×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Wakulima kukosa maji huku mitambo ya kuzalisha umeme wa maji nchini Tanzania ikikauka

by Kizito Makoye | Thomson Reuters Foundation
Friday, 26 June 2015 11:11 GMT

Dugout fishing canoes sit on the banks of the Mtera reservoir in southern Tanzania. TRF/Zuberi Mussa

Image Caption and Rights Information

Move to protect hydropower reservoirs would limit access by other users, including farmers and fishermen

DAR ES SALAAM, Tanzania Juni 26 (Thomson Reuters Foundation) —  Tanzania, nchi yenye vivutio kama Mlima Kilimanjaro na mbuga ya wanyama ya Serengeti, ina desturi ya kulinda ardhi kwa ajili ya ikolojia na uzuri wa nchi.

Kwa sasa, nchi hii ina sababu mpya kuongezea kwenye orodha ya maeneo yaliyohifadhiwa: Umeme.

Ikiwa inakumbwa na ukame unaoathiri uzalishaji wa umeme wa maji wakati ambapo kumekuwa na ongezeko la hitaji yaw a umeme,  serikali ya Tanzania inapanga kuazimia vyanzo vya maji vya Mtera na Kidatu vilivyopo kusini mwa nchi hiyo kuwa maeneo yanayohifadhiwa.

Mpango huo tata utazuia shughuli zote za uzalishaji mali —ikiwemo kilimo cha umwagiliaji kufanyika kwenye maeneo ya mabwawa ya maji na vyanzo vingine vilivyoorodheshwa.

Ni jaribio la kuondoa ushindani wa maji ambao wenye dhamana wanasema unaathiri uzalishaji wa umeme.

Hata hivyo, wakulima wanasema mpango huo utavuruga shughuli za kilimo, ufugaji, uvuvi na njia nyingine za kutafuta riziki kwenye eneo hilo.

“Nimekuwa nikilima kwenye eneo hili maisha yangu yote,” alisema Eliudi Samizi kutoka Kijiji cha Kisimani mkoani Dodoma, ni miongoni mwa wakulima 8000 wa mpunga watakaofukuzwa kutoka kwenye kingo za mto Ruaha Mkuu.

“Kama mtu akiniambia kuacha kuvua au kulima nitafanya shughuli gani kulisha familia yangu.”

Umeme wa nguvu ya maji, unaochangia takribani asilimia 57 ya umeme wote unaoingizwa kwenye gridi ya taifa, umekuwa ukiathiriwa sana na upungufu wa maji kutokana na ukame wa mara kwa mara.

Hata hivyo, ongezeko la shughuli za binadamu kama vile kilimo cha umwagiliaji, uvuvi na ufugaji zimechangia ukubwa wa tatizo, kwa mujibu wa shirika la ugavi wa umeme TANESCO.

Mpango wa serikali kuzuia matumizi ya maji Mtera na Kidatu umekuja mapema  baada ya TANESCO kuomba ridhaa kuondoa watu wanaofanya shughuli pembezoni mwa mitambo yao, ambao kwa mujibu wa kampuni hiyo, wanaharibu vyanzo vya maji pembezoni mwa mitambo, na kuiacha ikiwa na maji machache ya kuzungushia mashine hizo.

Mbogo Futakamba, katibu mkuu wa wizara ya maji amesema mitambo ya Mtera na Kidatu ni miongoni mwa maeneo 153 nchini iliyoainishwa kwa lengo la kulindwa kulingana na sera ya maji ya taifa, inayotilia mkazo ulindwaji wa vyanzo vya maji vilivyo hatarini.

“Tumekwisha ainisha vyanzo kadhaa vya maji vilivyo hatarini kuharibiwa,” aliiambia Thomson Reuters Foundation kwa njia ya simu kutoka Dodoma. “Tunasubiri tu taratibu za kisheria ndipo tutavitangaza vyanzo hivyo kuwa maeneo tengefu.”

Kwa mujibu wa wakulima, Serikali tayari imekuwa ikizuia shughuli za kilimo kwenye maeneo kadhaa ya Iringa na Morogoro, ambayo ni wazalishaji wakubwa wa chakula, ili kusaidiwa kuongeza mtiririko wa maji kuendesha mitambo ya umeme.

Pendekezo hili jipya litafanya zuo hilo kuwa la kudumu.

Hata hivyo, wakulima na wafugaji wanadai kwamba hawatendewi haki. Adui mkubwa anayenyonya maji mtoni, ni mabadiliko ya tabia nchi.

“Sidhani kwamba kufukuza wakulima wasifanye umwagiliaji litakuwa suluhisho la kudumu kwa kuwa hamna maji ya kutosha mtoni kujaza mabwawa hayo,” alisema Damas John, mfugaji maeneo ya Kidatu.

Wachambuzi wa mambo wanakubali, wakisema iwapo serikali haitaweka mikakati ya kukabiliana na tishio la mabadiliko ya tabia nchi, kama vile kuweka mpango wa uvunaji wa maji ya mvua au kujenga mabwawa madogo madogo kuhifadhi maji ya ziada wakati wa mvua, uzalishaji wa umeme hautaimarika.

“Mabwawa madogo yataweza kuhifadhi maji ili kutoa sapoti kwa bwawa kubwa katika miezi ya ukame,” alisema Ladislaus Chang’a mkurugenzi wa utafiti na hali ya hewa wa Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania. “Maji yaliyohifadhiwa huenda yakatumia kujazia mabwawa na kuzuia kima cha maji kisishuke sana.”

 

UMEME AU CHAKULA?

Bwawa la Mtera, ni bwawa kubwa lililokuchimbwa lililopo kwenye mto Ruaha kwenye mpaka wa Dodoma na Iringa, linafanya kazi ya kutunza maji kwa ajili ya bwawa dogo la kuzalishia umeme la Kidatu.

Kulingana na kima cha maji, bwawa la Mtera huongezeka ukubwa na kufikia takribani kilometa za mraba 150 na 600 (maili 58 hadi 230).

 Kwa mujibu wa Justus Mtolera, meneja wa Bwawa la uzalishaji umeme la Kidatu, upungufu mkubwa wa maji mara nyingi husababishwa na matumizi ya maji kwa shughuli za kilimo nyanda za juu, ufugaji na wanyama pori. Upungufu huo husababisha matatizo kwenye uzalishaji umeme.

Huku akikubali kwamba ni muhimu kwa serikali kuendeleza shughuli za umwagiliaji, Mtolera anaona umeme wa maji ni injini ya maendeleo ya kiuchumi unaopaswa kupewa kipaumbele.

“Serikali lazima iingilie kati kuepuka mgao wa umeme usio wa lazima utakao athiri shughuli za uchumi” alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wataalam wanasema hatua ya serikali kulinda maslahi yake kwenye umeme wa maji inaathiri watu wake.

Mtaalam wa haki ardhi Yefred Mnyenzi amesema serikali imekuwa ikishindwa kuweka uwiano kati ya kulinda maslahi ya watu wake na kuendeleza mipango ya kibiashara. Mpango mpya wa kulinda vyanzo vya maji kwenye mitambo ya umeme, amesema, ni mfano mmoja wa serikali kutoa kipaumbele kwenye viwanda huku ikifanya maisha ya wakulima masikini na wafugaji kuwa magumu sana.

“Hali ya baadaye kwa wakulima wadogo wadogo haijulikani kwa kuwa haki zao kupata na kutumia rasilimali maji zinakanyagwa na wawekezaji wakubwa,” Mnyenzi aliwaka. “Ni muda muafaka sasa kwa watunga sera kutilia maanani na kusikia kilio cha wakulima maskini wanaohitaji maji na ardhi kwa maisha yao ya kila siku.”

(Imeandikwa na Kizito Makoye; imehaririwa na Laurie Goering; Tafadhali nukuu Thomson Reuters Foundation, tawi la hisani la Thomson Reuters, inayoandika habari za majanga yanayokabili wanadamu, haki za wanawake, biashara ya binadamu na rushwa.tembelea www.trust.org/climate)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->