×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Wakulima wadogo watumia mitandao ya kijamii kukabiliana na mabadiliko ya hali anga

by Caleb Kemboi | Thomson Reuters Foundation
Tuesday, 16 July 2013 10:00 GMT

Mkulima Julius Cheruiyot atumia simu yake ya rununu kupata ushauri kuhusu kukumbatia mabadiliko ya hali ya anga. THOMSON REUTERS FOUNDATION/ Caleb Kemboi

Image Caption and Rights Information

Using their smart phones, farmers in Kenya’s Rift Valley are accessing advice on raising crops able to stand up to changing weather patterns

ELDORET, Kenya (Thomson Reuters Foundation) — Julius Cheruiyot alianza ukulima akiwa na umri wa miaka kumi na sita.

Alilazimika kuacha shule kutokana na ukosefu wa karo ya shule. Alifanya kazi kwa shamba la babake katika kaunti ya Uasin Gishu, eneo la bonde la ufa nchini Kenya.

Cheruiyot ana umri wa miaka 32. Yeye ni baba ya watoto watatu. Ukulima umemwezesha kusomesha na kulisha familia yake.

Hata hivyo wakulima wadogo wadogo wanaendelea kuathirika pakubwa kutokana na ongezeko la mabadiliko ya hali ya anga nchini Kenya.  Jambo hili limemfanya Cheruiyot kujiunga na wakulima wengine ambao wanatumia mitandao ya kijamii kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga.

Cheruiyot amesimama kwenye shamba lake la ekari tano. Anatoa simu yake na kufungua mtandao wa facebook kwenye ukurasa wa Young Volunteer for Enviroment ili kujifahamisha habari za punde kuhusu mazingira na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali anga.

“Mitandao ya kijamii…imetusaidia sana”,na taarifa tunayoipokea, sasa  tunaweza kujua wakati mwafaka wa kupanda, kwa sababu wakati mwingine tumegundua tunapata hasara wakati wa majira ya  mvua fupi na mvua nyingi  tusipochukua hatua mwafaka”.

Kubadilika kwa hali ya anga katika miaka ya hivi karibuni kumeathiri wakulima wengi nchini Kenya na maeneo mengine ya mashariki mwa bara Afrika.

Cheruiyot anasema kwa muda wa takriban miaka kumi iliyopita, ameshuhudia mabadiliko makubwa ya hali ya anga. Kuanzia kwa msimu wa mvua chache majira ya upanzi au msimu wa mvua nyingi majira ya mavuno. Mabadiliko haya yamechangia kwa mapato duni au ukosefu wa mazao kabisa.

Alipata kufahamu kuhusu kikundi cha Young Volunteers for the Environment katika maonyesho ya kilimo.

“Niliamua kujiunga na kikundi hiki, na tangia wakati huo nimejifunza mengi kuhusuiana na mabadiliko ya hali ya anga na jinsi ya kukabiliana nayo kama mkulima mdogo”, akaeleza.

Shirika la YVE Afrika nchini Kenya ni tawi la shirika la Pan African lililobuniwa mwaka wa 2011 nchini Togo. Shirika hili linaelezea wasiwasi kwa kiwango cha uzalishaji katika sekta ya kilimo, hatua inayochangia uhaba wa chakula na umaskini katika eneo hilo. Lengo lao hasa ni kuwasaidia wakulima wadogo kuelewa njia bora za kuendeleza kilimo ili kuongeza mapato.

YVE inahusisha vijana kote nchini kushiriki katika maswala yanayohusu mazingira na kuchangia kwa manufaa bora kwa jamii ili kuiwezesha kukabiliana vilivyo na mabadiliko ya hali ya anga.” Haya ni kwa mujibu wa rais wa shirika hilo Emanuel Serem.

KUKABILIANA NA ONGEZEKO LA JOTO.

Shirika la YVE lina wanachama kumi. Lengo la shirika hili lililoko eneo la Bonde la Ufa ni kuhamasisha uma kuhusu  mabadiliko ya hali ya anga na jinsi ya  kukabiliana na ongezeko la hali ya joto. Eneo hilo linatambuilka kama ghala la taifa nchini Kenya. Wanachama wake walipata mafunzo kwa kuhudhuria mikutano na warsha zilizoandaliwa na mashirika ya mazingira.

Kikundi hiki kina zaidi ya wafuasi 900 katika mtandao wa facebook ambao wanapata habari kutoka kwa tovuti na kufanya majadiliano  kuhusu kilimo.

Utumizi  wa mitandao ya kijamii miongoni mwa vijana nchini Kenya unakua kwa kasi. Wengi wainatumia kama njia ya kutangamana, YVE inaitumia kuwafikia wakulima wadogo.

“Mabadiliko ya hali ya anga ya hivi maajuzi yameathiri wakulima wa nafaka katika maeneo ya bonde la ufa. Wengi hawafahamu kinachoendelea”. Asema Ken Ruto Kiongozi wa Northrift Theatre Ambassadors. Shirika hili pia linatumia mitandao ya kijamii kuhamamsisha vijana kuhusu maswala ya uhifadhi wa mazingira.

“Kupitia mitandao ya kijamii tumeweza kuwaelimisha wakulima wadogo wadogo  kupanda miti mashambani mwao kama njia bora ya kukabiliana na mabadiliko ya hali anga.” Alidokeza Ruto ambaye kikundi chake kiko mjini Eldoret kaunti ya Uasin Gishu.

Eneo la bonde la ufa linajulikana kwa upanzi wa mahindi na ukuzaji wa mifugo wa maziwa. Hata hivyo, upanzi wa mahindi kila mwaka umekumbwa na changamoto kutokana na uhaba wa mvua, pia mkurupuko wa maradhi yanayosababishwa na wadudu kama vile Maize Lethal Necrosis ambayo yaliathiri mazao katika maeneo ya bonde la ufa, Septemba 2012 na kuenea kote nchini.

Kutokana na kubadilika kwa hali ya anga YVE linawashauri wakulima kupanda aina ya mimea inayofaa kulingana na msimu wa wakati huo. Miongoni mwa mazao yanayopendekezwa kutokana na uwezo wa kukabiliana na kubadilika kwa hali ya anga ni mtama, ngano, viazi na wimbi. Kikundi hiki kinaeleza kuwa kubadilisha upanzi wa mimea shambani kunasaidia udongo kupunguza makali ya kemikali na kuboresha rotuba yake.

“Tumekuwa tukipanda mahindi tangia wakati wa ukoloni na hii imeathiri uzalishaji”, alisema mkulima Cosmas Biwott. Kufuatia ushauri wa YVE amegeuza na kupanda viazi, amefurahia matokeo yake. “Inakua vizuri na natarajia mavuno tele”, alisema, huku akicheka.

Kwa mujibu wa Rais wa YVE, wakulima wana haja ya kupata habari kuhusu kubadilika kwa hali ya anga. Serem anasema baadhi ya wakulima wanaamini kuwa kupungua kwa mazao shambani ni laana inayotokana na machafuko ya ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 yaliyokumba sehemu ya nchi, ikiwa ni pamoja na mkoa wa bonde la ufa.

Serem anahoji kuwa ameridhika na jinsi  wakulima wanavyopokea juhudi za shirika hilo.

CHANGAMOTO YA KUTOFAHAMU NA KUAFIKIA HABARI MUHIMU.

“Wakulima wadogo wadogo wanatoa maoni na kuuliza maswali zaidi”, alisema. Lakini anakiri kuwa huduma ya YVE hazipatikani kwa kila mtu. Wakulima wengi  ambao hupata huduma wanatumia simu inayopokea mtandao wa internet. Lakini wakulima ambao wanaishi mashinani hupata ugumu kufikia mtandao na sio wote ambao wanaelewa kutumia mtandao ya kijamii.

Cosmas Biwott ni mmoja wa wakulima wadogo eneo la bonde la ufa ambao wanatumia huduma wa mtandao ya kijamii. Anaonya kuwa kiwango cha kutojua kusoma na kuandika ni cha juu.

 

“Mitandao ya Kijamii imetusaidia sisi...kupata habari zaidi kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya hali ya anga, lakini wakulima wengi hawajui kutumia simu au hata kusoma habari”, alisema. “Hiyo ni changamoto kubwa.”

Biwott anahoji kuwa wakulima wanaweza faidika kutokana na kituo cha habari kilicho na vifaa bora vya mawasiliano pamoja na mtandao.

Serem anasema YVE  inatarajia kufungua ofisi katika kila kaunti eneo la Bonde la ufa ili kufikia wakulima kupitia vikao na maonyesho ya kilimo.

 “Kati ya watu kumi, nane ni wakulima katika mkoa wa bonde la ufa”, akasema. “Kwa hiyo tunahitaji kukumbatia umoja kwa minajili ya kuwepo kwa uwezo wa kupata chakula cha kutosha nchini”.

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->