×

Our award-winning reporting has moved

Context provides news and analysis on three of the world’s most critical issues:

climate change, the impact of technology on society, and inclusive economies.

Kisima kitumiacho nishati ya jua chawalinda watoto wa wafugaji nchini Kenya huku ukame ukizidi

by Isaiah Esipisu | @Andebes | Thomson Reuters Foundation
Wednesday, 8 February 2017 08:57 GMT

A herders' borehole is helping protect the lives of thousands of children and animals as a new drought hits

JIMBO LA TURKANA, Kenya, Feb 8 (Thomson Reuters Foundation) – Kisima kilichochimbwa na wafugaji katika juhudi za kustahimili kiangazi sasa kimebadilika kuwa tegemeo kwa maelfu ya watoto na mifugo huku msimu mwingine wa kiangazi ukibisha hodi. Hayo yamewezekana kutokana na matumizi ya pampu itumiayo nishati ya jua na matangi ya kuhifadhi maji.

Kisima hicho kimekuwa kama chemichemi jangwani, katika eneo hilo kame lililo katika Afrika ya Mashariki, ambapo mashirika ya misaada husema kuwa ukame mtawalia unahatarisha maisha ya mamilioni ya watoto.

Kisima hicho ambacho kilichimbwa kwa mathumuni ya kuwasaidia wafugaji 12, sasa kimeimarishwa hivi kwamba kinatoa maji kwa maelfu ya mifugo na watu wanaoishi chini ya Mlima Pelekech, eneo la Lokore, katika jimbo la Turkana.

Hivi sasa, wachungaji wa mifugo wanaweza rudisha mifugo wao nyumbani kila siku ili wanywe maji, jambo ambalo wanasema ni baraka kwao.

Jacinta Akiru mwenye miaka 65 na watoto 5 asema kuwa kwa kawaida, huwa ni tatizo kubwa mifugo zinapopelekwa mbali na nyumbani kutafuta malisho na maji kwani watoto wao hutegemea kunywa maziwa ili kuishi. Na kama hakuna maziwa, inamaanisha kifo kwao.

Mwezi uliopita, Shirika la msalaba mwekundu lilitabiri kuwa nambari ya Wakenya watakaokosa chakula huenda ikaongezeka maradufu ifikapo mwezi wa Aprili hadi watu milioni 2.4 kutoka watu milioni 1.3, haswa katika sehemu za kaskasini mwa nchi na maeneo ya pwani.

Mwanzo kabisa, baada ya kuchimba kisima, wafugaji walichota maji kwa kutumia ndoo na kamba, ambapo wangechota kiasi kidogo sana kwa matumizi ya nyumbani.

Tulipoanza mradi huu, ilikuwa katika juhudi za kupata angalau maji kidogo ya matumizi ya nyumbani, asema Angeline Namudang, ambaye ndiye muwekahazina wa Lokore Community Disaster Management Committee, ambacho ndicho kikundi kilichochimba kisima.

Mbeleni, wafugaji hao walikuwa wanaishi majuma kadhaa, na hata miezi malishoni mbali na manyumbani mwao wakitafuta malisho haswa wakati wa ukame. Wanaporudi, walikuwa wanapata aidha afya ya watoto waliowaacha nyuma imedhoofika, na hata wengine kufariki dunia.

Hayo yalibadilika wakati pampu itumiayo nishati ya jua ilipowekwa mnamo mwaka wa 2013, kwa msaada wa shirika la kimataifa lijulikanalo kama Veterinaries Sans Frontiers Germany.

Kisima hicho sasa kinasukuma maji hadi vioski katika vijiji viwili, na pia mabwawa mawili kwa matumizi ya mifugo.

Huu ni kama wokovu kwetu, asema Lotit Agirai, mume wa bibi sita na baba wa watoto 30.

Bwana huyo mwenye miaka takribani 70 asema kuwa kufikia maji ya matumizi ya nyumbani na hata mifugo ndilo jambo bora zaidi lililomtendekea maishani.

Mwana huyo alikuwa akitembea pamoja na mifugo wake umbali wa kilomita 30 hadi eneo la Karamoja nchini Uganda akitafuta maji na malisho.

Kufikia sasa, nyumba 625 zinatumia kituo hicho cha maji. Kila nyumba ina takriban watu saba, na kila nyumba ina wanyama wapatao 150 wakiwemo mbuzi, kondoo, ngamia na punda.

Kila nyumba hulipa shilingi 300 za Kenya kila mwezi, ambapo malipo ya shilingi mia moja ni ya kuchota maji kwa matumizi ya nyumbani, na shilingi 200 ni kwa matumizi ya mifugo.

Pesa hizo hutumiwa kwa kutengeneza mitambo hizo zinapoharibika, na kwa kulipa walinzi wawili ambao hulinda kisima hicho usiku na mchana.

Kisima hicho hakijakauka, na bado kinatoa maji licha ya kiangazi kikuu, ambacho wataalamu wa mambo ya mazingira wanasema kinaweza kulinganishwa tu na kile cha mwaka wa 2011.

Kuwa na maji, pia inamaana kutakuwa na visa vichache vya magonjwa yatokanayo na maji kama vile kuhara, kuhara damu na homa ya matumbo, asema Purity Ndumbi, muuguzi mkuu katika kituo cha afya cha Waso, huko Isiolo, Jimbo lililo kaskazini mashariki mwa nchi, ambayo vilevile ni sehemu kame.

Kunapokuwa na ukame, magonjwa kama hayo huzidi, muuguzi huyo aliambia shirika la Thomson Reuters Foundation.

Hilo pia hutendeka kwa mifugo, kulingana na Johnson Wamalwa, afisa mkuu wa mifugo jimbo ndogo la Turkana ya magharibi.

Wakati kama huo, wanyama wengi kutoka sehemu mbalimbali hutumia bwawa moja kukunywa maji, jambo ambalo linarahisisha usambazaji wa magonjwa, asema afisa huyo.

Hivi sasa, maelfu ya mifugo zimekufa kaskazini mwa jimbo hilo kutokana na magonjwa yasababishwayo na kiangazi, kuchoka kutokana na miendo mirefu, na hata kukosa malisho.

Kati ya mwezi wa Desemba na Januari, zaidi ya mbuzi na kondoo wapatao 6000 walikufa kutokana na ugonjwa wa goat plaque katika jimbo ndogo la Laisamis, Jimbo la Marsabit kaskazini mashariki mwa nchi, kulingana na Michael Baariu, afisa wa mifugo katika eneo hilo.

Ugonjwa huo unatokana na virusi hatari vya kuambikizana na husababisha kifo kwa mbuzi na kondoo.

Hata hivyo, wakaazi wa Lokore wako na usalama, kwani hawajapoteza mifugo zao tangu mwanzo wa kiangazi kilichoanza katika mwezi wa Juni mwaka uliopita.

Tunatarajia pia watoto wetu watabakia na afya njema hadi mwisho wa msimu wa kiangazi, asema Akiru.

(Tafadhali pigia debe Thomson Reuters Foundation, mkono hisani wa Thomson Reuters, unaoripoti hali ya misaada, haki za wanawake, ulanguzi, haki za mali, na mabadiliko ya hali ya hewa. Tembelea http://news.trust.org/climate)

Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.

-->