MAIMAHIU, Kenya, Jan 19 (Thomson Reuters Foundation) – Sio wanawake wengi huwekeza katika biashara za nishati safi nchini Kenya. Lakini vifo vya kuku vilimgeuza  mfugaji kuku Lydia Waithera kuwa mwekezaji katika sekta hiyo.

Waithera alipoteza kuku wengi kutokana na baridi wakati wa usiku na akaanza kutafuta mbinu ya kuzuia ndege wake kuathirika na baridi hiyo.  Mwanzoni, alianza kutumia makaa ya kawaida lakini makaa hayo yakasababisha ndege wengi kufa kutokana na sumu ya monoksidi kaboni.

Lakini, kutokana na ushauri wa wakulima wenzake, aligeukia makaa ya kutengezwa, almaaruhu  briquettes. Makaa hayo yanatengezwa kutoka kwa mabaki yanayopatikana kwenye uzalishaji wa sukari viwandani, vumbi inayotoka kwa makaa na pia mchanga. Matumizi ya makaa hayo yalimpunguzia mzigo wa kuongeza makaa kwenye majiko ndani ya nyumba za kuku kwani yanadumu muda mrefu ikilinganishwa na makaa ya kawaida.

Katika muda wa miaka miwili, mahitaji yake ya makaa hayo yalifikia gunia 200. Hii ilichangia atafakari mbinu ya kupunguza gharama ili kuokoa fedha.
Miaka minne baadaye, baada ya kupokea mafunzo ya biashara na mkopo, yeye huzalisha tani moja ya makaa hayo kila siku, na amewaajiri watu wanne. Aliwekeza kiasi cha $ 1,200 kwenye biashara hiyo na thamani yake sasa ni $ 18,000. “Niligundua kuwa ni mradi wa faida kubwa na sijawahi kuangalia nyuma,” alisema.

Ukosefu wa mitaji na ujuzi kuhusu uzalishaji wa kawi  safi  miongoni mwa wanawake wa Kenya hadi sasa umechangia wanaume kudhibiti kwa kina kikubwa biashara ya nishati mbadala nchini humu. Hata hivyo, polepole, wanawake wameanza kukabiliana na changamoto hiyo. 

MAARIFA MAPYA

Ili kuafikia ndoto yake ya kumiliki kampuni ya kutengeza makaa hayo, Waithera alianza kushirikiana na shirika la Global Village Energy Partnership (GVEP), ambalo linalenga kuongeza upatikanaji wa nishati katika nchi zinazoendelea.

Shirika hilo lilimsaidia kwa ustadi kupata ujuzi wa ujasiriamali aliohitaji kuendesha kampuni. “Sikuwa na ujuzi wa kuweka kumbukumbu za matumizi ya fedha,”  alisema Waithera. “Lakini kupitia mafunzo ya kina nimeweza kupata ujuzi huo.”

Mnamo mwaka 2014, shirika la GVEP pia lilimsaidia Waithera kupata mkopo wa

 $3500 kutoka taasisi za fedha ili kupanua biashara yake.  “Sasa lengo langu ni kuzalisha tani 3.5 za briquettes kila siku na kuajiri wafanyakazi sita,” alisema.

 

Licha ya kupokea mafunzo kuhusu unakili wa kumbukumbu za matumizi ya fedha   na ujuzi, Waithera hata hivyo, angali anakabiliwa na upinzani kwenye jitihada za kuimarisha biashara yake kutokana na mitizamo nchini Kenya kwamba  biashara ya nishati mbadala sio ya wanawake.

“Nilipokuwa nikiangalia mashine za kununua, wauzaji walidhani nimetumwa na mtu mwingine na wakauliza niwajuze ‘mmiliki’ ili wamweleze jinsi ya kutumia mashine hizo,” alisema. “Lakini hali inabadilika.”

Hata hivyo, alisema, taasisi za fedha bado zinasita kuwakopesha fedha wawekezaji wa kike au kutambua kuwa sekta hiyo inaweza kunawiri na kuwapa faida wawekezaji.   

Kuna matatizo mengine pia ikiwa ni pamoja na ukosefu wa wafanyakazi wenye uzoefu na pia kiwango duni cha mashine zilizotengenezwa nchini. “Mashine njema hutoka nje na ni za gharama kubwa,” alisema.

Waithera alisema masuala haya yote yanaweza kushughulikiwa iwapo vyuo vikuu na taasisi za utafiti wa kiufundi zitashirikiana na wajasiriamali wa sekta ya nishati mbadala, ili kukuza utoaji mafunzo katika teknolojia ya nishati safi, hasa miongoni mwa wanawake. Hali hiyo itaimarisha sekta ya nishati endelevu huku pia ikiboresha ubora wa bidhaa zake, alisema.

Sammy Kitula, mratibu wa utoaji wa mtaji wa shirika la GVEP, anakubaliana na Waithera “Ni jambo la kusikitisha kwamba vyuo vikuu vichache tu nchini Kenya ambavyo vinatilia maanani mafunzo kuhusu nishati mbadala.  Kupitia teknolojia sahihi na mafunzo, wanawake wajasiriamali zaidi wanaweza kujiunga na sekta hiyo.”

 

WANAWAKE  WASHIRIKI BIASHARA

Wanawake tayari wanatekeleza baadhi ya majukumu muhimu katika sekta ya nishati mbadala nchini Kenya. Huku wengi wa wabunifu na mafundi wakiwa wanaume, wanawake kwa kiasi kikubwa ndio hufanya kazi ya kuuza bidhaa na utengezaji wa baadhi ya viungo au vipuri muhimu kama vile vigae vya kuweka ndani ya majiko ya kuni ya kizazi kipya.

Kitula alisema mashirika kadhaa yasiyokuwa ya kiserikali yanawaongoza wanawake katika biashara ya nishati safi kupitia mafunzo, kubuni  mitandao na kupata fedha.

Alisema shirika lake huwaunganisha wanawake wanaowekeza katika sekta ya nishati ya kijani na taasisi za fedha kwa kutoa dhamana ya mkopo na kuuliza taasisi hizo kuwatoza riba ya chini. Nayo Wizara ya Nishati inaendesha mpango wa kutoa mafunzo kwa wanawake katika vituo vyake vya nishati yake, alisema.

Kulingana na Kitula, juhudi hizo sasa zimeanza kuzaa matunda kwani kuna ongezeko la idadi ya wanawake wanaotaka mafunzo na kutafuta mtaji wa kuanzisha biashara katika sekta ya nishati mbadala.

Waithera anawahimiza wanawake wa Kenya kunyakua fursa ambayo imeletwa na nishati safi akisema watapata faida kubwa.
“Soko ni kubwa. Ni vigumu kutimiza mahitaji ya wateja,” alisema.

 

(Taarifa ya Justus Wanzala, Mhariri ni  Laurie Goering)

 

 

Topics
Energy Women's rights