Na Kizito Makoye
DAR ES SALAAM (Thomson Reuters Foundation) – Mradi wa utunzaji mazingira ujulikanao kama REDD+ ulipokuja Tanzania mwaka 2008, ulileta ahadi za matumaini ya kupunguza ukataji miti hulela na madhara ya tabia nchi.
Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti mpya, pesa zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo tayari zimekwisha malizika, na kutishia hatima na juhudi za nchi hiyo ya Afrika Mashariki za kulinda misitu yake.
REDD+ (Mradi wa kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na ukataji holela wa misitu)ni mpango wa shirika la Umoja wa Mataifa unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuzisihi nchi zilizo endelea kuzilipa nchi maskini ili kulinda misitu inayohifadhi hewa ukaa.
Nchi tajiri hutoa motisha kwa kununua hisa ili kupunguza uzalishaji hewa ukaa na pesa hiyo hutumika kuifanya misitu ya kitropiki iendelee kusimama na kuhudumia jamii inayoizunguka.
Hata hivyo ripoti ijulikanayo kama REDDX(Matumizi ya REDD+) iliyochapishwa mwezi machi na shirika la Forest Trends, linalo fuatilia maendeleo ya misitu duniani, inasema kuwa ufadhili kwa mpango wa REDD+ nchini Tanzania umekwama bila ya fedha zozote kutolewa toka mwaka 2010.
Matokeo yake ni kwamba, ripoti hiyo inasema , miradi yote ya majaribio ya REDD+ Tanzania – pamoja na shughuli muhimu za uhifadhi misitu na matumizi bora ya ardhi imesimama.
“Ukosefu wa fedha za wahisani ni swala linaloleta wasiwasi mkubwa katika jitihada za kuendeleza REDD+ nchini Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.
Mradi huo ulivyokuja Tanzania kwa mara ya kwanza, Norway ndiyo ilikuwa mfadhili mkubwa , ikitoa dola millioni $80.2 au asilimia 85.5 ya fedha zote za REDD+ nchini, zitakazo lipwa ka awamu kwa kipindi cha miaka mitano.
Wafadhili wengine ni pamoja na Finland, Ujerumani, Uingereza, Ubelgiji, taasisi ya Rockefeller, Benki ya dunia, Umoja wa mataifa na Tanzania yenyewe.
Pesa hizo zilitumika kuandaa mpango mkakati wenye vipaombele 10, pamoja na kuziainisha na kupambana na sababu kuu za ukataji miti holela na upimaji usio shaka wa kiwango cha uchafuzi wa hewa ukaa.
Hata hivyo kwa mujibu wa ripoti hiyo, mtiririko wa pesa kutoka mpango wa hali ya hewa na misitu wa Norway, zilipungua kwa kiwango kikubwa toka mradi huo ulivyoanzishwa.
“Kufuatia upungufu wa fedha kutoka Norway zilizoanzisha mchakato wa REDD+ nchini Tanzania mwaka 2009, jitihada sasa simegonga mwamba”alisema Brian Schaap Mtafiti mwandamizi wa REDDX, katika taarifa yake.
Kuondoa hitilafu
Kuhusika kwa Norway kwenye mradi wa REDD+ nchini Tanzania pia ulipata dosari. Mwaka 2012, mradi huo ulikosolewa wakati shirika la World Wide Fund for Nature (WWF) lilikumbwa na kashfa ya rushwa iliyohusisha utafunwaji wa pesa za Norway takribani dola milioni 1.3 zilizo kuwa zimelengwa kwa mradi wa REDD+. Mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Stephen Mariki alikataa tuhuma hizo lakini baadae alijiuzuru.
Na kwa kuwa ni asilimia 18 tu ya pesa za REDD+ zinaenda serikalini, kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakosoaji wanasema kwamba pesa nyingi mno za walipakodi wa Norway zinaelekezwa kwenye mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi za elimu ya juu na hamna chochote kinachopelekwa kwenye kujenga uwezo.
Maeneo mengi nchini , wananchi maskini wamegeukia misitu kama ni chanzo cha kujipatia kipato, wanavuna miti na kuuza kama mkaa na mbali. Hiyo pia imechangia kuangamia kwa takribani heka 420000 za misitu kila mwaka , mwa mujibu wa taarifa ys shirika la chakula duniani FAO
Kwa sasa, miradi inayofadhiliwa na Norway imewafunza wenyeji 50,000 namna ya uhifadhi endelevu wa misitu, wakati mradi mwingine umeanzisha mpanga wa matumizi ardhi kwa ekari 82,754 za ardhi, ilisema taarifa hiyo ya REDDX. Jitihada hizo za REDD+pia zimesaidia kuanzisha uangalizi wa hewa ukaa katika aina saba za miti na kupunguza hewa ukaa kutokana na ukataji holela wa miti, ripoti hiyo ilisema.
Hata hivyo maofisa kutoka ubalozi wa Norway wangali wanatambua jitihada lizizofanywa naTanzania katika mradi wa REDD+ wakiongeza kwamba baadhi ya miradi tayari imeanza kurejesha mazingira katika hali yake ya awali.
Uwekezaji mkubwa
Kupungua kwa pesa kwenye mradi wa REDD+ kwa hakika na ishara ya mafanikio alisema
Kiwango cha pesa kilichotolewa kwa mwaka kimepungua na maendeleo ya miradi yameonekana mingi ikiwa tayari imekamilika, na kwa mantiki hiyo kiwango cha matumizi yam waka ni pungufu kuliko mwanzo mwa usharika huo,” alisema Berit Tvete ofisa anayehusika na mazingira na mabadiliko ya tabia nchi katika ubalozi wa Norway.
Baadhi ya miradi ya utafiti ya majaribio ilikamilika miaka miwili iliyopita, na zimetoa mafunzo mazuri na ufahamu mpya,” aliiambia Thomson Reuters Foundation kwa barua pepe.
Kwa mujibu wa Tvete, Ubalozi wa Norway ungali unatekeleza mpango wake wa awali, ulioongezwa muda mpaka mwaka 2016 kwa kuwa si pesa zote zilitumika . Kuna miradi miwili bado inaendelea na mwingine wa tatu ungali unaandikwa, aliongeza
Aliongeza kusema si kila mradi wa uhifadhi umedorora, baadhi yake imesha kamilika na ndiyo maana pesa zilizotengwa zimekwisha.
Na Norway inakusudia kutimiza ahadi yake iliyoitoa mwaka 2008 kuendelea kuisapoti miradi yote mpaka zitakapokamilika, Tvete aliongeza kusema. “Makusudio ya jitihada zilizopo ni kuiwezesha Tanzania kushiriki kwenye mpango wa malipo ya REDD+ yanayotokana na matokeo,” Tvete alisema.
Hata hivyo kuhusu mchango wa Norway , “hakuna mipango yoyote yenye uhakika itakayoleta pesa za ziada kuendeleza mradi wa REDD+,” alihimiza.
Faustine Ninga, mratibu wa miradi ya kijamii ya rasilimali katika shirika lisilo la kiserikali linalojulikana kama Tanzania Natural Resources Forum, hana shaka hata kidogo kuwa Norway huenda isitelekeze uwekezaji wake mkubwa nchini Tanzania ili kulinda misitu.
Amezungumzia mradi mwingine mkubwa Kituo cha uangalizi wa hewa ukaa, iliotengenezwa kupima na kuweka kumbukumbu ya hewa ukaa kwenye rasilimali za misitu nchini Tanzania, ikiwa ni moja ya sababu za Norway kuendelea kuweka milango ya ufadhili wazi. “Kwa kuwa huu ni mradi mkubwa hautakuwa na maana yoyote kuuacha uangamie,” alisema.
Hata hivyo bila ya ahadi zozote rasmi kutoka Norway, hatima ya miradi ya REDD+ nchini Tanzania ingali mashakani. Kwa sasa, kwa mujibu wa ripoti ya REDDX, Serikali ya Tanzania inafanya mazungumzo na benki ya dunia na kuomba takribani $3.5 kuimarisha miradi yake ya REDD+ na kuhakikisha kwamba kazi kubwa iliyofanyika mpaka sasa haipotei bure.
“Wahisani wasipo rejesha nia yao ya kufadhili miradi ya uhifadhi wa misitu nchini,jitihada zote zilizofanywa awali zitapotea,” alisema Schapp, Mtafiti mwandamizi wa REDDX.
(Imeandaliwa na Kizito Makoye; uhariri Jumana Farouky na Megan Rowling. Tafadhali nukuu Thomson Reuters Foundation, shirika la hisani la Thomson Reuters, linalohusika na habari za majanga ya binadamu, haki za wanawake, biashara ya binadamu nyumba na mabadiliko ya tabia nchi. Tutembelee www.news.trust.org)