NAIROBI (Thomson Reuters Foundation) Itawezekana mabadiliko ya serikali nchini Kenya kuleta dhamira ya kisiasa ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na majanga mengine kama hayo?

Wiki chache zilizopita baada ya serikali mpya nchini Kenya kuapishwa, mafuriko yamewaua watu wengi, huku wengine wakilazimika kuhama makwao. Jambo hilo limesababisha majanga yatokanayo na hali ya hewa kuangaziwa kisiasa.

Mnamo Aprili 18, Naibu wa Rais William Ruto alisema kuwa mafuriko hayo yamesababisha vifo vya watu 60 na kulazimisha wengine 35,000 kuhama makwao.

Baadhi ya maeneo yaliyoathirika pakubwa ni eneo la Tana, ambapo familia zipatazo 6,000 zimepata hasara kubwa baada ya Mto Tana kuvunja kingo zake huku maji yakiharibu mimea mashambani. Wanavijiji wengine wamefariki dunia kwa kuzama.

Itakumbukwa kuwa, mnamo mwezi wa Agosti mwaka jana, zaidi ya watu 50 katika sehemu hiyo waliuawa kinyama wakati jamii mbili zilikuwa zikipigania maji na sehemu ya kulisha mifugo baada ya lishe kukauka kutokana na kiangazi.

Mithika Mwenda, ambaye ni katibu mkuu katika shirika la Pan Africa Climate Justice Alliance, asema kuwa migogoro kama hizo zaweza kutabiriwa, na hivyo basi serikali inatakikana kujiandaa mapema ili kuepusha vifo.

Mithika asema kuwa anaona uchungu mwingi mno watu wanapoaga dunia, watoto wanapofanywa mayatima, na mali inapoharibika katika hali inyoweza kuepukika.

Hata hivyo, kuna dalili kuwa serikali mpya itaweza kushughulika. Naibu wa rais ametangaza kuwa serikali inatarajia kuunda sheria na mamlaka ya kushughulikia maafa nchini kupitia mswada utakaopendekezwa bungeni hivi karibuni.

Hadi sasa, Kenya haina sera rasmi ya kushughulikia maafa, jambo ambalo husababisha mwitikio duni yanapotokea.

Ruto asema kuwa, haifai kabisa Kenya kufumaniwa na maafa yanayoweza kutabirika.

Hata hivyo, Mithika Mwenda ana matumaini kwa sababu, tofauti na serikali zilizopita ambapo rais angechagua mtu yeyote kuongoza wizara ili kuridhisha urafiki ama uaminifu wa kisiasa, katiba mpya nchini imeundwa kukomesha matumizi hayo mabaya ya madaraka.

Mwenda asema kuwa mambo mengi yalienda mrama katika uongozi uliopita kwa sababu watu walijikuta na madaraka katika nyanja wasizozielewa vema.

Lakini, katiba mpya inahitaji rais kupendekeza waziri, kisha baadaye waweze kupelelezwa hadharani kwa kuonyeshwa katika runinga kabla ya kuapishwa. Wakati huo, Mkenya yeyote anaweza kupinga pendekezo la rais iwapo ana ushahidi wa kuridhisha kuonyesha kuwa aliyependekezwa hafai.

Hii ina maana kuwa, kwa mara ya kwanza katika historia ya Kenya, wizara huenda zikaongozwa na watu waliohitimu katika nyanja hizo.

John Kioli, ambaye ni mkurugenzi mkuu katika shirika la Green Africa Foundation asema kuwa Kenya yaweza kutatua shida zake za kimazingira iwapo kutakuwa na nia njema kisiasa.

Sehemu ya Budalangi magharibi mwa nchi ya Kenya, kwa mfano, imekumbwa na mafuriko ya kila mwaka kwa miaka mingi. Lakini kwa msukumo wa mbunge wa sehemu hiyo, serikali imeweza kukarabati lambo mbili katika miaka tano zilizopita. Na kwa mara ya kwanza kwa miongo miwili, wakaazi wa sehemu hiyo hawajatatizwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa iliyonyesha nchini hivi maajuzi.

Evans Kituyi, mkaazi wa Kenya ambaye ni mtaalam wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi  asema kuwa kuna matumaini kuwa serikali mpya itaweza kusukuma nchi hatua kadha mbele katika maswala ya sera za kimazingira, kupitia uongozi wa wizara mbalimbali.

Mtaalam huyo asema kuwa, kutokana na taaluma inayodhihirika katika miundomsingi za serikali, kuna uwezekano wa sera kutekelezwa, na pesa kutumika katika miradi zilizopendekezwa.

Muungano wa Jubilee, ambao ndio uliounga mkono kuchaguliwa kwa Rais Uhuru Kenyatta na kuunda serikali unapanga kuekeza katika kawi safi kuwezesha wakenya asilimia 70 walio mashambani kupokea nishati.

Ilivyoandikwa katika manifesto ya muungano huo, serikali inatarajia kusaidia kujenga viwanda vya nishati ya jua ambavyo vitamilikiwa pamoja na jamii, ili kuzalisha nguvu za umeme. Wanajamii wataweza kuuza umeme wa ziada kwa kampuni ya kusambaza nguvu za umeme nchini.

Hata hivyo, serikali iliyopita iliekeza pakubwa katika kusambaza nguvu za umeme mashambani kupitia msaada kutoka serikali ya Ufaranza. Ingawaje, bado watu wengi mashambani hawajapata huduma hiyo, huku wakilazimika kutumia kuni, dizeli na mafuta ya taa ambayo yana madhara katika mazingira.

Hivi sasa, Kenya inategemea umeme wa maji. Wakati maji yanapopungua mitoni, umeme huo hupungua, na hivyo basi, jenereta za dizeli hutumika kujaza uhaba huo.

Kama ahadi za serikali zitatimizwa, basi watu mashambani watapewa mikopo midogomidogo ili kununua vifaa vya kuzalisha umeme bila kudhuru mazingira. Mikopo hizo, kulingana na manifesto ya Jubilee zitaweza kulipwa kupitia mfumo wa kulipa bili ya umeme kwa kupitia simu za rununu.

Jambo lingine la kutizama ni juhudi za kurejesha hadhi ya msitu wa Mau ambao kwa sasa umewachwa wazi. Msitu huo huhifadhi maji mvua inaponyesha kisha kuyaachilia polepole kwa mwaka mzima

Katika siku za karibuni, Ruto amepingana wazi na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuhusu uhamishaji wa watu waliojenga katika msitu huo. Wengi walioadhirika ni watu kutoka jamii ya naibu huyo wa rais.

Mnamo mwezi wa Novemba, gazeti la Daily Nation ambalo ndilo linaongoza nchini Kenya lilimnakili Ruto akisema kuwa: “Tangu uhuru, Wakalenjin hawajawahi lala nje kwa baridi kama ilivyotendeka wakati walipofurushwa kutoka msitu wa Mau, ambapo waliishi kwa amani. Shida zao zilianza pale Waziri Mkuu pamoja na Waziri wa Ardhi James Orengo walipoidhinisha kufurushwa kwao.”

Tangu aapishwe kama naibu wa rais, Ruto hajawahi toa maoni kuhusu waliofurushwa kutoka msitu wa Mau. Lakini, Manifesto ya Jubilee inaahidi kuwa serikali itahakikisha kuwa wakimbizi wote wa ndani kwa ndani wamerudishwa makwao kisheria, na pia serikali itahakikisha watapata mahali pa kuishi kwa hesima.

Isaiah Esipisu ni mwandishi wa habari wa kujitegemea aliye na makao mjini Nairobi.

Topics
Climate Politics Adapting to Climate Change cor-gov Energy Extreme Weather Forests