DAR ES SALAAM, Tanzania (Thomson Reuters Foundation)—Katika hali ya tishio la hali mbaya ya hewa, bunge la Tanzania limepitisha sheria kusaidia mamlaka za serikali kukabiliana na dharura na kuwakinga watu na hatari za majanga.

Sheria hiyo mpya, ambayo inajaribu kuziba nyufa na mapungufu ya uwezo wa nchi kukabiliana na majanga asili na yale yanayosababishwa na binadamu, inaanzisha shirika jipya litakalokuwa na jukumu la kukabiliana na majanga.

Shirika la Kudhibiti Majanga (DMA) litakuwa na kazi ya kuangalia na kukinga athari za mafuriko, ukame, mvua za mawe, dhoruba na njaa, pamoja na kuhifadhi vifaa muhimu vya kusaidia wahanga wa majanga.

Tanzania inazidi kuwa hatarini kukumbwa na mafuriko, ukame na dhoruba za kitropikali ambazo zimeathiri maisha ya watu na shughuli zao za kiuchumi, kuvunja miundo mbinu na kusababisha upungufu wa chakula na matatizo ya afya. Kasi ya utokeaji wa majanga hayo, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa mataifa, umeleta athari kubwa kwa jamii husika na kudhoofisha uwezo wa nchi kusaidia wahanga.

Jenister Mhagama, Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu anayeshughulikia uratibu wa sera amesema sheria hiyo mpya itaboresha zaidi uwezo wa serikali kukabiliana na majanga.

“Tutakuwa na mfumo madhubuti wa tahadhari katika ngazi za mkoa na wilaya ili mamlaka husika ziweze kujiandaa na kukabili athari za majanga kwa haraka zaidi.”

Kwa mujibu wa waziri, shirika hilo litakuwa na nguvu za kuamuru uokoaji wa watu kwenye maeneo hatari kupiga marufuku, au kuzuia matumizi, au uuzaji wa pombe, silaha na vitu vingine kwenye maeneo ya majanga.

Kwa mujibu wa serikali, wahalifu wamekuwa wakipata fursa ya kuiba au kupora vitu muhimu wakati wa majanga kiasi cha kuzuia wahanga wa majanga kupata stahili zao. Sheria mpya itakabiliana na tatizo hilo.

Sheria hiyo pia inaanzisha mfuko maalumu utakaokusanya pesa za kusaidia shughuli mbalimbali za majanga.

Kwa sasa, shughuli za kukabiliana na majanga zinafanywa na idara maalum chini ya ofisi ya waziri mkuu. Hata hivyo, utafiti uliofanywa na shirika la umoja wa mataifa miaka mitatu iliyopita, inaonyesha udhaifu mkubwa kwenye mikakati ya kukinga na kukabiliana na majanga.

Udhaifu huo ni pamoja na kushindwa kutenga maeneo ambapo maji ya mafuriko yanaweza kupelekwa, au kuanzisha teknolojia ya kisasa kuzuia mafuriko kama vile kujenga kingo maalumu za mafuriko.

“Moja ya vitu tunavyotaka kufanya ni kuzipa mamlaka za mikoa nguvu kukabiliana na dharura mbalimbali ili watu waweze kuzifikia huduma muhimu majanga yanapotokea,” Mhagama alisema.

Chini ya sheria mpya, kamati za mikoa na wilaya zilizo chini ya shirika zitakuwa na nguvu kuamuru uhamishwaji wa watu, au kutumia rasilimali fedha na watu zilizopo kuchukua hatua za tahadhari, kuliko kusubiri maelekezo kutoka ngazi za juu.

Hatua za tahadhari zilizoainishwa kwenye sera mpya ni pamoja na kuanzisha mipango madhubuti ya mawasiliano, mafunzo, kuimarisha mahitaji wakati wa dharula kama vile mahema na chakula, na kuhakikisha hatua za tahadhari, makazi ya dharura pamoja na shughuli za uokoaji zinafanyika.

Wapinzani hata hivyo wanatilia shaka kama hatua zinazopendekezwa zitatosha kukabiliana na majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa kama vile dhoruba iliyoua watu 47 na kuwaacha wengine 5000 bila makazi huko Mkoani Shinyanga mwezi uliopita baada ya nyumba zao kuharibiwa na kufunikwa na mafuriko.

“Siamini kama tumefikia viwango vinavyohitajika kuepusha athari zinazoweza kusababishwa na majanga. Taasisi zetu bado ni dhaifu sana kiutendaji na ujuzi, na hazina rasilimali,” alisema James Mbatia, mbunge na mtaalam wa majanga katika kipindi cha television.

Katika mahojiano na Thomson Reuters Foundation, Masozi Nyirenda, mtaalam wa majanga anayefanya kazi na Mamlaka ya Elimu Tanzania alisema sera mpya itafanya kazi tu kama itabadilisha utaratibu uliopo na kuifanya Tanzania iwe makini zaidi kukabiliana na majanga.

“Kwa ujumla, huwa tunasubiri mpaka janga limetokea kabla ya kuchukua hatua, na hatuchukui hatua haraka iwezekanavyo kuokoa maisha na mali,” alisema.

Nyirenda alisema kitengo cha maafa kama vile idara ya zimamoto na polisi wanapata bajeti finyu sana kuwawezesha kukabiliana na matukio yanayozidi ya majanga.

“Vitengo vyetu vya maafa havina vifaa maalum kusaidia kukabiliana na majanga. Vifaa vya zimamoto vyote vimepitwa na wakati, kuna magari machache ya wagonjwa, boti, chopa, kwa kiwango kikubwa, vimesababisha vifo na uharibifu wa mali,” Nyirenda alisema.

Kwa mujibu wa Nyirenda, ukosefu wa mfumo mzuri wa mipango miji umesababisha nyumba nyingi zijengwe kwenye maeneo hatari.

“Mfumo wa mipango miji ambao ungeweza kusaidia jitihada mbalimbali za kuepusha majanga ni dhaifu mno. Kwenye maeneo mengi, nyumba zimesongamana kiasi kwamba wakati wa majanga jitihada za uokozi zinakuwa ngumu sana. Majanga kama moto, mafuriko au mlipuko wa magonjwa yanaweza kuongezeka sana katika maeneo hayo.”

Topics
Climate Politics Adapting to Climate Change Extreme Weather hum-nat