BAGAMOYO, Tanzania (Thomson Reuters Foundation)–Ali Shaaban wala hakushangaa kukuta bango kubwa likiwa limesimikwa ndani ya shamba lake likibeba ujumbe unaomuonya asijihusishe na shughuli zozote za kilimo kwenye eneo hilo.
Wiki chache zilizopita mkulima huyo mwenye umri wa miaka 56 aliwaona wazungungu asiowajua wakivinjari na magari yao aina ya 4X4 kijijini kwake wilaya ya Bagamoyo, takribani kilomita 70 kutoka jiji la Kibiashara la Dar es Salaam.
Mzee huyu pia alisikia tangazo kwenye Radio yake ya kizamani likionya watu wanaoishi ndani ya shamba la Razaba kuondoka mara moja.
Licha ya kuwa wameishi hapo kwa miaka mingi, Shaabani anakabiliwa na tishio la kuondolewa, wakati serikali ikijiandaa kuhamisha mamia ya kaya zinazoishi eneo hilo ili wampishe mwekezaji wa shamba la miwa.
“Huu ni mtihani mkubwa maishani mwangu” alisema. “Katika umri huu wapi duniani naweza kwenda na familia yangu? Sioni mahala popote watoto wangu wanapoweza kupaita nyumbani”
Wakulima mkoa wa Pwani nchini Tanzania wanapinga kile wanachokiona kuwa na ushirika mwovu wa serikali na wavamizi wanaopora ardhi ya kijiji ili kuanzisha miradi ya mazao ya nishati yaani biofuel.
Wilayani Bagamoyo, wakulima wanadai Kampuni ya Uswidi ya EcoEnergy imepora ardhi hekari 5000 ya kijiji ilatayo baada ya kushawishi wanakijiji kuwajengea shule, hospitali na ahadi ya nafasi za kazi.
EcoEnergy inakusudia kujenga mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji wa ethanol huko Razaba, ikikadiria kuzalisha tani 125,000 za sukari Megawatt 100,000 za umeme na lita million 25 za ethanol kila mwaka.
Katika tovuti yake EcoEnergy imeandika kuwa ardhi inayogombaniwa ni josho la ng’ombe lililotelekezwa—lilitumika kati ya mwaka 1976 na 1993—hata hivyo Razaba kuna zaidi ya familia 600 zingali zikiishi.
“Tumekuwa tukiishi humu tangu mwaka wa 1950,” alisema Ali Ngwega, mmoja wa viongozi wa kijiji huko Bagamoyo.” Sasa serikali inatufanya kuonekana kama wavamizi ili kulinda maslahi ya mwekezaji”
Hata hivyo Mkurugenzi wa EcoEnergy, Anders Bergfors, atupilia mbali tuhuma za uporaji ardhi akidai kwamba kampuni yake imefuata taratibu zote za umiliki wa ardhi hiyo.
Bergfors alinukuliwa akisema kuwa kampuni yake inakusudia kuweka mikataba na wakulima wadogo wanaoishi pembezoni mwa shamba hilo ili wawe wabia katika uzalishaji wa sukari.
“Tungependa waanzishe vikundi vidogo vidogo ikiwa ni takribani ekari 100 kwa kila mshiriki, tutakuwa na mikataba ya kisheria.”
Kwa mujibu wa Bergfors, mradi huo ni muhimu sana kwani unaongeza uzalishaji wa sukari nchini, pamoja na umeme sawia na uzalishaji wa eethanol inayoweza kutumika kama nishati mbadala.
Begfors alisema mradi wa Razaba huenda ukazalisha ajira kwa watu 2000, na kwa kupitia mpango wa wazalishaji wanje zaidi ya watu 1500 wataajiriwa ukiachilia mbali ajira zisizo rasmi zitakazofika 15,000
Kupoteza hakiardhi
Hata hivyo serikali inashikilia msimamo kuwa kuishi kwenye eneo hilo kwa muda mrefu si kigezo cha kuwa wamiliki halali wa ardhi husika.
“Sheria iko wazi, muwekezaji ndiye mmiliki halali wa eneo hilo” alisema Anna Tibaijuka, Waziri wa ardhi na makazi.
Hati rasmi za Ardhi ni ngumu kupata Tanzania, kutokana na urasimu na rushwa. Wakati ardhi ya kijiji haipaswi kuuzwa kwa wageni, ukosefu wa maandishi inamaana kwamba wanakijiji wanapoteza uthibitisho.
Kwa mujibu wa Kituo Cha Uwekezaji Tanzania, mchakato wa upatikanaji ardhi unamtaka muwekezaji kukabidhi maombi yake kwa baraza la kijiji husika kupitia viongozi wa wilaya. Mkutano wa kijiji ndipo utaitwa ili kujadili wazo hilo na endapo kipande cha ardhi kitadhibitiswa kuchukuliwa na mwekezaji, umiliki wa ardhi husika unahamishiwa serikalini, na serikali ina mamlaka ya kukodisha ardhi husika hadi miaka 99.
Tatizo ni kwamba, “ardhi ya kijiji ikishahamishiwa serikalini, wanakijiji wanapoteza haki zao zote za umilili mpaka mwisho wa mkataba wa upangaji,” alisema Abdi Kagomba, meneja afisa wa mawala ya kisheria wa Tanzani Investment Centre.
Kwa Kipindi cha miaka michache sasa migogoro ya ardhi baina ya wenyeji na wawekezaji imesababisha makampuni lukuli kusitisha mipango yao ya uwekezaji wilayani Bagamoyo na Rufiji Mkoani Pwani.
Kituo cha Uwekezaji kinasema, kuna zaidi ya makampuni 40 yaliyoonyesha kupenda kupata ardhi kwa ajili ya mazao ya nishati Tanzania. Kwa sasa ekari 436,000 zimetengwa kwa uzalishaji wa mazao ya nishati.
Upatikanaji wa ardhi na rasilimali virahisi nchini Tanzania umevutia sana wawekezaji, baadhi yao wameshawishiwa na serikali, wataalam wanasema.
Kote duniani, madhara ya mabadiliko ya tabia nchi na upungufu wa nishati yamelazimu nchi nyingi kuanzisha sera zinazopendelea matumizi ya nishati mbadala. Na wakati mkutano wa nchi tajiri zaidi duniani 2012 G8 ulishuhudia kuanzishwa kwa mpango mpya wa usalama wa chakula an lishe, unaohimiza sekta binafsi kuwekeza kwenye kilimo. Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzo kuwekeza.
Hapo Awali.
Hata hivyo kwa kuwa matamanio ya umiliki ardhi yangali yanazidi, wakulima wa Bagamoyo na Rufiji wameambulia kuwa wahanga wa uporaji ardhi.
Utafiti wa Juni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Mazingira cha Sweden unaoitwa “Biofuel production and its impact on local livelihoods in Tanzania,” unaonyesha kuwa tabia ya serikali kukumbatia wawekezaji imedhoofisha uwezo wa wenyeji kulinda maslahi yao.
Licha ya kuwa Sheria za Tanzania zinaelekeza kampuni kuomba ardhi kupitia kituo cha uwekezaji, utafiti huo unaonyesha mazingira ambapo wawekezaji binafsi wamekwepa sheria na kufanya makubaliano na wenyeji ili wawape ardhi.
“Katika baadhi ya kesi, makubaliano kati ya wawekezaji na wenyeji yalifanyika kwa mdomo, hata hivyo wenyeji walichukulia kuwa tayari ile ilikuwa ni mikataba” wakati wawekezaji walijua imeafika bila ya maandishi hawakuwa na wajibu wa kutekeleza ahadi yoyote ile.
Utafiti huo unasema mipango mingi ya ununuzi wa ardhi umegubikwa na mizozo kwa kuwa wawekezaji wanaonekana kutotekeleza ahadi wanazozitoa kwa wenyeji.
Hata kama ardhi imenunuliwa kisheria, Utafiki unaonyesha kwamba wakulima ambao ardhi zao zimo ndani ya mpango wa uwekezaji, kwa mara nyingi hawana nguvu ya kudai serikali katika kufidia jinsi inavyostahili.
Kwa wakulima wanaopinga mpango wa serikali na EcoEnergy. Tafiti hii inatoa matumaini
“Wakulima wamefanikiwa kwenye baadhi ya maeneo kuwafukuza wawekezaji pindi wanapoona haki zao zinakandamizwa, hata pale makubaliano yanapokuwa yamefanyika,” watafiti wamesema.
Na hivyo ndivyo wakulima wa Razaba wanapanga kufanya.
“Tutafanya tuwezalo kutetea haki zetu” alisema mkulima Hidaya Mwinyijuma.
Kizito Makoye ni mwandishi Mwandamizi aliyepo Dar es Salaam amebobea kwenye uandishi wa habari za mazingira na utawala bora.