Nishati ya jua kwa kadi yaleta kawi safi kwa maskini nchini Kenya

by Isaiah Esipisu | @Andebes | Thomson Reuters Foundation
Thursday, 20 June 2013 20:45 GMT

Home systems paid by installment plan win a major clean energy award

KITALE, Kenya (Thomson Reuters Foundation) – Katika soko ya Sibanga, kadri kilomita 10 kutoka mji wa Kitale Magaribi ya Kenya, Timothy Nyongesa aingia katika duka la wagawaji la Mibawa kununua kifaa anachotumai kitatoa mwangaza kwa elimu ya watoto wake, na afya ya jamii yake.

Kwa kulipa malipo ya mwanzo ya shilingi elfu moja, Nyongesa anajipatia kifaa kitakachozaa kawi kwa matumzi nyumbani mwake. Kisha anarukia baiskeli na kuelekea kijiji cha Sinyerere, kilomita sita kutoka sokoni.

Familia ya Nyongesa ni mojawapo ya familia 3,000 katika sehemu ya Kitale ambapo tangu mwaka wa 2011, wanatumia nishati ya jua badala ya mafuta ya taa ili kuangaza nyumba zao.

Bwana huyo asema kuwa kamwe hawezi kuwaruhusu watoto wake kuitumia koroboi kusoma, wakati ambapo wale wa jirani wanatumia nishati ya jua.

Vifaa hivyo vya nishati ya jua vinatarajiwa kuinua matumizi ya nishati ya jua miongoni mwa maskini nchini Kenya, katika mtindo unaowezesha maskini wengi kumudu shilingi elfu kumi. Baada ya kulipa malipo ya mwanzo ya shilingi elfu moja, mteja anatakiwa kuendelea kulipa shilingi 120 kila baada ya wiki moja. Baada ya malipo 80 ya shilingi 120, mteja hupata haki ya kumiliki kifaa hicho.

Kadi zilizo na nambari ya kanuni iliyofichwa huwezesha wateja kutoa malipo kiusalama kutoka manyumbani mwao kwa njia ya ujumbe mfupi wakitumia simu za rununu.

Ubunifu wa Azuri Technologies ambayo ni kampuni ya Uingereza iliyobuni kifaa hicho kijulikanacho kama IndiGo, imejishindia tuzo la Ashden.  Ashden inajulikana kote ulimwenguni kwa kutuza ubunifu wa kawi safi katika kupunguza umaskini na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Simon Bransfield-Garth, ambaye ndio afisa mkuu wa Azuri alisema kuwa ni jambo la ajabu kuona jinsi watu walivyo na hamu ya IndiGo. Asema afisa huyo, kampuni ya Azuri itaongeza usambazaji wa vifaa hivyo ili kufikia wateja wengi zaidi.

Katika ujumbe wakati wa kuzindua ripoti mpya kuhusu nishati mbadala, Achim Steiner, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa kwa Mazingira alisema kuwa, matumizi ya nishati mbadala inazidi kunawiri kote ulimwenguni. Hivyo basi, inabidi makampuni na jamii kutumia mbinu hizo ili kupunguza uenezaji wa hewa chafu, haswa ile ya kaboni.

Hata hivyo, nia ya Nyongesa kutumia nishati ya jua ni kwa sababu ya afya ya wanawe, wala sio kitu kingine.

Wataalam wa afya wasema kuwa taa za mikebe hutoa moshi ulio hatari kwa binadamu. Nyongesa asema kuwa tayari, watoto wake wanalalamikia kuumwa na macho, hali ambayo anahisi inatokana kwa kutumia koroboi.

Bwana huyo mwenye miaka 51, na wake watatu anakwepa kutoa hesabu kamili ya watoto wake. (Tuseme ni 15), lakini anasema 11 ni wanafunzi. Kila baada ya shule, hao hutumia koroboi kwa masomo ya nyumbani kwa muda wa masaa mawili kila siku.

Mafuta ya taa pia yana madhara kwa mazingara. Kulingana na hesabu ya British Air Transport Association, tani moja ya mafuta ya taa ikichomwa, inatoa tani 3.15 ya hewa aina ya kaboni, ambayo imelaumiwa pakubwa kwa kuongeza joto ulimwenguni. Joto hilo limesababisha mabadiliko ya tabia nchi.

Hata hivyo, utafiti wa hivi maajuzi uliofanywa na chuo cha National Institute of Health unakisia kuwa zaidi ya familia milioni mia tano kote ulimwenguni bado wanatumia mafuta ya taa. Kila mwaka, familia hizo hutumia mafuta kiasi cha lita bilioni 7.6.

Hiki kifaa alichokinunua Nyongesa ni cha pili katika familia yake, kwa muda wa miezi mitatu. Cha kwanza alimpa mkewe wa kwanza.

Kifaa hicho cha IndiGo kina paneli inayoweza kutoa wati tatu, betri, taa mbili, sinia ya simu, na kamba za kuunganisha.

Kifaa hicho kimeundwa kufaidi maskini, haswa barani Africa. Mbali na Kenya, vifaa vya IndiGo vinauzwa kule Malawi, Sudan ya Kusini na Zambia.

Hata hivyo, duka la Mibawa ndilo la kipekee linalosambaza vifaa hivyo nchini Kenya, asema Mamasaka.

Walakini, mfanyibiashara huyo asema kuwa tayari amegundua wafanyibiashara wengine watano Magharibi ya Kenya na anatazamia kuwasambazia vifaa hivyo hivi karibuni.

Ingawa kuchanga shilingi mia moja ishirini kila wiki ni kazi ngumu kwa wakaazi maskini, wengi wanapendelea malipo hayo ikilinganishwa na bei ghali ya mafuta ya taa. Cha muhimu ni kuwa, baada ya kukamilisha malipo, basi mteja anapata fursa ya kukimiliki kifaa hicho.

Kwa wale ambao hawajiwezi kabisa, Namasaka huwapa muda zaidi, kama mwezi mmoja kutafuta hizo pesa.

Emanuel Siboe, anayetumia IndiGo asema kuwa kifaa hicho kimeleta ‘ukombozi’.

Mbali na shilingi mia moja alizozitumia kila siku kununua mafuta ya taa, Siboe alilazimika kutembea hadi madukani ili kuchaji simu yake ya rununu kwa shilingi ishirini mara tatu kwa wiki.

Akiongeza malipo ya kuchaji simu ya mkewe na mwanawe, basi alihitajika kulipa shilingi 180 kila wiki.

Lakini akiwa na kifaa hicho cha kuzalisha nishati ya jua, anapata huduma hizo zote bila malipo.

Isaiah Esipisu ni mwandishi wa habari maalumu kwa kuripoti kilimo na mazingira. Anaweza kupatikana kupitia esipisus@yahoo.com

 

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.