HAI, Tanzania (Thomson Reuters Foundation)—Peter Chuwa kwa mda mrefu amekuwa akimwagia maji shamba lake la mpunga kwa kutumia mfereji unaochota maji mtoni. Siku hizi, hata hivyo, maji ni machache, na uzalishaji mpunga kwa njia hii sio endelevu.
Kipindi cha ukame miaka miwili iliyopita, na maji mengi yaliyokuwa yakimsaidia kuua magugu kwenye shamba lake na kumhakikishia mavuno bora licha ya mvua hafifu yalikauka, kiasi cha kuathiri mavuno na kipato chake.
“Nilikosa amani kabisa kwa kuwa mazao yalikauka kabla hata msimu wa mavuno,” alisema. “Inafikia hatua nakosa hata chakula cha kulisha familia yangu,” Chuwa alisema.
Kwa sasa, hata hivyo, mfumo wa umwagiliaji kwa njia ya matone, ulioanzishwa kusaidia wakulima kukabiliana na ukame, umesaidia kurejesha mavuno yake, na kumfanya awe imara zaidi kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuokoa muda, anasema.
“Unafungua koki tu na kuacha mtambo utiririshe maji kwenye mizizi, kinyume na mfumo wa kawaida unaotumia muda mwingi sana na nguvu,” alisema.
Akiwa katika shinikizo la ukame, mkulima huyo mwenye umri wa miaka 65 katika kijiji cha Kikavu Chini, Wilaya ya Hai, mkoa wa Kilimanjaro, ameamua kuzalisha mazao yanayohitaji maji machache, kama vile mbogamboga, mahindi, viazi na maharage. Mfumo wa matone, unaotumia maji machache sana umekua mkombozi kwani unamudu kuzalisha mazao hayo, alisema.
Chini ya mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na Catholic Relief Services—Shirika kubwa la maendeleo duniani, wakulima kijiji cha Kikavu Chini wanafundishwa kutumia mfumo wa umwagiliaji na mbinu nyingine za kuhifadhi maji ikiwa na mpango wa kukabiliana na ukame.
Chuwa ni miongoni mwa wakulima 25 walioanza kutumia technolojia hiyo, inayotoa maji kiasi kinachohitajika tu, na kupunguza matumizi ya maji kwa asilimia 75 na kupunguza upotevu wa maji kwa njia ya mfuke.
Nguluma Mbaga, afisa ugani wa Kikavu Chini amesema teknolojia hiyo imekuja muda muafaka huku wakulima wakijaribu kutafuta njia ya kukabiliana na ukame na madhara mengine yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi.
Ilan Bar, mtaalam wa kilimo mstaafu anayefanya kazi kwa kujitolea katika mradi huo, amesema wakulima wengi walioanza kutumia njia ya matone kumwagilia wanaiona ni nyepesi na yenye manufaa makubwa.
“Naamini wakulima watakuwa na nafasi nzuri kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Kijiji hiki kipo kwenye eneo kame lisilopata mvua za kutosha hivyo wakulima hawana budi kutumia maji kwa busara,” alisema.
Ufoo Adonikamu, Mratibu wa program wa Catholic Relief Services, amesema shirika hilo linalofadhiliwa na Shirika la maendeleo la marekani (USAID), linafanya kazi bega kwa bega na mashirika mengine na taasisi za serikali kuhakikisha vifaa vya umwagiliaji wa matone vinawafikia wakulima sehemu nyingine za nchi.
Kwa sasa Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya umwagiliaji 39 kwenye hekari 16,710, kwa kutumia teknolojia ya matone kwa gharama ya Shilingi 667.5 billion (karibu dola milioni 400), kwa mujibu wa wizara ya kilimo chakula na ushirika.
Wachambuzi wa mambo wanasema nchi ina nafasi nzuri ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa kilimo chake ni cha utegemeaji mvua. Hata hivyo, kuweka mifumo ya kilimo cha umwagiliaji endelevu kunahitaji uwekezaji mkubwa.
“Ni lazima utilie maanani mzigo wote wa sababu za kijiografia na za kilimo kuifanya miradi ya kilimo cha umwagiliaji iwe endelevu,” alisema Makarius Mdemu, mkufunzi kitengo cha udhibiti wa maliasili chuo kikuu cha ardhi, Dar es Salaam.
Bunge la Tanzania mwaka jana lilipitisha sheria ya umwagiliaji yenye lengo la kulinda wakulima dhidi ya athari za mabadiliko ya tabia nchi na pia kuwasaidia wakulima kutumia umwagiliaji kuzalisha chakula zaidi, na kuondoa umaskini
Sheria hiyo mpya inayoruhusu wakulima kupanua shughuli zao kwenye maeneo yanayomilikiwa na serikali iwapo watatumia kilimo cha umwagiliaji endelevu, pia inaruhusu kuanzishwa mfuko wa maendeleo ya umwagiliaji kusaidia skimu mbalimbali zinazokabiliwa na matatizo ya fedha.
Kilimo ni uti wa mgongo wa taifa. Kinachangia zaidi ya robo ya pato la wastani (GDP,) kutoa asilimia 85 ya mauzo nje na kuajiri takribani asilimia 80 ya watanzania wote wenye uwezo wa kufanya kazi.
Nchi ina hekari milioni 29.4 million za ardhi inayofaa kumwagiliwa, kati yake ni ekari 589,245 tu zinazomwagiliwa kwa sasa, kwa mujibu wa wizara ya kilimo chakula na ushirika.
Mwandishi Kizito Makoye, Mhariri Laurie Goering.