×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Ndege zisizo na rubani zasaidia jamii kutathmini athari za mafuriko Dar es Salaam

by Kizito Makoye | @kizmakoye | Thomson Reuters Foundation
Wednesday, 4 January 2017 07:00 GMT

Community members map out flood risks in Tandale neighbourhood, Dar es Salaam. TRF/Kizito Makoye

Image Caption and Rights Information

With almost 70 percent of its inhabitants living in informal settlements, Dar es Salaam is highly vulnerable to flooding

TANDALE, Tanzania, Januari 4 (Thomson Reuters Foundation) —Taswira ya ndege ndogo isiyo na rubani inayoelea angani kwenye mitaa ya Tandale kutathmini eneo lenye watu wengi linaloathiriwa na mafuriko mara kwa mara ilizua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo hilo waliochoshwa kabisa na mafuriko ya mara kwa mara.

“Ninafurahi kuona kwamba hatua zinachukuliwa kudhibiti mafuriko, alisema Happy Malimbo, mkazi wa eneo hilo mwenye umri wa miaka 35.

Kwa kusaidiwa na ndege hizo zisizo na rubani, mamlaka za jiji wanaandaa mpango kulinda na kusaidia wakaazi wa maeneo yanayoathiriwa na mafuriko, kama vile Tandale, na kutoa mwanya wa matumaini kwa wakaazi hao.

Tangu mwaka 2013, halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imekuwa ikishirikiana na Benki ya dunia na wadau wengine, wakiwemo Shirika la Msalaba Mwekundu, na shirikisho la Open Geospatial kupima barabara, mifereji na madimbwi ya maji ya mafuriko kutumia ndege zisizo na rubani.

Ukiitwa Ramani Huria, mradi huo unalenga kusaidia jamii kwenye maeneo ya msongamano kutengeneza ramani sahihi za maeneo yao, ambazo zaweza kutumika kupunguza hatari ya mafuriko na kusaidia jitihada za uokozi, maofisa wa jiji wamesema.

Mafuriko huja kila mwaka Tandale, moja ya maeneo yenye makaazi holela jijini Dar, hata hivyo ukosefu wa mikakati ya kukinga mafuriko ina maana kwamba mafuriko ya asili husababisha janga kuu.

Wenyeji wanasema wamekuwa wakipata hasara kila mara kutokana na mafuriko, yanayowaacha mamia bila ya makazi.

“Nilipoteza mali yangu nyingi, nyumba yangu ilivyozingirwa na mafuriko mwezi Aprili mwaka jana,” alisema Malimbo, Mwenye watoto watatu.

Ikiwa zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wake wakiishi kwenye makazi holela, Dar es Salaam, jiji kubwa nchini Tanzania liko katika hatari kubwa ya mafuriko, hasa kwenye maeneo ya msongamano kama Tandale.

Mvua kubwa hunyesha mara mbili kila mwaka, mara nyingi  ikisababisha mafuriko makubwa yanayowalazimu maelfu ya watu wahame nyumba zao na kusababisha hasara ya maelfu ya dola za marekani.

Dar es Salaam's informal settlements are vulnerable to flooding when heavy rain swells rivers. TRF/Kizito Makoye

USHIRIKA WA JAMII

Juliana Letara, Mkuu wa kitengo cha mipango miji cha wilaya ya Kinondoni, amesema mradi wa Ramani Huria umewafundisha wanafunzi wa chuo kikuu na wenyeji kutambua na kuyapima maeneo yaliyo hatarini kukumbwa na mafuriko, kuziwezesha mamlaka za jiji kuchukua hatua inayostahili kwa wakati.

Tarafa nyingi huko Tandale, Wilaya ya Kinondoni, zimepimwa na kuandaliwa mpango wa dharura wa mafuriko, na mpango wa ustahimilivu wa jamii unaoanzisha njia za kujiokoa.

“Kama ukijua maeneo yanayoathiriwa na mafuriko, unaweza ukaweka miundombinu kuepusha athari kwa raia,” Alisema Letara kwa Thomson Reuters Foundation.

Uzalishaji wa takwimu changanuzi na kwa kushirikiana na mradi tofauti wa shirika la Msalaba mwekundu kudhibiti mafuriko, imesaidia kuanzisha vikundi vidogo vidogo vinavyo weka mpango wa dharura wa mafuriko kwenye maeneo 10 yanayokumbwa na majanga kila mara.

“Michoro ya Ramani Huria ni rahisi kutumia na zinaweza kutumiwa na mtu mwenye elimu yoyote,” alisema Letara. “Jamii inajisikia hali ya umiliki wa ramani hizo maana ilishiriki kuziandaa.”

“Kwa sasa tuna ramani, na ramani ni kitu cha muhimu sana kuanza nayo,”alisema Diwani wa kata ya Tandale Osigili Lossai. “Tunaweza kutambua maeneo mbalimbali ya kuyatafutia ufumbuzi. Ni dira inayotuongoza kuweka mipango mipya na kujipanga sisi wenyewe tukishirikiana na jamii.”

Maofisa wa Tandale pia wanatumia ramani hizo kutambua maeneo ambayo mafuriko husababisha magonjwa ya mlipuko.

“Ramani hizi zinatusaidia kutambua nyumba zenye wagonjwa wa kipindupindu na kuandaa mpango wa kukabiliana,” alisema Lossai.

A woman carries a drone that is helping flood-prone Dar es Salaam suburbs map out flood risks. TRF/Kizito Makoye

TEKNOLOJIA NAFUU

Ndege zisizo na rubani zinapiga picha nzuri zinazotumika kutengeneza ramani na mpango wa kukabiliana na mafuriko.

Frederick Mbuya, Mshauri Mtaalam wa Benki ya Dunia anayefanya kazi na Tume ya Sayansi na Teknolojia, amesema Ndege hizo ni teknolojia mahususi ya kufanya usanifu wa anga kwa upimaji ardhi.

“Matumizi ya ndege hizi ni rahisi sana kuliko njia nyingine za asili zinazotumika kupiga picha.” Alieleza Thomson Reuters Foundation.

 Ofisa wa wilaya ya Kinondoni Letara alisema ndege hizo zinaweza pia kupima maeneo yasiyoweza kupitika wakati wa mafuriko, na kuhimiza umuhimu mkubwa wa kutumia teknolojia hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa Benki ya dunia Loy Nabeta, taarifa mbalimbali zinazochukuliwa kwenye maeneo yanayokabiliwa na mafuriko jijini Dar, inajumuisha watu milioni 1.3, imewekwa kwenye tovuti maalumu inayoweza kufikiwa na mtu yoyote.

Wataalam wanasema watu wengi wanaoishi kwenye maeneo yenye mafuriko hawana la kufanya kwa kuwa ni maskini, hata kama wanajua maisha yao na mali yao iko hatarini.

Kwa kuwa msimu wa mvua haudumu sana, wakazi wa mabondeni wako tayari kuishi na hatari ya mafuriko, na muda mfupi husahau taabu iliyowakumba, alisema mkazi wa Tandale, Salum Kiponda.

Hata hivyo, Ramani huria inaweza kubadilisha mtazamo kwamba mafuriko ni jambo linaloweza kuvumilika.

“Mara nyingi hatujui ni lini mafuriko yatakuja, na nini cha kufanya, hata hivyo taarifa hii mpya inatupa mwanga wa kujua na kujikinga kabla ya hatari haijatukumba,” Alisema Malimbo.

(Imeandikwa na Kizito Makoye; Mhariri Megan Rowling. Tafadhali nukuu Thomson Reuters Foundation, tawi la hisani la shirika la Thomson Reuters linaloandika habari za majanga, haki za wanawake, biashara haramu ya binadamu na mabadiliko ya Tabia nchi Tembelea http;//news.trust.org

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->