Na Isaiah Esipisu

NAIROBI, Agosti 29 (Thomson Reuters Foundation) – Aina za mpunga chotara zilizobuniwa kwa mara ya kwanza katika Afrika Chini ya Sahara zina mavuno mara nne zaidi ya aina zingine zilizoboreshwa, wasema wanasayansi, ambao wanatumia teknolojia ya mtandao kubaini mazingira bora ili kuongeza mazao.

Aina hizo 15 ambazo zimekuzwa nchini Kenya na Tanzania, pia zinastahimili magonjwa fulani na mazingira ya joto yanayopatikana magharibi mwa Kenya katika maeneo ya ziwa, na sehemu za pwani.

Wakulima katika maeneo hayo wamekuwa wakitegemea mbegu chotara za mpunga kutoka nchi za nje haswa kutoka Asia, ambazo wakati mwingine hukosa uzoefu wa mazingira ya maeneo ya Afrika Chini ya Sahara.

Wakati hali ya hewa inavyozidi kubadilika, na ardhi ya kilimo inavyozidi kudidimia kutokana na shinikizo la idadi ya watu, wataalam wasema kuwa kuna haja ya kutumia mbinu bunifu ili kuzalisha chakula.

Ukosefu wa chakula barani Afrika unatarajiwa kuongezeka hadi tani milioni 60 ifikapo mwaka wa 2020, iwapo hatua mwafaka hazitachukuliwa. Hayo ni kwa mujibu shirika la Alliance for a Green Revolution in Africa (AGRA).

Joe DeVries, Mkurugenzi wa Mipango ya kuimarisha mfumo wa mbegu barani Afrika katika AGRA asema kuwa mazao katika bara hili ni madogo mno kutokana na ukweli kuwa wakulima wana uwezo mdogo wa kupata mbegu zilizoboreshwa.

Mwanasayansi huyo alisema kuwa wakulima wengi hupanda mbegu zilizobuniwa zaidi ya miaka 30 zilizipita.

Denis Ketere, mkurugenzi mkuu wa shirika la African Agricultural Technology Foundation (AATF), ambalo lilibuni mbegu hizo chotara kwa kushirikiana na uma na sekta ya kibinafsi alisema kuwa, teknolojia ya kubuni mbegu chotara ndio iliboresha uzalishaji wa mpunga kule Asia, haswa Uchina.

Uzalishaji wa zao hilo barani Asia uliongezeka kutoka wastani tani 1.89 kwa kila hekari moja mnamo mwaka wa 1949 hadi tani 6.71 kwa hekari mnamo mwaka wa 2012.

“Kwa kutumia teknolojia kama hii”, asema Kayode Sanni, meneja wa mradi wa mpunga katika shirika la AATF, “tunatazamia kuona Afrika ikiweza kulisha Afrika. Mnamo mwaka wa 2014”, asema mwanasayansi huyo, “bara la Afrika liliagiza tani milioni 12 za mchele kutoka Asia.”

Shirika la AATF, likishirikiana na kampuni ya kibinafsi ya Hybrids East Africa Limited.Limebuni mbegu  za mpunga chotara zipatazo aina 140, kwa kutumia mimea zenya asili ya Afrika.

Miongoni mwa mbegu hizo, 15 bora zaidi ambazo huzaa tani 7 hadi 10 kwa hekari moja zimewasilishwa kwa shirika la kuchunguza afya ya mimea yani Kenya Plant Health Inspectorate Service (KEPHIS) ili zifanyiwe majaribio kote nchini.

Kampuni moja kutoka Amerika ijulikanayo kama aWhere Inc ambayo ni mshirika wa mradi wa kubuni mpunga chotara imeunda kifaa kitumiacho mtandao ambacho huwawezesha wanasayansi kujua sehemu bora za kuzalisha mbegu kwa wingi huku wakifaidika kwa kuelewa sehemu zilizo na mazingira bora zaidi.

Aina za mpunga zilizoboreshwa kama vile New Rice for Africa (Nerica) tayari zinatumika katika mashamba barani Afrika.

Katika mbinu hii ya uboreshaji, mbegu aina mbili huzalishwa kwa njia ya uchavushaji mtambuka, kisha mbegu inayopatikana inazidi kuzalishwa kwa kutumia mbinu ya uchavushaji wa kibinafsi mara kadha hadi wakati mbegu bora zaidi itakavyopatikana.

Mbegu hiyo bora basi, ina uwezo wa kuzidi kuzaa mbegu zingine kupitia uchavushaji wa kibinafsi kwa sababu maua yake yana sehemu za kiume na zile za kike.

Kuzalisha mbegu chotara, mimea tofauti za asilia huzalishwa tofauti kwa kutumia uchavushaji mtambuka, kisha mimea za mbegu zinazopatikana pia kuzalishwa kwa njia ya uchavushaji mtambuka ili kupata mbegu chotara. Mbegu hii chotara ina mazao mengi kuliko zile mbegu asili. Utaratibu huo hurudiwa kila wakati ili kupata mbegu chotara.

Hivi sasa, mavuno kutokana na mbegu za mpunga zilizoboreshwa katika Afrika chini ya Sahara ni takriban tani 2.3 katika kila hekari. Lakini, aina kadha za mbegu chotara zimeweza kuzalisha kati ya tani saba na 10 katika kila hekari, asema Sanni. Mazao hayo ni bora zaidi kuliko walivyotarajia  wanasayansi.

Sanni, asema kuwa hayo ni mafanikio makubwa.

Tatizo moja ni kuwa mbegu zinazotokana na mimea chotara haziwezi tumika kama mbegu tena, kwani ule uwezo wa kutoa mazao bora zaidi hupotea kutokana na maumbile yake.

Hilo lina maana kuwa haiwezekani wakulima kuhifadhi mbegu zinazotokana na mazao hayo, bali, wanahitajika kutegemea kampuni za mbegu kuzalisha mbegu chotara kila msimu wa upanzi.

Hili limekuwa tatizo, haswa kwa wakulima maskini wasioweza kumudu bei ya juu ya mbegu chotara,  asema John Mann, mkurugenzi mkuu wa Afritec Seeds Ltd, kampuni ambayo imefanya majaribio ya mbegu chotara zaidi ya mia moja, chini ya AATF.

Lakini kupitia mradi huu, asema bwana huyo, kuna mbinu bunifu, ya kusaidia wakulima wasiojiweza, hivi kwamba wanaweza kukopa mbegu, na kisha walipe baada ya kuvuna.

Ingawa wakulima watalazimika kununua mbegu kila msimu wa upanzi, faida ya juu inayotokana na mbegu chotara inatarajiwa kuwa juu zaidi ya gharama hiyo ya mbegu, asema Sanni.

Mbali na Misri, ambayo imekuwa ikizalisha mpunga chotara kwa kiwango cha juu kwa zaidi ya muongo mmoja, hakuna nchi nyingine kote barani Afrika ambayo imefaulu kuzalisha mbegu chotara asili.

Wakulima wa Misri wamezidisha mazao ya mpunga nchini humo hadi tani 10 kwa kila hekari moja, huku wakijipatia sifa kutoka kwa mashirika, miongoni mwao Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni la Umoja wa Mataifa.

Wakulima ambao wameshiriki katika majaribio ya mbegu hizo katika Afrika ya Mashariki wanasubiri kwa hamu kusikia kuwa mbegu hizo zimehalalishwa kwa matumizi, pengine baada ya miezi kadhaa wakati shirika la KEPHIS litakapokamilisha uchunguzi wake unaochukua misimu miwili.

Charles Wawo, mwenyekiti wa Ahero Irrigation Scheme Multi-Purpose Co-operative Society kule Kisumu asema kuwa wanachama tayari wametenga pesa za kununua mbegu hizo mpya.

Kenya na Tanzania zitakuwa nchi za kwanza kabisa kufaidika na upanzi wa aina hizo za mpunga chotara. Baada ya hapo, majaribio yataanzishwa kote Afrika ya Mashariki, Magharibi na Kusini, asema Sanni.

Topics
Climate Technology Adapting to Climate Change fod-env fod-gen fod-hun hum-hun