Farmers are breeding catfish in "home dams" that capture rainwater, helping them cope with water scarcity
Na Isaiah Esipisu
MBEERE, Kenya (Thomson Reuters Foundation) – Wakulima katika maeneo kame za mashariki na kaskazini mwa Kenya wamegundua mbinu ya kuendelea kufanya biashara hata maji yanavyozidi kudidimia, kwani sasa wanafuga samaki aina ya kambale.
Sylvester Kinyori asema kuwa hiki ndicho chanzo cha mapato yake siku hizi. Bwana huyo mwenye miaka 32 anaendesha kioski katika mji wa Isiolo ambapo anauza bidhaa za samaki kutoka kwa wakulima wa eneo hilo ambao wamegeukia ufugaji samaki.
Kinyori, ambaye ni mzaliwa wa Turkana, eneo la wafugaji kaskazini mashariki mwa Kenya, sasa anaendesha maisha kwa kuuza minofu ya samaki zilizopikwa pamoja na mayai, na mikate.
Wakulima wadogowadogo walianza kufuga samaki katika maeneo haya miaka nne zilizopita, baada ya shirika moja la kibinadamu kuwaonyesha njia rahisi ya kutega maji ya mvua katika mabwawa ya kinyumbani.
Maji hayo huwekwa katika mabwawa yaliyochimbwa katika boma, na yameundwa kwa kutumia karatasi la plastiki nzito ili kuzuia maji kumezwa na mchanga.
Mbinu hii ilianzishwa na wenyeji wa Yatta mashariki mwa Kenya ambao walijumuika pamoja ili kutafuta mbinu za kuepuka kutegemea misaada, ijulikanayo kama Mwolio, katika lugha ya Kikamba.
Baada ya mafanikio ya kutema misaada mnamo mwaka wa 2009, shirika la ActionAid Kenya liliamua kueneza mbinu hizo kwa wakaazi wengine kote mashariki na kaskazini mashariki mwa Kenya.
Sehemu hizo ni kame, ambapo wakati mwingine hupokea mvua iliyo chini ya milimita 150. Sehemu hizo zina mito za msimu, nyinginezo ambazo hufurika kwa masaa machache tu, baada ya mvua kubwa, huku ikiwalazimisha akina mama kuchimba visima katikakati mwa mito ili kutega maji yaliyonaswa chini ya mchanga.
Uchanganuzi wa mwenendo wa hali ya hewa, uliochapishwa na serikali ya Marekani mnamo mwaka wa 2010 ulionyesha kuwa mvua iliendelea kudidimia katika maeneo ya kati yanayozalisha chakula tangu miaka ya 1960.
Pia, ripoti hiyo ilitabiri kuwa sehemu kubwa ya nchi huenda ikapungukiwa na mvua kwa kiwango cha milimita 100 katika misimu ya mvua nyingi ifikiapo mwaka wa 2025. Pia, ilibainika kuwa joto liliongezeka kwa nyuzi moja tangu mwaka wa 1975.
Hilo basi, linasisitiza umuhimu wa wakulima kuweka juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Iliponyesha mnamo mwaka wa 2012 katika maeneo ya Kitui na Isiolo, jamii kadhaa ziliweza kutega maji katika mabwawa ya kinyumbani. Hapo ndipo waliamua kuanza ufugaji wa samaki katika mabwawa hayo.
John Njiri, mkaazi wa kijiji cha Mashamba kule Mbeere alisema kuwa karibu wakulima wote walitangulia na ufugaji wa samaki aina ya perege, ambayo imepigiwa debe mno na serikali kuonyesha kuwa hiyo ndio aina ya samaki iliyo bora zaidi kufuga nyumbani.
Lakini, mavuno yake hayakuridhisha, huku ikiwalazimisha wakulima hao kubadilisha mbinu iliponyesha mvua tena mnamo mwaka wa 2014.
Njiru asema kuwa, wakulima wote waliamua kufuga samaki aina ya kambale, kwani wale waliojaribu ufugaji wa samaki huyo mnamo mwaka wa 2012 waliridhishwa zaidi ya wale waliofuga perege.
Mnamo mwaka wa 2015, wale waliofurahia mavuno ya kambale walipata motisha ya kuegeza zaidi wakati mvua ya masika isiyotarajiwa iliponyesha mnamo mwezi wa Septemba mwaka jana.
Njiru asema kuwa kutokana na majaribio ya wanavijiji, samaki aina ya kambale, ambao wana aina ya mikia katika sehemu za midomo wamedhihirisha uwezekano wa kustahimili hali ngumu ya hewa ikilinganishwa na samaki aina ya perege.
Bwana huyo aliambia shirika la Thomson Reuters Foundation kuwa wanafurahia kwani wanaweza kula samaki sasa. Alisema kuwa, ni matumaini yake kuwa ufugaji wa samaki katika maeneo hayo utadumu, ikizingatiwa hali ya hewa inayozidi kubadilika.
Samaki aina ya kambale aliyekomaa huuzwa kwa shilingi mia tano za Kenya katika masoko ya maeneo hayo. Ili kuwanenepesha, wakulima wengi hulisha samaki hao kwa samaki aina ya perege.
Wakati huohuo, mahitaji ya samaki wadogo wa kufuga wa aina ya kambale yameletea wenyeji biashara. Rhoda Mwende mkaazi wa kijiji cha Kanyonga katika jimbo ndogo la Mbeere amejifunza mbinu za kipekee za kuzalisha samaki wa kufuga.
Mama huyo mwenye watoto watatu, ambaye miaka tano zilizopita alitegemea chakula cha misaada, aliuza samaki hao wachanga wapatao 40,000 kwa wakulima wenyeji mnamo mwezi wa Septemba, hapo akajipatia shilingi 400,000.
Kutokana na msimu wa mvua nyingi wa mwezi wa Aprili, binti huyo aliuza zaidi ya samaki 80,000, na kujipatia shilingi 800,000.
Hivyo basi, ametumia pesa hizo kujinunulia shamba ekari moja na nusu, ambapo anaishi na wanawe, na pia mama yake.
Mwende amenakili utaratibu wa kuzalisha samaki wa kufuga, kuanzia kudunga samaki wa kike shindano ili kutoa homoni za kuzalisha mayai, kwa kufinya mayai hayo, kutoa mbegu za uzazi kwa samaki wa kiume, na hata kuunganisha mayai hayo na mbegu.
Ni jambo la kufurahisha kuona watu waliotegemea chakula cha misaada miaka michache zilizopita wakibadilisha maisha yao kwa kutumia mawazo yao wenyewe, asema Dinah Wambua, afisa wa ActionAid kule Makima, Mbeere.
Wakulima hao huvuna samaki kutoka mabwawa yao wakati kiwango cha maji kinapoanza kupunguka, na kisha wanasubiri wakati mvua iliyo nadra itakaponyesha tena, ili waweke samaki wengine wachanga.
Bwawa la nyumbani lililo na kina cha futi nane na futi 20 mraba laweza kubeba maji ya kusaidia familia ya watu wanane, na kunyunyiza kwa ekari moja ya shamba kwa mwaka mmoja, asema Njue Njangungi, afisa kiendelezi wa maswala ya kilimo katika kata ya Kyome Thaana, Mbeere.
Bwawa kama hilo laweza kukuza samaki kambale wachanga wapatao 1000.
Elizabeth Musyoka, mkaazi wa Kithambioni kule Kitui, mashariki mwa Nairobi asema kuwa mabwawa hayo ni ushindi mara mbili kwao.
Kwa hivi sasa tuko na maji, na pia watoto wetu wananufaika na vitoweo ambavyo huwapatia madini ya protini ambayo walikuwa wakikosa kila wakati, asema mama huyo.
Our Standards: The Thomson Reuters Trust Principles.