LOIYANGALANI, Kenya, June 17 (Thomson Reuters Foundation) – Katika tamasha ya kitamaduni ya Ziwa la Turkana katika jimbo la Marsabit nchini Kenya, Mariam Lemuska amejizuia kusikiliza ngoma na nyimbo za jadi. Bali, anajifunza jinsi ya kuunda mkate wa Uhabeshi, ujulukanao kama injera.
Lemuska, mwenye umri wa miaka 39, ni mkaazi wa jamii ya wafugaji ambao chakula chao kikuu ni nyama, maziwa na damu. Lakini, hali ya ukame inayozidi kuharibika inachangia mno vifo vya wanyama hao. Hivyo basi, Lemuska kutoka jamii ya El Molo ako tayari kutafuta mbinu mbadala za kulisha familia yake.
Binti huyo asema kuwa wanyama wao hufa kwa wingi hali ya anga inavyoharibika zaidi, huku wakiachwa na njaa kubwa. Hivyo basi, ni sharti ajifunze njia zingine za kuishi.
Katika tamasha hii, anamtazama kwa makini afisa wa kilimo anavyoonyesha jinsi ya kupika vyakula mbadala ikiwemo mtama, maziwa, keki ya asali na chapati ya malenge.
Kila mwaka, jamii mbalimbali katika jimbo la Marsabit, ambalo ndilo kubwa zaidi nchini Kenya hukutana ili kusherehekea utamaduni wao. Lakini, mabadiliko ya tabianchi yanavyozidi kukithiri katika eneo hilo, mkutano huo kwa sasa unatumiwa kuonyesha mbinu mbali mabali za kukabiliana na hali hiyo ambayo inazidi kubadilika.
“Ni lazima tutumie fursa hii na idadi ya watu waliyo hapa, kwa sababu ni changamoto kubwa kuwafikia vijijini kutokana na ukubwa wa jimbo hili, barabara mbaya, na mtandao mbaya wa mawasiliano,” asema Guyo Galicha Iyya, mratibu wa hali ya ukame katika jimbo hilo.
Katika maonyesho hayo, maafisa wa serikali ya jimbo wanawashauri wakaazi kuzingatia kufuga mifugo kama vile mbuzi na kondoo badala ya ngombe, kwa sababu wanyama hao wadogowadogo hula chakula na maji kidogo, na pia wana uwezo wa kustahimili ukame.
Kwingineko, watu wanafunzwa jinsi ya kutega maji ya mvua, na jinsi ya kukuza mimea zinazostahimili hali ngumu ya ukame, zikiwemo zile zilizoundwa na taasisi ya utafiti wa kilimo na mifugo nchini Kenya.
Fatuma Shufkisho, afisa wa kilimo kutoka sehemu ya Saku katika jimbo la Marsabit asema kuwa kwa kutokana na hali ya anga inayozidi kubadilika, kuna haja ya wakaazi kuzingatia vyakula mbadala ili kujikimu kimaisha.
Tamasha hiyo ya siku tatu, ambayo hufanyika katika mji wa Loiyangalani, ilianzishwa na utawala wa mashinani mnamo mwaka wa 2008 kama njia ya kuhimiza usalama katika jamii za wafugaji katika jimbo hilo, pamoja na kusherehekea utamaduni.
Jamii ambazo huhudhuria tamasha hiyo ni pamoja na watu wa El Molo, Rendille, Samburu, Turkana, Dassanatch, Gabra, Borana, Konso, Sakuye, Garee, Waata, Burji na Somali.
Tamasha hiyo huzingatia nyimbo na kitamaduni. Lakini wingi wa watu katika sehemu ya maonyesho ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi ni ishara kuwa jambo hilo lina umuhimu katika sehemu hiyo.
Kawaida, asema Jonah Samana wa shirika la Hunger Safety Net Programme, kuwasiliana na watu katika jimbo hilo ni ndoto. Shirika hilo hutoa misaada za kifedha badala ya chakula katika maeneo kame nchini Kenya.
Marsabit ina idadi ya watu 300,000 walioenea katika kilomita 71,000 mraba. Ilhali jimbo la Mombasa, kwa kulinganishwa lina watu milioni moja walioenea katika kilomita 219 mraba (maili 85).
Samana asema kuwa, kila mara imebidi wategemee mashirika yasiyo ya kiserikali ama watu waliojitolea ili kuwasiliana na wakaazi vijijini.
Bwana huyo asema kuwa kupasha habari kwa jamii ni ngumu kwa sababu wakaazi hao ni watu wa kuhamahama.
Watu hao uhama kutafuta lishe bora ya mifugo wao, hivyo basi, kufanya vigumu kuwaleta pamoja kwa ushauri.
Umbali wa mwendo pia hufanya vigumu wakaazi kufikia afisi kuu ili kunufaika na masomo, asema Iyya.
Kwa mfano, ni kilomita 700 kutoka Ileret hadi Marsabit ukitumia barabara mbaya mno, kilomita 300 kutoka Loiyangalani kufika afisi kuu. Safari hiyo inagarimu shilingi elfu mbili mwendo mmoja. Hiyo ina maana kuwa, ndio mtu aende Marsabit na arudi, ni lazima auze mbuzi watatu.
Emanuel Lekulo, aliyetembea kilomita 10 kutoka El Molo ili kuhudhuria tamasha ya Loiyangalani asema kuwa bali na kujiburudisha na miziki za kitamaduni, amejifunza kuhusu magonjwa ambayo yamewasumbua mbuzi wake kwa muda mrefu, na jinsi ya kuwapa chanjo.
Mara nyingi, asema Lekulo, wakaazi hupoteza mifugo wao kwa magonjwa wasiyoyaelewa. Lakini siku hii, bwana huyo asema amepewa nambari ya simu ya afisa wa mifugo, ndipo aweze kumpigia simu kila anavyohitaji usaidizi.
Ilikuwa muhimu kwa bwana huyo kuhudhuria tamasha hiyo, kwani mbali na kujifurahisha, amejifunza memgi.