×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Unyunyuziaji mashamba maji waongezeka barani Afrika

by Justus Wanzala | Thomson Reuters Foundation
Friday, 9 September 2016 15:06 GMT

A farmer works in an irrigated field near the village of Botor, Somaliland April 16, 2016. REUTERS/Siegfried Modola

Image Caption and Rights Information

Haja ya kunyunyuzia mashamba maji inaongezeka lakini, haki ya wanawake kumiliki ardhi, kupatikana kwa kawi safi, mikopo pamoja na mafunzo vinahitajika

Na Justus Wanzala

STOCKHOLM, Septemba  9 (Wakfu wa Thomson Reuters) – Mataifa ya Afrika  Kusini mwa jangwa la Sahara yanashuhudia ongezeko la wakulima wanaomiliki viapande vidogo vya ardhi wanaotaka kunyunyuzia mashamba yao maji kutokana na hali ya anga isiotabirika. Wataalam  wa kilimo na maji wanadokeza pia  kuwa haja ya kunyunyuzia mashamba maji inatokana  na ongezeko la haraka la idadi ya watu kwenye mataifa kama vile  Nigeria na Kenya, hali inayochangia haja ya kuzalisha chakula zaidi.

Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti kuhusu sera za Chakula  (IFPRI) inakadiria kuwa zaidi ya hekari  milioni moja zinazomilikiwa na wakulima wenye vipande vidogo  vya ardhi zinanyunyuziwa  maji katika kanda hii, kwa mujibu  wa  takwimu za serikali na picha za Satelite.

Nchini Tanzania, eneo la ardhi  lenye mashamba madogo madogo  yanayonyunyuziwa maji  limeongezeka kutoka hekari  33,500 mnamo mwaka  2010  kufikia takriban hekari  150,000 kwa sasa, kulingana na IFPRI. Hata hivyo, mtafiti wa taasisi hiyo Ruth Meinzen-Dick, anasema hekari milioni 29 kwenye nchi hiyo ya Afrika Mashariki zinaweza kunyunyuziwa maji.

Kuimarika kwa unyunyuziaji mashamba  maji kunaweza kuchangia usalama wa chakula katika mataifa  yaliyoko  kusini mwa jangwa la Sahara hasa ikikumbukwa kuwa eneo hilo linazidi kuathirika na mabadiliko ya hali ya hewa. Hali hiyo pia inaweza kuchochea  ustawi, Ruth na wenzake waliohudhuria kongamano la Kimataifa kuhusu Maji mjini  Stockholm nchini Sweden walisema hayo.

 

"Unyunyuziaji maji kwenye mashamba madogo madogo ni njia moja ya kukabiliana na mabadiliko  ya hali ya hewa," alisema  Dawit Mekonnen, Mtafiti wa IFPRI  aliyeko nchini  Ethiopia.

UPANUZI

Ongezeko la idadi ya wakulima wanaonyunyuzia mashamba maji limetokana sio tu na hali mbaya ya hewa lakini pia  limechangiwa na kupatikana kwa pampu za nafuu kutoka China katika mwongo mmoja uliopita. Hayo ni kwa mujibu wa Jennie Barron, Mtafiti wa matumizi ya maji katika Taasisi ya Kimataifa kuhusu usimamizi wa maji (IWMI).

Hata hivyo ili kuongeza zaidi idadi ya  wakulima wanaonyunyuzia vipande vya ardhi maji, kutahitaji mabadiliko mengi. Mabadiliko hayo ni kama vile kupunguzwa kwa ushuru unaotozwa pampu zinazoagizwa kutoka nje pamoja na utoaji wa mafunzo kwa wakulima hasa wanawake kuhusu ujuzi wa kisasa wa kunyunyuzia maji mashamba, watafiti walisema.

Kuhakikisha wanawake ambao ni nusu ya idadi ya watu wanaofanya kazi katika sekta ya kilimo wanamiliki ardhi kisheria ni muhimu  katika kuhakikisha wanawekeza fedha zaidi  kwenye  kilimo  kupitia unyunyuziaji mashamba yao maji, walidokeza wataalam hao. "Wanawake  hugandamizwa  zaidi kwani hawamiliki ardhi au mali," alisema Barron.

Mekonnen alisema unyunyuziaji mashamba maji unazidi kuwa njia muhimu ya kuwasaidia wakulima kwenye mataifa kama vile Ethiopia, Ghana na Tanzania kukuza chakula  cha kutosheleza  mahitaji ya jamaa wao kwa mwaka mzima na pia kupata fedha kwa kuuza chakula cha ziada wakati bei imeongezeka. 

VIKWAZO

Shida moja aliotaja ni kwamba mataifa ya Kusini mwa Jangwa la Sahara hayajatengeneza ramani ya rasili-mali yake ya maji yalioko chini ya ardhi, hali ambayo inachangia wakulima wenye vipande vidogo vya ardhi kutofahamu yaliko maji.

Uimarishaji wa uvunaji wa maji ya mvua na ujenzi wa mabwawa madogo madogo ili kuyakusanya maji ya mvua ardhini  unaweza kuwasaidia wakulima hasa kwenye maeneo ambayo hayana maji ya chini ya ardhi, walisema wataalam.

Kutokana kwamba kusambaza maji kunahitaji kawi, kuwasaidia wakulima wenye vipande vidogo  vya ardhi kupata kawi safi kama vile kawi ya jua na  ile inayotoka kwa upepo  pia  kutawawezesha  kunyunyuzia mashamba yao maji, alisema, Mekonnen.

Kuwepo kwa  fedha kutoka  hazina za vilabu vya kuchanga fedha za  akiba  ili kuweza kutolewa kama mikopo ikiwemo taasisi za kifedha za kutoa mikopo  ndogo ndogo, pia kutachangia wakulima  wenye vipande vidogo vya ardhi kumudu gharama ya vifaa vya kunyunyuzia mashamba yao maji, walisema wataalam.

Hata hivyo, Tim Prewitt,  Afisa Mkuu Mtendaji wa shirika  la kimataifa  la kutoa Misaada (IDE), alisema utoaji wa ufadhili  kwa wakulima wenye mashamba madogo madogo  bado  ni changamoto na hii ni kwa mujibu wa hali ambazo shirika lake  limekumbana nazo.

"Nchini Ghana tulianza  kushirikiana na mashirika 12 ya kifedha madogo madogo, lakini kwa sasa tumesalia na mashirika mawili tu," alisema na kueleza kuwa hali hiyo inatokana na  wakulima kushindwa kulipa fedha wanazokopa pamoja na gharama ya  juu kwa mashirika ya fedha kushughulikia mikopo hiyo.

Kulingana na IWMI, ni asili mia saba pekee ya mashamba kwenye mataifa ya Afrika yaliyoko kusini mwa jangwa la Sahara ambayo yananyunyuziwa maji, kiwango ambacho ni cha chini zaidi ikilinganishwa na maeneo  mengine duniani.  

(Uandishi ulitekelezwa na Justus Wanzala; Mhairi ni  Laurie Goering :; Tafadhali unapochapisha makala haya tambua Wakfu  wa Thomson Reuters, Kitengo cha misaada cha kampuni ya Thomson Reuters, kinachochapisha habari kuhusu  huduma za kibinadamu, mabadiliko ya hali ya hewa, haki za wanawake, ulanguzi  na haki za umiliki wa mali. Tembelea: http://news.trust.org/climate)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->