Foundation kwamba ukataji holela wa misitu wilayani humu unatishia  ustawi wa misitu ya asili, hata hivyo, aliongeza serikali imechukua hatua kukomesha tatizo hilo.

“Tumeimarisha ulinzi kwa kuongeza idadi ya walinzi wa misitu. Yeyote atakayeonekana akifanya shughuli yoyote isiyoruhusiwa ndani ya msitu atakamatwa na kushtakiwa kwa mujibu wa sheria,” Babu alihimiza.

Hata hivyo, kuwanasa wakataji holela wa misitu ni vigumu. Licha ya maelekezo ya mara kwa mara yanayotolewa na serikali, ukataji haramu umekuwa ukiendelea bila kusita huku miti mingi ikikatwa ndani ya msitu mnene kukwepa mamlaka, alisema.

Misitu ya Rufiji inakabiliwa na shinikizo kubwa kwa takribani muongo mmoja kutokana na ongezeko la watu, ukataji holela wa mbao, ongezeko la kilimo na matumizi ya kuni, maafisa uhifadhi wasema.

Tanzania ina hekari million 33 za misitu na miti ya mbao, hata hivyo, nchi hiyo imekuwa ikipoteza takribani hekari 400,000 ya misitu kwa mwaka kwa miongo miwili mfululizo, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo kwenye utafiti wake wa 2010 ujulikanao kama Forest Resources Assessment.

Katika harakati ya kupunguza ukataji haramu wa misitu, serikali mwaka 2010 ilianzisha shirika huru lenye dhamana ya kusimamia ustawi wa misitu lijulikanalo kama Tanzania Forests Services Agency. Hata hivyo, shirika hilo limeshindwa kusimamia vilivyo rasilimali ya misitu, alisema Felician Kilahama, afisa misitu mwandamizi mstaafu aliyekuwa akifanya kazi katika idara ya misitu na nyuki wizara ya maliasili na utalii.

ASILIMIA 96 YAKATWA HOLELA

Afisi ya mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ilitoa taarifa mwaka 2012 inayosema takribani asilimia 96 ya misitu inayokatwa Tanzania inakatwa kinyume cha sheria. Ukataji huo holela ni matokeo ya mipango mibovu ya serikali kushindwa kusimamia rasilimali misitu, ilisema.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ukataji haramu wa misitu, unaoathiri sana mapato ya serikali ni jambo lenye kutia shaka nchini Tanzania.

Wizara ya Utalii na Rasilimali, kwa mfano, ilisema nchi imepoteza takribani shilingi billion 23 ($13.5 million) katika mauzo ya mazao ya misitu kati ya mwaka 2011-2012 kutokana na ukataji haramu wa misitu.

Huko Rufiji, rekodi ya mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya misitu zinaonyesha zaidi ya asilimia 70 ya mazao yote ya mbao hayajulikani yanapokwenda, kiasi cha kusababisha hasara kubwa ya mapato ya serikali kutokana na ushuru, na kodi mbalimbali.

Wakazi wa Rufiji wanawatuhumu maafisa wa msitu wa Rufiji kwa kushirikiana na wahalifu. Walisema maafisa hao mara nyingi hutoa vibali au kuruhusu utoroshwaji wa shehena haramu za mbao.

Naibu Afisa mtendaji mkuu wa Wilaya, Adinad Mwenda, hata hivyo, alikanusha tuhuma hizo akisema wenyeji wa hapo pia wamechangia kukata miti holela.

Wakati taratibu za serikali zinasema kwamba ukataji wa misitu inayozunguka wilaya uangaliwe kwa karibu na miti yote inayokatwa igongwe muhuri baada ya kuthibitishwa imekatwa kihalali, wakaazi wamesema hatua hizo si kila mara zinafuatwa.

Kwa mujibu wa wakazi, magogo hutoroshwa kupitia njia za panya na wahalifu wakisaidiwa na maofisa wa polisi ambao mara nyingi hujifanya kukagua magari ili wabaini mbao zinazoibiwa, kumbe wanasaidia wahalifu kutimiza dhamira yao ovu.

“Sina imani na jeshi la polisi hata kidogo. Mara nyingine hukamata washukiwa wa uhalifu na kuwaachilia bila mashtaka yoyote,” Alisema Justin Mfinanga, wa kijiji cha Ikwiriri.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani Ulrich Matei, hata hivyo alikanusha tuhuma hizo, akisema jeshi la polisi linafanya kazi kwa mujibu wa taratibu.

“Ninakupa changamoto kuleta majina ya afisa yeyote anayeshirikiana na wahalifu. Wataadhibiwa.” Alisema.

Tatizo mojawapo linalodhoofisha juhudi kupunguza uvunaji haramu wa misitu ni kwamba faini na tozo mbalimbali ni ndogo mno ukilinganisha na makosa yenyewe, maofisa wa misitu walisema.

Mharifu anayekamatwa na shehena ya mbao zenye thamani ya shilling Milioni 100 ($59,000) huenda akatozwa faininya shilling 500,000 ($294), walisema.

"Faini hizi ndogo haziwafanyi wahalifu kuacha shughuli zao haramu kwa kuwa wanaokosea huweza kumudu kuzilipa,” alisema Athumani Lunduli, afisa muhifadhi wa misitu kijiji cha Chumbi Rufiji

(Imeripotiwa na Kizito Makoye; kuhaririwa na Laurie Goering)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->